Mtoto aliyeokolewa tumboni mwa mama aliyeuawa Gaza afariki dunia

Israel. Mtoto aliyeokolewa kutoka tumboni mwa mama yake aliyekuwa mahututi baada ya shambulizi la anga la Israel kusini mwa Gaza amefariki dunia.

Mtoto huyo wa jinsia ya kike, aliokolewa akiwa hai kutoka tumbo la mwanamke wa Palestina aliyeuawa katika shambulio la Israel kwenye ukanda wa Gaza.

Mtoto Sabreen al-Sakani alizaliwa kupitia upasuaji katika Hospitali ya Rafah muda mfupi baada ya saa sita usiku Jumapili Aprili 21, 2024.

Katikati ya matukio ya machafuko madaktari walimfufua mtoto, kwa kutumia pampu ya mkono kupeleka hewa kwenye mapafu yake.

Kwa mujibu wa BBC, mtoto huyo alifariki dunia Alhamisi Aprili 25 na amezikwa karibu na mamake yake.

Mtoto Sabreen alikuwa miongoni mwa watoto 16 waliouawa katika mashambulizi mawili ya anga huko Rafah mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wote waliuawa katika shambulio la bomu lililolenga nyumba walimokuwa wakiishi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, shambulio hilo lililotekelezwa usiku katika Mji wa Rafah liliwaua raia wa Palestina wapatao 19.

Kati ya raia19 hao, watoto 13 kutoka familia moja waliripotiwa kuangamia kwenye shambulio hilo.

Mtoto huyo wa kike alisemekana kuwa na uzani wa kilogram 1.4 na aliokolewa kupitia upasuaji wa dharura baada ya waokoaji kubaini kwamba mama yake alifariki akiwa na ujauzito wa wiki 30.

Usimamizi wa Hospitali ya Rafah ulisema mtoto huyo atakuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi cha wiki 3 hadi 4 kabla ya kuangalia mchakato wa kuruhusiwa kutoka hospitali.

“Baada ya kipindi hicho tutaangalia jinsi mtoto huyu ataondoka na atakwenda wapi, iwe kwa familia, kwa wajomba zake au hata babu na bibi. Hapa ndio kuna huruma zaidi, hata kama mtoto huyo alisalimika, alizaliwa akiwa yatima tayari,” daktari alisema.

Vita baina ya Jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza vimeendelea tangu Oktoba 2023.

Inaarifiwa zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza ambao ni takribani milioni 2.3 wametorokea katika Mji wa Rafah kutafuta hifadhi dhidi ya mashambulizi ya Jeshi la Israel

Related Posts