Dodoma Jiji yaizamisha KMC, yapaa kibabe

BAO la Paul Peter limetosha kuipandisha Dodoma Jiji kwa nafasi tatu juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kutoka nafasi ya 10 hadi ya nane baada ya kufikisha pointi 28.

Bao la Peter lililofungwa kipindi cha kwanza na kudumu hadi dakika zote 90 za mchezo, limeifanya Dodoma Jiji kukusanya pointi zote sita kwa KMC ambao pia walikubali kichapo cha mabao 2-1 Novemba 3, 2023 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amesema ushindi walioupata unampa matumaini ya kubaki msimu ujao huku akimwaga sifa kwa wachezaji wake kuwa ni wapambanaji ambao anaamini wataibakiza timu Ligi Kuu msimu ujao.

“Haikuwa rahisi, nawapongeza vijana wangu kwa kupata matokeo katika mchezo huu na matokeo hayo yanatupa mwanga wa kuona namna gani tutakuwa bora katika mechi zijazo ili tuweze kubaki msimu huu,” amesema.

Kocha wa KMC, Abdihamid Moalin amesema wamesahau matokeo yaliyotokea wanasonga mbele kwa kuweka umakini kwenye mechi sita zilizobaki.

“Tumepoteza mchezo sasa tuna tunaangalia namna gani tunapata matokeo kwenye michezo sita iliyobaki, lengo ni kuhakikisha tunafikia mikakati ya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu,” amesema.

KMC pamoja na kufungwa imeendelea kusalia katika nafasi ya saba ikikusanya pointi 32 baada ya kucheza mechi 24 huku Dodoma Jiji ikifikisha pointi 28 na kukaa katika nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 23.

Mechi zinazofuata kwa timu zote mbili Dodoma Jiji itakuwa ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate Mei 4 huku KMC ikiikaribisha Kagera Sugar.

Related Posts