Wizi wa miradi ya Serikali Geita, Shinyanga, Katavi, Singida, Mtwara balaa

Mwanza. Vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma vimeendelea kuwa kitendawili, baada ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kubaini kasoro katika matumizi ya mabilioni ya fedha kwenye mikoa mitano.

Mikoa iliyoguswa na ripoti hiyo ya utendaji kazi wa Takukuru kwa Aprili hadi Juni mwaka huu ni Geita, Shinyanga, Katavi, Singida na Mtwara, ambayo katika miradi tofauti imebainika kuuingia mtego huo.

Hali hiyo inaendelea licha ya viongozi mbalimbali akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan kukemea hadharani suala la rushwa huku wakielekeza usimamizi thabiti wa fedha za umma.

“Fedha nyingi tunazileta fedha zinaliwa, zinaharibiwa mnaangalia tu, hakuna uchunguzi hakuna kinachoendelea hadi viongozi waje waseme hapa kafanye uchunguzi, hapa msimamishe, hapa fanya hivi hatuendi hivyo ndugu zangu.

“Niwaombe kwamba miradi inayoletwa huku ni ya kwenu, mimi na mawaziri wangu tunatoka maeneo tofauti na sisi tunapiga kelele huko kwetu kama mambo hayaendi kwa hiyo inayokuja huku ni ya kwenu simamieni,” alisema Rais Samia Februari 6, 2022 wakati akiangalia maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara.

Hata hivyo, ilichokibaini Takukuru kwenye mikoa hiyo ni sawia na kile kilichopo katika ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2022/23, makusanyo ya Sh6.18 bilioni yaliyokusanywa kupitia mashine za POS hayakuwasilishwa katika akaunti za benki za mamlaka 96 za Serikali za mitaa.

Pia, kwa mujibu wa CAG, sehemu za huduma za afya na vifaatiba vilivyonunuliwa vyenye thamani ya Sh4.94 bilioni havitumiki jambo linaloisababishia Serikali hasara.

Katika Mkoa wa Shinyanga, Takukuru ilimfikisha mahakamani Meneja wa Chama cha Ushirika Kahama (Kacu), Abduly Mauga kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kadhalika, imewaburuta mahakamani vongozi wanane wa vyama vya msingi Kangeme na Mshindi mkoani humo kwa tuhuma za rushwa.

Kati ya kesi tano zilizofunguliwa mahakamani, nne zinaendelea na moja Jamhuri imeshinda huku wahusika wakiamriwa kurejesha Sh24 milioni waliyoipata kwa rushwa.

Hayo yalibainika baada ya uchunguzi uliofanywa na Takukuru katika chama hicho, kinachojishughulisha na kilimo cha tumbaku, pamba na mazao mchanganyiko.

Ilibainika vyama vya msingi 13 vinavyosimamiwa na Kacu vinadaiwa madeni na wanachama wake, huku Mauga akitajwa kuhusika.

“Tulibaini kuna viongozi wanakopa fedha benki na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi, kughushi ankara za malipo, kutoa fedha kwenye akaunti za chama na kuzigawana na kufanyika kwa malipo yasiyo halali kwa madai ya kulipa wafanyabiashara walioleta ya pembejeo kwenye Amcos,” amesema Donasian Kessy,  Mkuu wa Takukuru Shinyanga.

Amesema hadi Julai 31, mwaka huu wahusika katika kesi ambayo jamhuri ilishinda walisharejesha Sh12 milioni.

Takukuru mkoani Geita imeanza uchunguzi wa upotevu wa vifaa vyenye thamani ya Sh1.7 bilioni katika mradi wa awamu ya pili wa ujenzi wa Hospitali ya Katoro.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Alex Mpemba amesema walibaini vifaa hivyo vilinunuliwa lakini havijawahi kutumika na havipo kwenye eneo la mradi.

Wakati huohuo, taasisi hiyo inachunguza ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Shule ya Msingi Nyamiboga inayojengwa kwa Sh27 milioni ambayo haijawekewa mashimo ya choo na mfumo wake.

Hayo yamefanyika, wakati vifaa vipo eneo la mradi na hadi sasa shughuli zimekwama kutokana na upotevu wa Sh7 milioni.

Kuhusu ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, Mpemba amesema kati ya miradi 25 yenye thamani ya Sh10.2 bilioni iliyokaguliwa, miradi mitano ilikutwa na upungufu.

Mkoani Mtwara, Takukuru imebaini upungufu katika ujenzi wa msingi wa vyumba vinne vya madarasa vya Shule ya Msingi Litehu wilayani Tandahimba unaogharimu Sh80 milioni.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Elisante Mashauri amesema ilibainika matofali yaliyotumiwa yalikuwa chini ya kiwango, hivyo kupindisha msingi.

Mbali na msingi huo, Mashauri amesema taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi 18 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh4 bilioni katika sekta ya elimu miradi  ni tisa, afya (5), ujenzi (2), maliasili (1) na kilimo mmoja.

“Miradi 14 sawa na asilimia 94.44 yenye thamani ya Sh2 bilioni imebainika kuwa na upungufu mdogo mdogo,” amesema Mashauri.

Katika hatua nyingine, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi, Stewart Mwakakyondo amesema Sh150 milioni kati ya Sh300 milioni zilizokusudiwa kulipwa kwa mzabuni wa utengenezaji samani za Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kinyume na mikataba zimeokolewa.

Mwakakyondo amesema halmashauri hiyo ilitaka kumlipa mzabuni asilimia 50 kinyume na utaratibu jambo ambalo lingesababisha upotevu wa fedha hiyo.

Amesema Takukuru baada ya kushinda kesi ya uhujumu uchumi 4002/24, dhidi ya mzabuni wa ukusanyaji wa ushuru kwa kutumia mashine za POS wilayani Mpimbwe Mkoa wa Katavi, Mahakama ilimuamuru kurejesha Sh20.3 milioni zilizotaka kupigwa na mkusanya mapato huyo.

Wakati huohuo, Takukuru imewalazimisha wasimamizi wa mradi wa matengenezo ya viti na meza 30 katika Shule ya Sekondari Kamalampaka wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, kurejesha Sh1.9 milioni baada ya kutengeneza samani hizo chini ya kiwango.

Mkuu wa Takukuru mkoani Singida, Sipha Mwanjala ameeleza kufikishwa mahakamani kwa baadhi ya watumishi kutokana na matumizi mabaya ya madaraka na kughushi nyaraka.

Kati ya watumishi hao kwa mujibu wa Takukuru, yumo ofisa elimu mkoa na ofisa michezo na utamaduni mkoa, kadhalika maofisa wengine wa kada ya elimu wa Manispaa ya Singida.

Mwanjala amesema katika kipindi cha miezi mitatu wameokoa Sh136 milioni zilizotokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika fedha hizo, amesema Sh18.8 milioni zimeokolewa katika Halmashauri ya Mkalama na Sh1.9 milioni zimeokolewa katika Halmashauri ya Itigi huku Sh1.1 milioni zikiokolewa Halmashauri ya Iramba.

Amesema Takukuru imepokea malalamiko 55 huku 20 yakihusu vitendo vya rushwa na uchunguzi unaendelea.

“Kesi tatu zilifunguliwa mahakamani, kesi tano ziliamuliwa kati ya hizo kesi nne jamhuri ilishinda ikiwamo iliyotokana na maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa alipofanya ziara katika Wilaya ya Manyoni na kesi moja ilishindwa,” amesema Mwanjala.

Kutokana na taarifa hizo, Mkazi wa Katoro mkoani Geita, Bakari Masanja amependekeza uchunguzi uendelee ili mengi zaidi yabainike.

“Wananchi waliaminishwa sana kwenye ujenzi wa hospitali hii (Katoro), lakini kutokamilika kunawafanya wakose imani na viongozi wao. Uchunguzi huu uende mbele uje na majibu ya lini miradi itakamilika,” amesema Masanja.

Mwanazuoni wa Uchumi, Profesa Samuel Wangwe amesema vitendo hivyo vinasababishwa na kukosekana uwajibikaji kwa viongozi wengi wa ngazi za halmashauri.

Kukosa uwajibikaji huko, amesema kunawafanya wengi washindwe kusimamia bajeti kama ilivyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.

“Kunapaswa kuwe na usimamizi mzuri wa bajeti na kuwe na utaratibu wa kuhuisha matarajio ya matumizi hii itawezesha kuepuka upigaji,” amesema Profesa Wangwe.

Kadhalika, amependekeza kwenye vigezo vya upimaji ufanisi matumizi ya fedha hizo za umma kiwe kimojawapo na kisimamiwe ipasavyo.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema kukosekana ukali wa sheria ndiyo sababu ya kuendelea kwa vitendo vya upigaji katika fedha za umma.

Amesema adhabu ya kufanya kosa la wizi serikalini mara nyingi ni ndogo zaidi ya wizi uliofanyika.

“Watumishi wanapiga hesabu akiiba Sh1 bilioni sheria itamuadhibu pengine kwenda mahakamani na kutozwa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi kadhaa na wakati mwingine kuondolewa kwenye nafasi yake.

“Kwa hesabu za haraka haraka adhabu hiyo ni faida kwa kiasi alichoiba, kwa hiyo yeyote yule anaona bora aibe afungwe kisha atoke atumie,” amesema Profesa Kinyondo.

Amesisitiza matukio yote ya upigaji yanachochewa na faida zilizopo katika kuiba badala ya hasara.

“Watu hawataacha kuiba kwa sababu wanafaidika kwenye wizi kuliko wakiacha kwa kuwa sheria zetu sio kali katika wizi, Takukuru na CAG wataendelea kuibua madudu lakini hakutakuwa na matokeo yoyote,” amesema Profesa Kinyondo.

Katika maelezo yake, ametolea mfano sheria za Jamhuri ya China kuhusu wizi wa fedha za umma, akisema ukipelekwa leo mahakamani kesho unahukumiwa kunyongwa.

(Imeandikwa na Mgongo Kaitira (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Florence Sanawa (Mtwara) na  Jamaldini Abuu (Singida)

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts