Katika hali isiyo kuwa ya kawaida, kijana Edward Futakamba, mkazi wa Mpanda mkoani Katavi amejikuta akifanya sherehe ya harusi bila ya mwenza wake, ikidaiwa siku chache zilizopita familia ya bibi harusi ilighairi kufanyika kwa ndoa hiyo.
Imedaiwa kuwa vikao vya maandalizi ya wawili hao kuoana vilikuwa zimekamilika, pamoja na kutangazwa kanisani, hata hivyo kwasababu ambazo bado hazijawekwa wazi, bibi harusi mtarajiwa hakufika kanisani wala ukumbini.
Kamati ya harusi imesema Familia ya bibi harusi baada ya kuzuia ndoa hiyo kufanyika haikuweza kutoa sababu za msingi isipo kuwa walidai, katika sherehe ya kumuaga bibi harusi mtarajiwa yani “Send off” bwana harusi huyo alionekana kuchangamka sana huku sababu nyingine wakidai ni kutomalizia mahari ya shilingi laki mbili kati ya ile waliokubaliana.
Hali hiyo iliwafanya kuandaa sherehe ambayo imefanyika katika ukumbi wa kichangani uliopo manispaa ya Mpanda lengo ni kuwafurahisha watu waliotoa michango yao.
Edward Futakamba ambaye alikuwa bwana harusi anasema anamshukuru mungu kwa yote yaliotokea kwani kupata na kukosa yote ni sehemu ya maisha.
“Sababu ya msingi hasa Kuzuia ndoa mpaka sasa sijajua upande wa bibi harusi ndio wanajua ila nachojua Mimi walienda tu kanisani kama familia wakiwa mama,mama mdogo,baba mdogo na ndugu wengine kwaajili ya kusitisha zoezi la ndoa.
“Kwakweli tumepata hasara watu walikua wameandaa kila kitu,gauni na mapambo yote ya bibi harusi yamegharimu thamani ya laki tano gauni bado lipo nyumbani hadi sasa hivi.
“Watu wamekubali kuandikisha mafundisho zaidi ya siku 90 alafu unakuja unasema hapana bado siku kama nne mbele baada ya kufanya Send of ni kitu ambacho hakileti picha nzuri kama kulikua na changamoto wangesema ila Mimi namshukuru mungu”