Dodoma. Baada ya malalamiko ya wafanyakazi kuhusu kanuni mpya za kikokotoo cha mafao ya mkupuo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema limewasilisha maoni kwa Serikali na bado majadiliano yanaendelea.
Kanuni mpya za mafao ya mkupuo zilianza kutumia Julai 2022 ambapo mafao hayo kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii ni asilimia 33.
Tucta inakuja na kauli hiyo siku chache baada ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU), kutoa taarifa ya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya hoja za pensheni.
Mjadala wa kikokotoo hicho umeendelea kutawala ndani na nje ya Bunge na hivi karibuni katika ziara zao mikoani Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-bara, Abdulrahman Kinana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi walikumbana na kero hiyo.
Kinana akiwa mkoani Mara baada ya kueleza suala hilo katika moja ya mikutano yake alisema chama hicho kimesikia kilio hicho, akiahidi litatafutiwa ufumbuzi.
Katika mkutano wake na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Vijijini Aprili mwaka huu, Kinana alisema: “Mimesikia sana hii habari ya kikokotoo kinapigiwa kelele nchi nzima.
“Lakini jambo moja ambalo nadhani limetamkwa rasmi hadharani na Katibu Mkuu wa Chama ndugu Nchimbi ni kwamba jambo hili atalifikisha kwa Mwenyekiti Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Dk. Samia Suluhu Hassan),” alisema.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 26, 2024, Katibu Mkuu wa Tucta, Heri Mkunda amesema Tucta ilishiriki katika kutengeneza kanuni hizo lakini sasa miaka miwili tangu utekelezaji uanze umeonekana haukidhi matarajio ya watu.
“Kuna watu katika utekelezaji wameshakutana nayo, wameona hali halisi. Watu wengi wametoa malalamiko na kilio kikubwa kwa Serikali na kwa mifuko yenyewe,” amesema.
Kwa mtazamo wa Mkunda, ni wakati muafaka kwa Serikali na mifuko kuona wanavyowea kuzingatia malalamiko ya watu na ninaamini Serikali inasikia.
Hata hivyo, amesema wameshawasilisha maoni yao kwa Serikali, wameshakaa kwenye majadiliano na bado wanaendelea na majadiliano kutokana na hali ilivyo katika ngazi ya chini.
“Tunasubiri huenda Serikali inaweza kusema kitu kutokana na matokeo ambayo yameshaonekana. Kwa sababu baada ya kuunganisha mifuko ni miaka mitano imepita na tumeona afya (uhimilivu) ya mifuko imeongezeka,” amesema.
Amesema ni wakati sasa wa kulitazama jambo hilo, ingawa kanuni zinasema kuhuisha kutafanyika kila baada ya miaka mitatu.
Lakini, amesema mabadiliko yoyote yatakayofanyika kuhusu mafao ya wastaafu yazingatie uendelevu wa mifuko.
Kuhusu utoaji wa maoni kuhusiana na kanuni hizo, Mkunda ameshauri Serikali na mifuko ya hifadhi ya jamii kuweka mazingira kupokea maoni ya mtu binafsi au taasisi lakini awali kabla ya kupitishwa fursa ya kutoa maoni yalikuwepo kama wanaweza kuyafanyia kazi basi wafanye hivyo.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leya Ulaya amesema wako katika kikao cha kupitia mambo mbalimbali na hawajafikia uamuzi wa nini wanafanya kuhusiana na kikokotoo.
“Hatujafikia (uamuzi) wa nini tunafanya na ndio maana nasema utupe muda. Maana tuna namna ya kufanya,” amesema Ulaya.
Katika uchambuzi wa THTU wamebaini maeneo yenye ukakasi, madhara yake na hivyo kuja na mapendekezo ya kuzitatua ili kuepusha kuathiri haki za wafanyakazi kupata stahiki husika pindi anapostaafu.
THTU imetaja changamoto hizo ni kikokotoo kinachotumika kutokidhi hali halisi ya wanachama, ushirikishwaji hafifu katika kujadili kiwango cha michango ya wanachama na wanachama kupunjwa mafao kwa kosa la mwajiri.
Nyingine ni ukokotoaji mbovu wa mafao kwa wenza, malipo yanayobagua watoto ambao ni wategemezi kwa mwanachama aliyefariki dunia na uwepo wa mafao tofauti katika mfuko mmoja na ukokotoaji wa mafao kwa kutumia ‘special lump sum’
Akizungumza Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk Paul Loisulie amesema vikwazo vilivyopo kwenye mfuko huo na pensheni vinaathiri haki ya mfanyakazi kupata stahiki husika pindi anapostaafu.
Amesema tangu kufanyika kwa marekebisho ya kanuni za mafao kwa wastaafu kumeibuka mijadala kinzani miongoni mwa wanajamii ya wafanyakazi ambao ndio wachangiaji wakubwa wa mifuko husika.
“Malalamiko hayo yamejengeka katika misingi miwili mikubwa. Msingi wa kwanza unatokana na utoaji wa mafao au huduma zisizozingatia mahitaji na uchumi wa wachangiaji na wategemezi wao,”amesema.
Ametaja msingi mwingine wa hoja za wanajamii na wafanyakazi ni uwajibikaji usioridhisha kwa upande wa uendeshaji na menejimenti ya mifuko husika kunakosababisha hali ya ukwasi wa mifuko kuwa mashakani.
Amesema katika utekelezaji wa majukumu yake na kwa manufaa ya wafanyakazi wote Tanzania, THTU iliunda kamati maalumu ili kuweza kupitia nyaraka mbalimbali zikiwamo sheria, kanuni na miongozo na kuandaa tamko hilo la kitaalamu, lengo likiwa ni kuishauri Serikali.
Ameitaka Serikali kuangalia hoja hizo saba walizoziainisha na kufanyia marekebisho ili kuondoa malalamiko yanayoweza kusababisha kukosekana kwa utulivu kwenye maeneo ya kazi na kwa jamii nzima.
Wakati wa mjadala bungeni wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri mkuu na taasisi zilizochini yake, wabunge walibana Serikali na kuitaka kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwani imekuwa kero inayolalamikiwa na watumishi wengi.
Baadhi ya wabunge waliochangia suala hilo ni Esther Bulaya, (viti maalumu) Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Kasali Mageni (Sumve), Joseph Musukuma (Geita Vijijini), Florent Kyombo (Nkenge), Dk Pius Chaya (Manyoni Mashariki) na Mwita Waitara (Tarime Vijijini).
Wabunge hao walitaka Serikali kukaa na wafanyakazi kuirejesha sheria hiyo bungeni ili iweze kufanyiwa marekebisho.
“Kwa uelewa wangu kama daktari wa akili, ninaona tunakwenda kutengeneza Taifa la watumishi wezi kwa sababu (wafanyakazi) wanalalamika kila siku suala la kikokotoo. Mimi sijasoma sana lakini nikiangalia mtu anapata asilimia 30 halafu 70 unamtunzia,” alisema Musukuma, katika mchango wake bungeni.
Hata hivyo, akihitimisha hoja ya bajeti yake, Aprili 15,2024, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imesikia ushauri, maoni na kupokea maoni mbalimbali kupitia wadau wakiwemo wabunge, wafanyakazi na vyama vya waajiri na wafanyakazi wenyewe.
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wafanyakazi wanaostaafu na itaendelea kufanya tathimini kwa kuzingatia sheria za kazi.
Aprili 19 mwaka huu, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi alisema suala la kanuni hiyo lina maelekezo ya Rais Samia na limeanza kufanyiwa kazi na majibu yatajulikana kwenye sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani itakayofanyika jijini Arusha.
Aprili 16, 2023 akiwa ziarani Rukwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliahidi kufikisha kilio hicho kwa Rais Samia ili kitafutiwe ufumbuzi kwa kuwa ni kero kubwa kwa wastaafu.
“Tatizo la kikokotoo linalalamikiwa sana na watumishi, imekuwa kero kubwa, kuna muda lazima tuangalie wananchi wetu, wanachama wetu, tuangalie tutafika wapi, lakini kwa kadri inavyowezekana tunapaswa kutatua kero za wananchi,” alisema Dk Nchimbi.