Mahakama Kuu yabatilisha uuzaji viwanja vya Hans Poppe

Tanga. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam, imebatilisha uuzaji wa viwanja viwili na vingine vilivyokuwa vinatakiwa kuuzwa, vilivyokuwa vinamilikiwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na pia mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Soka ya Simba, Zacharia Hans Poppe, baada ya kubaini uuzaji huo ulikuwa batili.

Mahakama imefikia uamuzi huo katika hukumu yake iliyotolewa Julai 31, 2024 na Jaji Elinaza Luvanda, katika kesi za ardhi  namba 104 iliyounganishwa na 105 zote za mwaka 2023 zilizofunguliwa na wasimamizi wa mirathi ya Hans Poppe, dhidi ya Benki ya Africa (BoA)  na Kampuni ya udalali ya Bilo Star Dept Collector.

Waliofungua kesi hizo ni Aldo Hans Poppe mdogo wa marehemu Zacharia, Angel Zacharia na Abel Zacharia ambao ni watoto wa marehemu (Zacharia).

Wote kwa pamoja walikuwa wakipinga uamuzi wa BoA kuuza viwanja hivyo kupitia kampuni hiyo ya udalali.

Katika kesi hizo walalamikaji walikuwa wanaomba Mahakama itamke kuwa mnada wa uuzwaji wa viwanja hivyo viliyowekwa dhamana ya  mkopo aliouchukua baba yao ulikuwa batili na haukuwa na uhalali wa kisheria kutokana na  notisi ya kisheria ya siku 14.

Viwanja hivyo ni namba 163 na 165 vilivyopo eneo la Ununio na nyumba namba 10 na  kiwanja namba 1057, kitalu ‘L’ Mbezi beach zote zikiwa Wilaya ya Kinondoni.

Katika hukumu hiyo ambayo nakala yake inapatikana katika tovuti ya mahakama. Mahakama mekubaliana na wadai na kutoa amri ya kubatilisha uuzwaji wa viwanja hivyo.

Lakini haijakubaliana na ombi la fidia ya Sh2 bilioni waliyokuwa wameomba wasimamizi hao wa mirathi ya Zacharia, baada ya kushindwa kubainisha kwa nini wanastahili kupewa fidia hiyo.

Kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu ukiwamo wa wa shahidi wa kwanza kutoka benki hiyo, alidai  Septemba 2011 na Machi 2014 Zacharia Hans Poppe (marehemu) kupitia kampuni za Z.H Poppe na Hans Pope Hotels zilikubaliwa na benki kuhusu mkopo.

Mkopo huo kulingana na barua yenye Kumbukumbu namba  PDO/CDT/cwl/781/11 ya Septemba 9,2021, ulikuwa wa Dola 700,000 za Marekani (Sh18,200,000,000) na Dola 2 milioni za Marekani (Sh520,000,000) .

Kulingana na barua nyingine yenye kumbukumbu namba  PDO/CDT/ern/0182/14 ya Machi 3,2014 mali zilizowekwa  kwa ajili ya dhamana ya mkopo huo ilikuwa ni nyumba namba 10, kiwanja namba 1057 kitalu L, chini ya hati ya umiliki namba 1131196/2 Mbezi Manispaa ya Kinondoni.

Nyingine zilikuwa ni viwanja namba 163 na 165, CT 45369/1 na kwamba, Zacharia Hans Poppe t/a Z.H. Poppe Co. ilibadilisha aina yake ya biashara kutoka umiliki wa pekee hadi kampuni ya dhima ndogo iliyopewa jina la Z.H. Poppe Limited.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Aldo (mmoja wa wasimamizi wa mirathi), hadi Novemba 26, 2019 ilionesha mkopo wa Dola 646,000 za Marekani (Sh1,679,600,000) za Kampuni ya Z.H, Poppe ulifanyiwa marekebisho na mkopaji alitakiwa kuilipa ndani ya miezi 15.

Alidai Novemba 2021 benki hiyo  walipokea barua kutoka kwa wakopaji zikimtaarifu kufariki kwa Zacharia Hans Poppe ambaye alikuwa mdhamini, mkurugenzi mkuu na mbia kwenye kampuni mbili zilizokopa.

Shahidi huyo wa kwanza upande wa wadai, alidai barua iliyotajwa ilieleza zaidi kwamba wakopaji wanafahamu kuhusu mali zilizowekwa dhamana na familia ya marehemu ipo kwenye majadiliano na mchakato wa kumteua msimamizi.

Aldo alitoa hati ya kifo ikionesha Zacharia Hans Poppe alifariki dunia Septemba 10,2021 na uamuzi wa Septemba 23,2022 ikiwaonesha wote watatu ni wasimamizi wa mirathi ya marehemu Zacharia.

Wakihitimisha ushahidi wao, wadai walidai kuwa wadaiwa, wakiongozwa na Benki ya BOA, walikosoa mchakato wa mnada kwa kuwa na taratibu zenye dosari.

 Wadai walidai kuwa hawakupewa notisi ya siku 60 kama inavyotakiwa, na pia wadaiwa walishindwa kutii matakwa ya notisi ya lazima ya siku 14 kabla ya kufanyika kwa mnada au mauzo yoyote.

Katika kesi hii, walalamikaji walidai kuwa mnada au mauzo yaliyofanyika kwenye mali yao hayakuwa halali kwa sababu hawakupatiwa notisi ya lazima ya siku 14 kabla ya mnada huo.

Walidai kuwa ununuzi uliofanywa na mtu wa tatu ni batili kwa kukosa uhalali wa hati miliki na kukiuka mchakato wa lazima wa uuzaji.

Kwa upande wa wadaiwa, walieleza kuwa, baada ya marekebisho ya mkataba mkopaji alishindwa kulipa, na benki ilitoa notisi ya siku 60 kwa walalamikaji.

Baada ya notisi hiyo kuisha, waliiagiza kampuni ya Bilo Star Debt Collector kuondoa mali ili kurejesha mkopo.

Bilo alitoa notisi ya mnada Machi 14, 2023, katika gazeti, na mnada huo ulipangwa kufanyika Machi 28, 2023, ingawa haukufanyika na badala yake ulihamishwa hadi Aprili 19, 2023.

Katika uamuzi wake, Jaji Luvanda alieleza kuwa hoja muhimu zilikuwa ni iwapo benki ilitoa notisi ya siku 60 kwa walalamikaji, na ikiwa mnada au mauzo ya mali husika yalikuwa halali.

Katika hoja ya kwanza, walalamikaji walidai kuwa saini zao kwenye notisi zilighushiwa. Hata hivyo, Jaji alieleza kuwa kughushi ni kosa la jinai na mzigo wa uthibitisho ni mkubwa zaidi katika kesi kama hizi.

Walalamikaji hawakuweza kutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yao ya kughushi.

Kuhusu mnada wa mali, Jaji alisema kumbukumbu zinaonyesha kuwa mali ya Mbezi pekee ndiyo iliombwa zabuni na Magreth Msanga alitangazwa mshindi wa zabuni hiyo kwa Sh140 milioni.

Walalamikaji walidai kuwa mnada huo ulifanyika chini ya notisi ya siku 14, lakini Jaji alieleza kuwa notisi fupi si sababu ya kubatilisha mnada, hasa kama mambo mengine ni sawa. Pia, walalamikaji hawakutoa ripoti ya uthamini ya thamani ya soko ya mali hiyo wakati wa mnada.

Jaji Luvanda alihitimisha kuwa mnada na zabuni ya mali ya Mbezi haiwezi kufutwa.

Hata hivyo, alikubaliana na walalamikaji kuwa umiliki wa mali hiyo utaathiri uuzaji wa mali nyingine huko Ununio, na kwa hivyo uuzaji wa mali hiyo haukuwa halali.

Related Posts