UONGOZI wa Tabora United uko katika mazungumzo ya kumuajiri aliyekuwa kocha wa Pamba na Coastal Union, Yusuf Chippo ili akawe msaidizi wa kocha mkuu Mkenya, Francis Kimanzi, ambaye muda wowote atatangazwa kuiongoza timu hiyo kwa msimu ujao.
Makocha hao ambao wote ni raia wa Kenya, wako katika hatua za mwisho za kukabidhiwa kikosi hicho ikiwa ni muendelezo wa maboresho ya benchi jipya la ufundi yanayoendelea ndani ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano mbalimbali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo alikiri kuwepo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo na moja ya klabu ya Ligi Kuu Bara ambayo hata hivyo hakutaka kuiweka wazi, huku akieleza mchakato utakapokamilika ndipo mashabiki watakapofahamu.
“Ni kweli niko Tanzania na niko katika mazungumzo na moja ya klabu zinazocheza Ligi Kuu Bara ambayo ningeomba nisiiweke wazi kwanza hadi pale mchakato utakapokamilika, muda sio mrefu nitakupa taarifa ya timu nitakayokuwepo,” alisema Chippo.
Chippo aliongeza, hashangazwi na makocha wengi kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini Tanzania kwa lengo la kufundisha timu za hapa kwa sababu ya ubora wa Ligi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ambao unavutia kila mmoja.
“Ukiachana na ushindani wa Ligi yenyewe ila Tanzania kuna mazingira mazuri katika utendaji wa kazi ndio maana wachezaji na makocha wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wanakuja hapa, kwangu ni heshima ikiwa nitapata nafasi ya kufundisha tena,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Tabora United, Richard Abwao alisema, kuanzia Jumatano ya Agosti 7, ndio wataanza kutoa taarifa za timu hiyo kuanzia benchi la ufundi na wachezaji wapya, hivyo mashabiki waendelee kuvuta subira.