Kazi inaendelea viwanja vya Leisure Lodge

AKIWA na matumaini makubwa ya kufanya vizuri, mchezaji Vicky Elias anaiongoza timu ya Watanzania kushinda mashindano ya mfululizo wa viwanja vitano ya Coastal Open ambayo yanaanza asubuhi hii katika viwanja vya Leisure Lodge, Mombasa, Kenya.

Elias ambaye anatoka klabu ya TPDF Lugalo  ya jijini Dar es Salaam, ameiambia Mwanaspoti  kutoka Mombasa kwamba yete na wenzake wanne, wamejiandaa vyema kuhakikisha wanafanya vizuri tena kama walivyofanya mwaka jana na miaka mingine iliyopita.

Vicky na wenzake kutoka mkoa ya Arusha na Dar es Salaam  waliondoka mwishoni mwa juma na wote walidai kuwa na azma ya kuiteka tena Mombasa kama walivyokuwa wakifanya kabla ya mashindano ya mwaka huu.

Wengine ambao asubuhi hii wanaanza mashindano haya ni Yasmin Challi na Shaz Myombe kutoka Dar Gymkhana wakati Neema Olomi kutoka klabu ya Arusha Gymkhana na Loveness Mungure wa klabu ya Kili Golf, wanatokea mkoa wa Arusha.

“Wote tuko vizuri kwa ajili ya kuanza vyema mbio hizi. Naamini sisi wote tutafanya vizuri kwa sababu viwanja hivi si vigeni kwetu,” alisema Elias ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Gofu nchini.

Mashindano haya yanaana leo Jumatatu, Agosti 5 katika viwanja vya Momabasa Lesire Lodge kwa mujibu wa waandaaji wake chama cha Gofu ya Wanawake Kenya (Kenya Ladies Golf Union).

Wachezaji kutoka nchi za jumuiya ya Afrika watashindanishwa katika viwanja vitano tofauti katika miji ya mwambao wa Kenya ya Mombasa, Vipingo na Malindi ili kupata mshindi wa jumla.

Nchi zinazoshiriki  ni wenyeji Kenya, Uganda, na Tanzania.

Katika  mashindano ya mwaka jana, Tanzania ilifanya vizuri baada ya kushinda nafasi mbili kati ya tatu za juu katika mchezo wa mashimo 18 ya ufunguzi uliofanyika katika viwanja vya Mombasa Leisure lodge.

Neema Olomi alimaliza  mshindi wa pili baada a kurudisha mikwaju 79  licha ya kufungana kwa idadi hiyo hiyo ya  mikwaju na  Vicky Elias wa TPDF Lugalo, lakini sheria ya kuhesabu nani kafanya vizuri mwishoni(countback) ilimpelekea Elias kumaliza katika nafasi ya tatu.

Loveness Mungure, ambaye mwaka jana alishinda mashindano ya wanawake ya Zambia, pia alifanya vizuri katika michuano hii ya pwani ya Kenya mwaka jana baada ya kumaliza wa tatu katika mfumo wa kuhesabu neti.

Baada ya kumaliza raundi ya kwanza katika viwanja vya Leasure Club, Watanzania watakuwa na kibarua kingine kesho ambapo watashiriki katika mchuano wa mashimo 36 katika viwanja vya Nyali kabla ya kuelekea Malindi Golf Club ambako watacheza mashimo mengine 18.

Mtihani wao wa mwisho utakuwa katika viwanja vya Vipingo Ridge ambako watamalizia raundi ya tano.

Related Posts