Meja Jenerali kuwaongoza Watanzania kushiriki michuano ya gofu Kenya

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Mkuu wa Utendaji Kivita na Mafunzo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ), Meja Jenerali Ibrahim Mhona anatarajiwa kuwaongoza wachezaji wa gofu wa Tanzania katika fainali za mashindano ya KCB East Africa Golf Tour, yatakayofanyika Desemba,2024, Nairobi, Kenya.

Meja Jenerali Mhona ni miongoni mwa wachezaji wanne wa gofu waliopata nafasi ya kushiriki michuano hiyo baada ya kuibuka mshindi wa pili kwa pointi 41 katika mashindano ya mchujo ya wazi yaliyofanyoka Agosti 3, 2024, viwanja vya Lugalo.

Mkuu wa Utendaji Kivita na Mafunzo JWTZ Meja Jenerali Ibrahim Mhona akipiga Mpira kwenye eneo la kuanzia mchezo wa Gofu (Tbox) kwenye shindano la KCB East Africa Golf Tour linalofanyika kwa siku moja katika Klabu ya Gofu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania JWTZ Lugalo.

Ushindi huo unamfanya aungane na wachezaji wengine, Peter Mlewi ambaye ni bingwa wa michuano kwa kupata pointi 42, wa tatu Khadija Selemani pointi 40 na Hawa Wanyeche alama 39 wote wakitoka Klabu ya Gofu Lugalo.

Akizunguza wakati wa kukabidhi bendera kwa timu hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro baada ya kufunga mashindano hayo, amesema michuano hiyo haiishii katika michezo bali kukuza umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia amewapongeza wachezaji na wadhamini wa mashindano hayo Benki ya KCB, kutokana na kujihusisha katika kuendeleza michezo mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa benki ya KCB, Cosmas Kimario, ametaja lengo lao ni kukuza mchezo wa gofu na kuahidi kuendeleza udhamini.

Related Posts