Dar es Salaam. Itakugharimu wastani wa Sh3.81 milioni kwa mwaka kumiliki jenereta linalotumia mafuta kwa ajili ya umwagiliaji katika kilimo na litadumu kwa miaka mitatu pekee.
Pia mkulima atalazimika kutumia Sh10 milioni kumiliki mitambo ya nishati ya umeme jua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambao kiuhalisia utadumu kwa miaka 20.
Hiyo ni kwa mujibu wa tathmini ya Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), kinachofafanua licha ya gharama kubwa za mwanzo katika usimikaji wa mtambo wa nishati ya umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji, kuna unafuu mkubwa baadaye.
Unafuu huo kwa mujibu wa Tarea, unatokana na muda mrefu ambao mtambo wa nishati ya umeme jua unadumu, huku ukiwa hauhusishi gharama za ziada za uendeshaji, wakati jenereta linahitaji mafuta kila linapotumika.
Chama hicho kimekwenda mbali zaidi na kueleza jenereta linalotumia mafuta katika kilimo cha umwagiliaji linazalisha kilo 487 za hewa ya ukaa, ambayo ni hatari kwa mazingira.
Mbali na tathmini ya Tarea, mkulima anayetumia nishati ya umeme jua mkoani Dodoma, Anthony Machai anasisitiza unafuu wa nishati hiyo katika kilimo, ukilinganisha na mtambo unaotumia mafuta.
Kwa mujibu wa Machai, katika shamba la ekari tatu kwa jenereta utalazimika kununua mafuta ya Sh50,000 kila siku kuwezesha kuvuta maji kutoka kisimani hadi kwenye mazao kwa ajili ya umwagiliaji.
Gharama hizo, anasema kwa mwezi ni sawa na kutumia Sh1.5 milioni kiasi ambacho ni maumivu kwa mkulima wa kawaida, lakini unapotumia mitambo ya umeme jua gharama ni kuifunga tu, baada ya hapo mkulima hatalazimika kuingia gharama za ziada.
“Pamoja na mazingira hayo, ni wakulima wachache ndiyo tunaotumia nishati ya umeme jua kwenye kilimo, wengi wanaona afadhali watumie majenereta na mafuta,” anaeleza.
Kwanini wengi watumie majenereta?
Kinachochochea wakulima wengi wachague majenereta licha ya faida ndogo wanayopata ni kile kilichoelezwa na Machai kuwa hawana uwezo wa kufunga mitambo ya umeme jua.
Machai anasema mtambo wa umeme jua unaomudu huduma za shamba la ekari nne hadi tano, unagharimu Sh9 milioni hadi 15 milioni.
Anasema ni wakulima wachache wenye uwezo wa kuwa na kiwango hicho cha fedha kwa wakati mmoja, ndiyo sababu wanakimbilia kwenye mafuta.
“Ni kweli ukifunga mtambo kwa gharama hizo hautahitajika kutoa gharama nyingine, lakini ni wakulima wachache wenye uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha kwa mkupuo,” anasema.
Kinachopaswa kufanywa, anasema Serikali iangalie utaratibu wa kuwawezesha wakulima kukopeshwa mitambo hiyo, ili walipe kidogo kidogo hadi watakapomaliza na kueleza kuwa gharama za mitambo huo zinarudishwa kwa awamu moja ya kilimo.
“Mwaka huu nimelima ekari moja ya nyanya kwa kutumia sola nimeingiza Sh12 milioni, hivyo msimu mmoja unakuwezesha kurudisha gharama za mtambo, lakini si kila mkulima ana uwezo wa kupata fedha ya kununua mtambo kwa mara moja, wakopeshwe,” anaeleza.
Anasema gharama kubwa za mtambo zinasababishwa na kodi zilizopo katika uingizaji wa bidhaa hizo nchini, hivyo anapendekeza kuwepo msamaha wa kikodi katika uingizaji wa bidhaa za sola nchini, ili kurahisisha wakulima na kuendana na mpango wa Serikali wa matumizi ya nishati safi.
Wasambazaji sola wanasemaje?
Akizungumza gharama za uingizaji wa sola nchini, meneja wa mauzo wa kampuni ya uingizaji wa mitambo ya nishati ya umeme jua ya Davis and Shirtliff, Octavian Ndago anasema imepungua maradufu kutokana na kile alichoeleza Serikali imeondoa kodi kwenye vifaa vya nishati ya umeme jua miaka miwili iliyopita.
Kwa mujibu wa Octavian, kwa sasa vifaa vya nishati hiyo vimewekewa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Hali hiyo, anasema imesababisha bei ya wati moja ya nishati hiyo ipungue kutoka zaidi ya Sh2,000 ya mwaka juzi hadi kati ya Sh500 na Sh800 kwa sasa.
“Serikali inafanya juhudi za kutoa msamaha ya kikodi. Hakuna VAT kwenye sola isipokuwa gharama za ufungaji mitambo, hasa ya kilimo zinahusisha mambo mengi,” anasema.
Ingawa kuna msamaha huo, Octavia anasema bado ufungaji wa mitambo ya nishati hiyo kwa mkulima itakuwa na gharama kubwa.
Ukubwa wa gharama hizo, anaeleza hausababishwi na bei ya sola, bali vifaa vingine vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilisha mtambo husika.
“Kwa mfano mteja anapotaka umfungie mtambo kwa ajili ya umwagiliaji shambani pale hautumii vifaa vya sola peke yake. Kuna mitambo mingine ambayo gharama zake ni kubwa na hicho ndicho kinachoongeza gharama za mitambo hiyo ya kilimo,” anasema.
Anapendekeza Serikali isiishie kupunguza kodi kwenye bidhaa za sola pekee, bali na mitambo yote inayohusika kwenye ufungaji wa nishati ya umeme jua kwa mkulima.
Kauli ya wasomi kuhusu sola
Ushauri kama wa Octavian unatolewa pia na msomi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Darius Mukiza anayesema gharama za mwanzo za kusimika mitambo ya umeme jua shambani zinapaswa kupungua.
Ili zipungue, anapendekeza kuwepo kwa msamaha wa kodi katika bidhaa za sola, pia vifaa vingine vinavyoambatana katika usimikaji wa mitambo.
Mwanzuoni huyo anaweka wazi juu ya uwepo wa baadhi ya wakulima katika mikoa ya Dodoma na Morogoro wanaotumia nishati ya umeme jua, lakini si wengi kwa sababu wengine hawamudu gharama.
“Serikali ikilipa kipaumbele hili suala la nishati ya umeme jua katika kilimo itasaidia mambo mengi kwa sababu ni nafuu kwa mkulima, pia ina hakika wa uzalishaji mwaka mzima,” anaeleza.
Kwa mtazamo wa Mhadhiri wa Nishati Jadidifu na Uhandisi Kilimo wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Yusto Yustas kuna haja ya kuongeza uwezo kwa wataalamu, ili watengeneze teknolojia za nishati hiyo kupunguza gharama za upatikanaji wake.
Anasema ni muhimu pia kuimarisha uwekezaji wa sekta binafsi katika kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za nishati za jua kwa gharama nafuu.
“Bahati nzuri haya yote yanawezekana kwa sababu sera zinazohusu kilimo, nishati, uchumi na elimu zina mlengo huo. Kubwa kabisa, Serikali yetu inaendelea kuboresha mikakati mbalimbali kurahishisha utekelezaji wa sera hizi,” anasema.
Katika sekta ya kilimo, anasema nishati ya umeme jua inatumika mnyororo wote wa thamani wa kilimo kuanzia mazao yakiwa shambani na hata kuyaandaa kwa ajili ya kula.
“Nishati hiyo inaweza kutumika katika maandalizi ya shamba kwa maana ya kuendeshea vifaa kuvuta maji kutoka kwenye vyanzo kwa jili ya kuandaa shamba ama umwagiliaji,” anasema.
Kadhalika, nishati hiyo inatumika kwenye uchakataji wa mazao kwa maana ya kuyakausha au kuzalisha ubaridi kwa yale yanayohitaji kwa ajili ya kuyapeleka sokoni.
Nishati hiyo pia kwa mujibu wa Dk Yustas, inatumika katika mitambo ya kuhifadhi mazao yakiwa sokoni.
Hata hivyo, mwanazuoni huyo anasema nishati ya umeme jua ni muhimu katika ulinzi wa usalama wa chakula kwa kuwa inawezesha uzalishaji zaidi.
Anasema ni muhimu kuimarisha matumizi ya nishati hiyo na itumike kwa usahihi, ili kuongeza thamani na ufanisi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula.