Kutokana na vurugu hizoWaziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer atafanya mkutano wa dharura leo hii Jumatatu. Mkutano huo wa usalama wa nchi kwa jina Cobra, utawaleta pamoja mawaziri na polisi watakaojadili jinsi ya kuzimaliza ghasia zilizozuka kwa mara ya kwanza huko Southport, kaskazini magharibi mwa Uingereza ambako watoto watatu waliuawa. Hadi kufikia sasa mamia ya watu wamekamatwa.
Soma Pia: Waziri Mkuu Starmer aapa kuwawajibisha walioshiriki ghasia
Katika hotuba yake kwa taifa, Starmer, amelaani ghasia za hivi majuzi za kupinga wahamiaji, ambapo amesema wahusika ni “majambazi wa mrengo mkali wa kulia”. Polisi wamesema mshukiwa wa mauaji ya watoto watatu huko Southport, Axel Rudakubana, mwenye umri wa miaka17, alizaliwa nchini Uingereza.
Mji huo wa Southport ni eneo la mkasa wa wiki iliyopita ambapo wasichana watatu wadogo waliuawa na watoto wengine watano walijeruhiwa vibaya waliposhambuliwa kwa kisu wakati walipokuwa wanahudhuria darasa la kujifunza kucheza dansa lililopewa jina la mwanamuziki nyota Taylor Swift.
Soma Pia: Polisi Uingereza waongeza ulinzi baada ya ghasia kuibuka
Baada ya tukio hilo machafuko yamezuka katika miji mingine kote nchini Uingereza huku waandamanaji wanaopinga wahamiaji wakikabiliana na polisi, na pia waandamanaji Waislamu wanaopinga maandamano hayo katika baadhi ya nyakati.
Polisi wamewalaumu wafuasi wa kundi la English Defence League, EDL pamoja na makundi yanayohusiana na kundi hilo kwa ghasia hizo. Kundi hilo la EDL linalopinga Uislamu lilianzishwa miaka 15 iliyopita na wafuasi wake mara nyingi wanahusishwa na vurugu kwenye mashindano ya soka.
Ghasia mbaya zaidi za siku ya Jumapili zilitokea kwenye mji wa Rotherham, kaskazini mwa Uingereza, ambapo waandamanaji waliokuwa wamejifunika nyuso zao walivunja madirisha katika hoteli ambayo imekuwa ikitumiwa kuwahifadhi wakimbizi.
Polisi ya Yorkshire Kusini imesema takriban maafisa 10 walijeruhiwa, akiwemo mmoja aliyepoteza fahamu.
Vyanzo: AFP/AP