Dhaka. Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina amejiuzulu na kukimbia nchi kutokana na maandamano yanayoendelea yaliyosababisha vifo vya watu takribani 300.
Tovuti ya Al Jazeera imesema Hasina ameondoka nchini humo leo Jumatatu Agosti 5, 2024 baada wananchi kupuuza amri yake ya kutotoka nje na kuvamia Ikulu ya Waziri Mkuu huyo iliyopo jijini Dhaka.
Takriban watu 300 wamefariki dunia tangu kuanza kwa maandamano wiki kadhaa zilizopita nchini humo, huku waandamanaji vijana wakilalamikia hali ngumu ya maisha na ukosefu wa ajira. Idadi kubwa ya vifo takribani 100 ilirekodiwa jana Jumapili.
Baada ya kujiuzulu kwa waziri mkuu huyo, Jeshi la Bangladesh limesema limeshikilia kwa muda mpaka pale hali itakapotengamaa na hivi sasa inafanya mawasiliano na viongozi wa kisiasa.
“Pia tutahakikisha haki inatolewa kwa kila kifo na uhalifu uliotokea wakati wa maandamano,” amesema Mkuu wa Majeshi wa Bangladesh, Jenerali Waker-Uz-Zaman baada ya kuthibitisha kuwa waziri mkuu amejiuzulu.
“Tumewaalika wawakilishi kutoka vyama vyote vikuu vya kisiasa na wamekubali mwaliko wetu na kujitolea kushirikiana nasi,” ameongeza jenerali huyo
Aidha, amewataka wananchi kuweka imani kwa jeshi hilo, akisema litarudisha amani ya nchi katika wakati huo wa mpito.
Televisheni mbalimbali nchini humo, zinaonyesha maelfu ya watu wakiingia katika makazi rasmi ya waziri mkuu.