Dar es Salaam. Waswahili husema, “kisicho riziki hakiliki,” methali hiyo imeakisi uhalisia katika familia ya Jamal Kwangaya iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Familia hiyo iliyokuwa katika matarajio ya harusi, ghafla mpango huo uligeuka huzuni, baada ya aliyetarajiwa kuolewa kupoteza maisha.
Bibi harusi mtarajiwa Hanifah Kwangaya ni mmoja kati ya ndugu wanne wa familia moja walipoteza maisha katika mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa Mei mwaka huu na kufuatiwa na Kimbunga Hidaya.
Mzizi wa mafuriko hayo ni mfululizo wa mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba 2023 kama zilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Akisimulia mkasa ulioondoa uhai wa Hanifah na wengine watatu, Kwangaya ambaye ni baba mdogo, anasema mwanawe alikuwa akiishi Kijiji cha Mope, eneo lililokuwa maalumu kwa shughuli za kilimo.
Ingawa kijiji hicho ni hatari kwa maisha ya binadamu hasa nyakati za mvua, Kwangaya anasema walilazimika kuendelea kubaki huko kwa kuwa ilikuwa vigumu kupata mtumbwi wa kuwahamisha.
Anasema mafuriko yalikiathiri kijiji hicho, hivyo walilazimika kuhamia ng’ambo katika Kijiji cha Kongoniongo.
“Kipindi cha maafa mtumbwi ulikuwa vigumu kupatikana, wale (ndugu) wakakwama kule katika maeneo yaliyopaswa kuhama,” anasema Kwangaya.
Anasema waliishi eneo hilo hadi mahitaji muhimu ya binadamu yalipokwisha; kwa kuwa walitumiwa fedha kwa njia ya simu, walitakiwa kwenda kuzitoa ili kununua mahitaji hayo.
Hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kutafuta mtumbwi wa kuwawezesha kufika Ikwiriri, kwa kuwa katika kijiji hicho hakukuwa na huduma za kifedha.
“Mahitaji yalishaisha, sasa wakawa wanalazimika waje huku (Kata ya Ikwiriri) wapate mahitaji,” anasema Kwangaya.
Anasema katika harakati za kwenda Ikwiriri walifanikiwa kupata mtumbwi na walipanda watu wanane wakiwamo sita wa familia moja.
“Walipanda hadi walipofika darajani mmoja wao wa kiume, alitaka kushushwa lakini dereva wa mtumbwi aliwataka wote washuke darajani hapo, wakakataa kwa kuwa hawakuwa na fedha ya kutokea eneo hilo hadi Ikwiriri, hivyo waliomba kuendelea na safari ya mtumbwi hadi eneo la jirani na Ikwiriri,” anasema Kwangaya.
Safari na mtumbwi wenye abiria saba iliendelea hadi walipolifikia Daraja la Rufiji; na hapo ndipo mzizi wa ajali ulipoanza.
“Yule dereva hakuwa anajua kama pale kwenye daraja kuna maji ya mzunguko kwa hiyo yakawa yanamvuta, alionekana yamemshinda.
“Akawa anashauriwa kupita chini ya daraja naye akatekeleza hilo na alivyofika mbele mzunguko wa maji ulizidi na kusababisha mtumbwi kupinduka,” anasema Kwangaya.
Baada ya mtumbwi kupinduka, anasema waliozama ni mwanawe na wajukuu zake wanne, lakini mmoja aliokolewa.
Anasema baada ya hatua hiyo, hatua za kutafuta miili ya waliozama ziliendelea kwa siku tatu bila mafanikio.
Kwangaya anasema siku ya nne kwa kushirikiana na Serikali, ndipo walifanikiwa kupata miili miwili; na siku iliyofuata ulionekana mwili mwingine, lakini uliobaki majini haukupatikana hadi sasa.
“Hiyo maiti ya mdogo hatukubahatika kuiona hadi hivi sasa, kwa hiyo tunashukuru kwa Serikali kutusaidia na kushirikiana na wananchi katika yote,” anasema Kwangaya.
Mbali na kupoteza wapenda wao, anasema mazao mbalimbali ikiwamo ufuta katika mashamba yote yamesombwa na mafuriko.
Kwangaya anasema hadi mwanawe Hanifah anafariki dunia hakuwa na mume, isipokuwa kulikuwa na matarajio ya ndoa.
Anasema kabla ya kufariki dunia, Hanifah alishamwambia kuwa, siku chache zijazo angempa taarifa rasmi juu ya mchumba wake.
“Kipindi alichokuwa anakuja huku kulikuwa na taarifa ya ndoa na kwa sababu wakati wake umefika ndoa imeishia hapo. Kwa hiyo hilo tulilijua kwamba kulikuwa na mchumba anayehitaji kumuoa,” anasema Kwangaya.
Anasema maisha ya familia nzima yameendelea kuwa magumu kwa kuwa mazao yote waliyotarajia kwa ajili ya chakula pia, yamepotea kwa mafuriko.
Hali inakuwa mbaya zaidi kwa kile alichoeleza, hata mahindi waliyoyapanda baada ya mafuriko hayo, yamesombwa tena na maji.
“Tulijaribu tena kwenda kupanda mahindi, kwa taarifa niliyonayo ni kwamba kuna maji yameyapitia nusu. Tunaiomba sana Serikali jicho lake liangalie Rufiji hasa Ikwiriri,” anasema.
Mtumwa Mbonde, shangazi wa marehemu anasema alipokea taarifa ya msiba kwa simu kwamba ndugu zake hao wamezama majini.
Baada ya taarifa hiyo, anasema walitafutwa askari wa zimamoto kwa ajili ya uokoaji ndipo walipofanikiwa kuiona miili ya wawili na baadaye mmoja na mwingine hadi sasa haujapatikana.
Anaeleza kuwa, binti aliyefariki dunia alikuwa mkulima na kwamba kifo chake kimeacha majonzi kwa kuwa ni vigumu kusahau.
“Ni msiba mzito hatutausahau kwa sababu ni pigo kubwa,” anasema Mbonde.
Historia ya mafuriko Rufiji
Ingawa mafuriko yaliyoshuhudiwa mwaka huu yalikuwa na athari kubwa, historia inaonyesha hii si mara ya kwanza kwa Wilaya ya Rufiji kukumbwa na mafuriko.
Inaelezwa kuwa, Rufiji imekuwa katika hatari ya kuathiriwa na mafuriko katika nyakati tofauti kama inavyoelezwa na Faraji Maloa, mkazi wa wilaya hiyo kwa miaka 40 sasa.
“Nafahamu historia hizi za mafuriko, mara ya kwanza mwaka 1936 kulikuwa na mafuriko makali yaliitwa Lilale na ndiyo yaliyotengeneza mito mbalimbali.
“Kwa mfano madaraja ya Ngayonga, Mtanga, Tingetingeni, Ruwoyi yote hayo ni zao la mafuriko hayo,” anasema Maloa.
Anaelezea historia hiyo kuwa, mafuriko hayo ya mwaka 1936 ndiyo yaliyotengeneza Ziwa la Umwe na mito Lingola, Urungu, Poka na Kingola.
Anasema mito na mifereji yote, imekuwa vyanzo vya mafuriko mvua kubwa inaponyesha.
Pamoja na eneo hilo kuwa hatari kwa mafuriko, anasema watu wanalazimika kuishi kwa kile alichoeleza, wanafuata rasilimali ardhi yenye rutuba.
“Unajua bonde ni ardhi yenye rutuba sana kwa hiyo mtu hawezi kuiepuka hiyo, lazima atakwenda kwenye ardhi yenye rutuba huwezi kwenda kulima kwenye ukame,” anasema Maloa.
Tangu mvua zilivyoanza Oktoba mwaka jana, anasema hakuna aliyetilia maanani hadi pale Serikali ilipotoa taarifa ya tahadhari.
Maloa anasema kuanzia Aprili mwaka huu, tahadhari hiyo ya Serikali ikawa katika uhalisia, wananchi walianza kushuhudia mafuriko huku mashamba na makazi yakisombwa na maji.
“Mimi nilikuwa na ekari 12 zote zilijaa mpunga, zimesombwa na mimi ndiyo nilikuwa nategemea hizo tu kwamba nikivuna nitakuwa na fedha na chakula cha kutosha,” anasema Maloa.
Anaeleza kuwa, hata kama wanahitaji msaada, lakini ni vigumu kupata utakaowatosheleza kwa kuwa idadi ya wanaoishi eneo hilo ni wengi.
Maloa anasisitiza umuhimu wa taarifa kutolewa mapema ili wananchi wajipange na hilo lisifanywe na mkuu wa wilaya pekee, bali kila ngazi.
“Tumeambiwa tuondoke kule bondeni kwa kuwa limefunikwa kabisa na maji, lakini yanakuja (maji) kwa sababu bwawa la Mwalimu Nyerere limejaa kupita kiasi,” anasema Maloa.
Akizungumzia vifo hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele anasema jumla ya watu tisa wamepoteza maisha.
Anasema kabla ya Kimbunga Hidaya walifariki dunia watu wawili akiwamo mwanamke mwenye umri wa miaka 20 na mtoto wa miezi miwili.
Vifo hivyo, anasema vilifuatiwa na vingine vinne vya familia moja.
“Kwa jumla tulikuwa na vifo tisa vilivyotokana na wananchi kutumia mitumbwi ilhali Serikali ilishakataza, lakini kwa maji kuzingira nyumba hakuna mtu aliyepoteza maisha,” anasema Gowele.
Hata hivyo, anasema iwapo wananchi wagezingatia miongozo waliyopewa na Serikali ya kuacha kutumia mitumbwi pengine wangeokolewa.
Meja Gowele anasema watu 89,000 wameathirika wanaojumuisha kaya 23,360.
Anasema nyumba 628 zimeathirika katika kata 12 kati ya 13 zinazopatikana wilayani humo, akisisitiza hiyo ni kabla ya Kimbunga Hidaya.
Ili kuepuka janga kama hilo, anasema Serikali iliomba ekari 150 katika msitu wa hifadhi kuanzisha makazi na baadhi ya wananchi wameanza kuingia eneo hilo ili kuepuka athari za mafuriko.
Anasema katika Kijiji cha Tungi, viwanja vinaendelea kutolewa kwa wananchi ili wakaishi salama.
Kuhusu misaada, anasema Serikali ilipeleka mahema 12, chakula zaidi ya tani 200 kwa ajili ya kuhudumia watu waliopo kwenye kambi na wale waliopo kwa ndugu jamaa na marafiki.
Mbali na Serikali, anasema misaada mingine ilipelekwa na mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, hivyo kutosheleza wakazi wa eneo hilo.
“Hivi juzi, ameleta misaada ya mbegu zenye thamani ya Sh40 milioni kutoka kwenye mfuko wake mwenyewe na ametafuta wahisani CRDB (benki) wametuletea mbegu za Sh40 milioni,” anasema Meja Gowele.
Anaeleza bado usambazaji unaendelea kuhakikisha mbegu zinatosheleza mahitaji.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation