Rais Samia akemea siasa kuchochea uvamizi wa hifadhi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya uanzishwaji wa vijiji vipya unaofanywa kwa masilahi ya kisiasa, akisema ndiyo inayochochea uvamizi wa maeneo ya hifadhi.

Sambamba na hilo, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii isisubiri wananchi wavamie na kuyaendeleza maeneo ya hifadhi ndiyo ishtuke, badala yake inapaswa kuyalinda mapema.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Jumatatu Agosti 5, 2024 alipowahutubia wananchi wa Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani humo.

Tabia za uanzishwaji vijiji vipya, amesema aghalabu hufanyika katika nyakati zinapokaribia chaguzi, wagombea wakilenga kunufaika kisiasa.

“Inapokaribia chaguzi hizi hasa madiwani, mtu akiona yuko vibaya upande mwingine wa eneo lake, anakwenda kusogeza watu kuanzisha kijiji.

“Sasa haya ya kuanzisha vijiji bila kujali tunavianzisha maeneo gani, vijiji vingi vilivyoanzishwa ndani ya maeneo ya hifadhi ni kwa ajili ya wanasiasa wameanzisha, iwe ni madiwani, iwe wabunge,” amesema.

Pamoja na kwamba wanasiasa hao ndiyo wanaowapeleka wananchi katika maeneo hayo, amesema haohao baadaye wanageuka kuwa watetezi wao, akidai wanapoondolewa kwenye hifadhi wanaonewa.

“Halafu ni haohao wanaokuja kusimama kuwatetea watu walioingia ndani ya hifadhi, lakini ulipowapeleka ulikuwa unajua ni eneo la hifadhi,” amesema.

Msisitizo wa Rais Samia ni kukomesha tabia hiyo kwa kuwa inavunja sheria na kuathiri uhifadhi wa ardhi kwa matumizi ya baadaye.

Katika hatua nyingine, amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki kulinda maeneo ya hifadhi, badala ya kuacha wananchi wavamie hadi kuweka makazi ya kudumu.

“Mpaka wananchi wanahamia wanajenga, wanajenga shule, kituo cha afya bado mnawaangalia baadaye huko wameshatulia ndiyo aah! vijiji wamevamia watoke, hii nayo sio haki,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amewataka wananchi wanaoidai Serikali fidia baada ya kupitiwa na miradi, wasubiri miradi hiyo ikamilike kwanza, kisha utaratibu utafanyika kuhakikisha wanalipwa.

Kinachosababisha uamuzi huo, amesema ni umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi, hivyo Serikali inaona ianze kuitekeleza kwanza kwa manufaa ya wengi, ndipo ichakate utaratibu wa fidia.

Mkuu huyo wa nchi ameibua hoja hiyo baada ya malalamiko ya wananchi wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro, kudai malipo ya fidia baada ya kupitiwa na mradi wa umeme wa Kihansi yaliyoibuliwa na mbunge wa Mvomero, Aboubakar Assenga.

“Kwa hiyo kwa wale wanaotudai fidia zao kwa maendeleo yao wenyewe tunaomba muwe na subira. Tuacheni tumalize miradi ya maendeleo wananchi wengi wafaidike, halafu tutaangalia masuala ya fidia,” amesema Rais Samia.

Katika maelezo yake, amegusia uwepo wa baadhi ya watu wanaoweka vikwazo vya utekelezwaji wa miradi husika kwa sababu hawajalipwa fidia.

“Tuacheni tufanye miradi, mambo ya fidia mimi nawahakikishieni hatonyimwa mtu haki yake. Tukiwa tayari tutalipa fidia, kwa hiyo niwaombe sana wananchi acheni miradi ijengwe kwa manufaa yenu, fidia itakuja kulipwa,” amesema.

Rais Samia amemwagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuuelekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda kununua mpunga mkoani humo.

Hata hivyo, amesema kuanzia sasa badala ya Sh500 iliyokuwa bei ya kilo moja ya mpunga mkoani humo, kwa sasa imeongezeka hadi Sh900.

Hadi anafikia uamuzi wa kupandisha bei hiyo, mkuu huyo wa nchi alishaombwa ridhaa ya kulitekeleza hilo na Bashe kwa kile kilichoelezwa bei ya awali iliwakandamiza wakulima.

Wakati anayaeleza hayo, Rais Samia amewataka viongozi wasiwe sehemu ya wanaowakandamiza wakulima katika ununuzi wa mpunga huo, akisema vitendo hivyo vinanyima  haki.

“Tumeweka viongozi ngazi mbalimbali tuwasaidie wananchi, mnapojiingiza kwenye biashara hii na kwenda kunyonya nguvu ya mkulima hufanyi haki, uwe diwani, uwe nani kama unafanya biashara hii ya kuongeza kipimo kwenye debe la mkulima hufanyi haki,” amesema.

Sababu ya kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, ana taarifa za uwepo wa viongozi wanaojihusisha na shughuli za biashara hiyo.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Bashe alipendekeza kuongezwa kwa bei ya mpunga kutoka Sh500 kwa kilo hadi Sh900.

Hata hivyo, amesema Serikali inafanya mikakati ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji, hasa kwa kuliendelea Bonde la Kilombero.

Related Posts