Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imetahadharisha kuhusu vitendo vya rushwa kipindi hiki Taifa linapojiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu.
Takukuru imesisitiza rushwa katika uchaguzi husababisha kuchaguliwa kwa viongozi wasio waadilifu, watakaotumia muda wao mwingi kurejesha fedha walizotumia na si kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Kinondoni, Elizabeth Mokiwa amesema wananchi wanapaswa kushirikiana na taasisi hiyo kutokomeza vitendo hivyo.
“Takukuru tunadhibiti rushwa wakati wote, ingawa kipindi hiki nchi inapoelekea kwenye uchaguzi tumeweka msisitizo mkubwa kwa sababu tunafahamu athari zake baadaye,” amesema na kuongeza;
“Kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa hawezi kuwa mwadilifu, atatumia muda mwingi kurejesha fedha alizotumia na si kuleta maendeleo kwa wananchi.”
Mokiwa amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo wameanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa wakati wa uchaguzi na wananchi wanapaswa kushirikiana na taasisi hiyo kuvitokomeza kuanzia sasa, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Tunaendelea kupokea malalamiko yanayohusu rushwa na kuyafanyia kazi kwa haraka, ili kudhibiti vitendo hivyo,” amesema.
Amesema pia wanatoa elimu ya rushwa shuleni na vyuoni, kufanya vikao na wadau na kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa.
Mbali na kutoa tahadhari hiyo, Mokiwa ameeleza wamepokea malalamiko 88 na kati ya hayo 32 yakihusu rushwa na yameshughulikiwa, sasa yapo katika hatua mbalimbali.
Mokiwa amesema mengine 43 ni ya asasi binafsi na 13 ni ya Tamisemi/Manispaa, huku saba yakiwa ya Wizara ya Ardhi, mawili ya Nida na matatu ya Dawasa na idadi kama hiyo ni ya polisi, mawili ya Mahakama na sita ni ya elimu.