Dar es saalam. Serikali ya Tanzania imesema upelelezi wa kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultani na wenzake, upo hatua za mwisho kukamilika.
Pia jalada la kesi hiyo lipo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kupitiwa na kuandaa taarifa muhimu kabla ya kusajili Mahakama Kuu.
Sultani na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane, yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na Frank Rimoy ameieleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Agosti 5, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif, Said Matwiko mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde, mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami;
Wengine ni John John maarufu Chipanda, mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.
Mwanga amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kuukamilisha, hivyo wameomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mwanga baada ya kueleza hayo, mmoja wa washtakiwa aliomba upande wa mashtaka waeleze upelelezi utachukua siku ngapi kukamilika, ili wajue.
Hakimu Lyamuya aliutaka upande wa mashtaka kutoa majibu ya swali lililoulizwa na mshtakiwa. Akijibu, wakili Mwanga ameomba wapewe mwezi mmoja kukamilisha upelelezi huo.
Tofauti na siku nyingine ambazo kesi hiyo husikilizwa kwa njia ya video, leo washtakiwa hao wamepelekwa mahakamani.
Hakimu Lyamuya alielekeza washtakiwa hao wapelekwe mahakamani baada ya tarehe iliyopita mtandano wa video comference kupata hitilafu, hivyo kushindwa kusikilizana na watuhumiwa.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hadi Agosti 19, 2024 itakapotajwa. Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Awali, washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matano, lakini Septemba 23, 2023 Mkurugenzi wa mashtaka nchini( DPP) aliwabadilishia hati ya mashtaka kwa kuwaongezea mashtaka matatu, likiwemo la kutakatisha fedha na kisha kuwasomea upya mashtaka.
Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu, shtaka linalowakabiliwa washtakiwa wote ambapo inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini.
Shtaka la pili inadaiwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 27.10.
Pia Novemba 4, 2023 washtakiwa Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 7.79.
Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD, huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Katika shtaka la nane inadaiwa Aprili 20, 2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.