Wenje atangaza nia kugombea nafasi ya Lissu Chadema

Mwanza. Joto la uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limeanza kupamba moto, baada ya Ezekia Wenje kutangaza nia ya kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho-Bara.

Wenje ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria Chadema yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita, anakusudia kujitosa kuomba ridhaa ya nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Tundu Lissu.

Mbunge huyo wa zamani wa Nyamagama, Mkoa wa Mwanza amesema hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari juu ya kusudio lake hilo, akisisitiza ameamua kuwania nafasi hiyo, ili kuongeza ufanisi wa kazi na uwajibikaji.

Wenje amesema baada ya tafakuri ya muda ameona ana uwezo wa kuwa msaidizi wa karibu wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye duru za kisiasa zinaonyesha atagombea tena uenyekiti kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

“Kutokana na uzoefu nilionao chamani, nimejitathimini kuwa nina uwezo wa kuwa msaidizi wa Mbowe, naomba ifahamike chama chetu cha Chadema kimekuwa kikijipambanua siku hadi siku katika kupigania haki za watu, ikiwemo uhuru, haki na maendeleo,” amesema.

Katika upande mwingine, amesema kulingana: “na utafiti wetu katika Kanda ya Ziwa tumebaini bado wananchi wanapitia maisha magumu, hivyo Serikali inatakiwa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati.

“Tumejiridhisha bado hali ya maisha ya wananchi wa Kanda ya Victoria ni mbaya, Chadema tunachukizwa na ugumu wa maisha kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa, utitiri wa kodi, tozo, ushuru na mazingira magumu ya kujipatia kipato,” amesema.

Wenje ameendelea kusema: “Ajabu ni kuona Serikali haijali kutatua matatizo na vikwazo vinavyowadidimiza katika wimbi la umaskini na unapokuwa msaidizi wa mwenyekiti ni kusikiliza, kushauriana na kumsaidia kwa sababu lengo letu ni kushika dola tukiwa na umoja, tutashinda.”

Hata hivyo, haijafahamika kama Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki atawania nafasi hiyo kwa mara nyingine au atapoumzika, kwani jitihada za kumtafuta kuzungumzia jambo hilo kwa njia ya simu zinaendelea, baada ya awali kutafutwa bila mafanikio.

Naye Katibu wa Chadema Wilaya ya Sengerema, Paul Fulano amesema Wenje kutangaza kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti haina maana kwamba hakuna maelewano kati yake na Lissu.

“Kanda ya Ziwa tumefurahi Wenje kuonyesha nia ya kugombea hii nafasi hii, maana hata Lissu kwa sasa tunavyomuona hana mpango wa kugombea nafasi ya chama, anataka agombee urais wa nchi, ili tugawanye majukumu yetu kwa urahisi katika chama,” amesema.

Julai 26, 2024, Lissu akizungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini kutoka ughaibuni, alitangaza nia ya kuwania tena urais katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Lissu ambaye mwaka 2020 aliwania urais na kushindwa na Dk John Magufuli wa CCM aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, alisema kwa sasa chama hicho kinaandaa wagombea wa nafasi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kinaibuka mshindi.

“Nia yangu ya kugombea mwaka 2025 ipo palepale, nitaitikia wito wa Watanzania na nitaitikia wito wa chama changu kama kitanitaka kufanya hivyo,” alisema Lissu.

Kutokana na nia hiyo ya Wenje, mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia na kisiasa, Hamduni Maliseli amesema kama katiba ya Chadema inaruhusu mtu kama Wenje kugombea, hakuna tatizo anaweza kushika nafasi hiyo kwa sababu amehudumu kwa muda mrefu ndani ya chama hicho.

“Bila shaka ni mtu sahihi kwa sababu yule ambaye ni makamu kwa sasa sidhani kama wanazidiana sana na Wenje ngazi ya siasa, labda kuna mambo amejifunza kutoka kwake ndio maana anataka kugombea nafasi hiyo,” ameongeza.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na masuala ya maendeleo ya jamii, Atiki Abubakari amempongeza Wenje kwa uamuzi wake wa kugombea nafasi hiyo akisema utaleta demokrasia ndani ya chama hicho.

“Uamuzi wa Wenje kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti unaonyesha wazi Chadema wameamua kuwa na demokrasia ndani yao na hilo lisiishie kwa nafasi ya makamu mwenyekiti tu, bali wapatikane wengine wanaogombea nafasi ya mwenyekiti,” amesema.

Related Posts