Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imeingia mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya ushauri ya Uturuki, Africapital Investment Holdings Ltd itakayosaidia kutafuta kampuni zitakazoingia ubia wa kutoa mitaji kwa wafanyabiashara nchini Tanzania.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga amesema changamoto inayowakabili wafanyabiashara nchini ni upatikanaji wa mitaji, hivyo mkataba huo utakuwa msaada kwa wale wote wanaotaka kuanzisha biashara na kikwazo kikawa mtaji.
“TPSF tumeamua kutafuta washirika watakaoleta mitaji yao nchini na kuwekeza kwa ubia na kampuni za Kitanzania, hasa wale wanaoanza biashara,” amesema Maganga.
Maganga amesema mitaji itaanzia Sh5 milioni na hiyo haitolewi kama mikopo, bali wataingia ubia na mwekezaji katika kukuza biashara nchini, kwani wafanyabiashara wanapoanza biashara hawakopesheki kwa kuwa hawana historia za benki.
Ili kupatikana kwa fedha hizo, Maganga amesema baada ya mkataba huo wataanza usajili wa kampuni na biashara wanazofanya, kisha watazichuja ili kupata wafanyabiashara wanaoonekana wakifanya vizuri katika sekta hiyo.
Hata hivyo, amesema mkataba huo utaelezea kwa upana zaidi jinsi gani wajasiriamali nchini watapata mitaji kupitia Africapital na TPSF.
Pia, amesema mwekezaji hatoweka mtaji pekee, bali na kuongeza ujuzi kwa wafanyabiashara wanaohitaji soko la kimataifa kwa biashara itakayoanzishwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Africapital, Burak Buyuksarac amesema wanafanya kazi na taasisi ndogo ili kupata mtaji kwa ajili ya kuanzisha biashara, hivyo wapo nchini kwa ajili ya kutoa ushirikiano.
“Tanzania ina uaminifu kwenye ufanyaji biashara na imeamua kuonyesha jitihada ya kusaidia wananchi wake katika kukuza biashara na kwa muda tuliosaini tutaleta kampuni nyingi kwa ajili ya kufanya kazi hapa,” amesema Buyuksarac.
Mbali na TPSF, Africapital imesaini mkataba wa mwaka mmoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambayo itashirikiana kwa ufanisi na wawekezaji wa kimataifa na wa ndani, ili kutafuta mtaji kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo, nishati, biashara na teknolojia.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassani alikuwa nchini Uturuki kwa ziara ya kiserikali ya siku tano ambapo pamoja na mambo mengine, alifanya mkutano kati ya wajumbe wa mabaraza ya biashara ya Uturuki na ujumbe wake.
Akizungumzia hatua hiyo, mtaalamu wa Uchumi, Profesa Samuel Wangwe amesema itasaidia kuinua wananchi kiuchumi, kuongeza pato la Taifa na itakuwa chachu ya uwekezaji wa ndani.
“Huo umoja ambao umekubali kuwatafutia wafanyabiashara kampuni za kutoa mitaji wamefanya jambo zuri ambalo linapaswa kuungwa mkono, lakini zizingatie hasa kwenye upande wa sayansi na teknolojia, ili kusaidia uzalishaji ambao utaleta ushindani ndani na nje ya nchi,” amesema Profesa Wangwe.
Msomi huyo ameongeza kuwa Uturuki imekuwa ikileta bidhaa zake nchini, hivyo kampuni hiyo iangalie namna ya kuwasaidia Watanzania kutengeneza bidhaa ambazo zitauzika nchini kwao kama ilivyo kwa upande wao.