Ukuta wa nyumba waua watoto watatu wa familia moja

Shinyanga. Mvua zinazoendelea kunyesha katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, zimesababisha vifo vya watoto watatu wa familia moja katika Kitongoji cha Miembeni B, Kijiji cha Mishepo baada ya kuangukiwa na nyumba waliyokuwa wamelala usiku wa kuamkia leo.

Akisimulia tukio hilo leo Ijumaa Aprili 26, 2024, mama wa watoto hao, Joyce Nchimbi ambaye amenusurika na mtoto wake mmoja, amesema mvua ilianza kunyesha saa nne usiku jana na ilipofika saa tisa usiku, ukuta wa nyumba ulianguka na kuwafunika watoto hao watatu.

Amesema wakati ukuta unaanguka, mume wake hakuwepo alikuwa kwenye familia ya mke mdogo na wakati anaomba msaada kwa majirani ndiyo taarifa zikamfikia.

Amewataja watoto wake waliopoteza maisha kuwa ni wa kike wawili Nkamba Ngasa (13), Gigwa Ngasa (8) na wa kiume, Salumu Ngasa aliyekuwa na miaka sita.

Hata hivyo, amesema nyumba yao ilikuwa imebomoka upande kwa muda mrefu lakini walikuwa wanaendelea kuishi na watoto wake licha ya mumewe kuelezwa na majirani aifanyie ukarabati lakini hakuzingatia.

“Mtoto wangu mdogo anaumwa nilikuwa naye wakati ukuta unaanguka, uliniponda mimi mgongoni nikawa nimemkinga mtoto, wanangu wengine ndiyo wakawa wamefunikwa na ukuta wote watatu,” amesema Nchimbi.

Baba wa familia hiyo, Ngasa Mataruma akizungumzia tukio hilo amesema alifika nyumbani kwake usiku baada ya kupigiwa simu na kukuta watoto wake wamepoteza maisha.

Alipoulizwa juu ya ubovu wa nyumba yake, alijibu tu, “naomba wasamaria wema wanisaidie hifadhi ya hawa waliobakia na chakula.”

Mkazi wa Kijiji cha Mishepo, Masai Kulwa amesema tukio hilo limewasikitisha na ametoa wito kwa wananchi pale wanaposhauriwa kujenga makazi bora, wazingatie.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Mishepo, Mary Peter amesema wananchi wengi wanaishi kwenye nyumba zenye nyufa kubwa na zimejengwa kwa tope, jambo linalohatarisha usalama wao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mishepo, Castory Jacob amesema alipigiwa simu usiku na majirani kupewa taarifa ya tukio hilo na alifika usiku huo na kukuta tayari watoto hao wamepoteza maisha na walitoa taarifa polisi waliofika eneo la tukio na kuchukua maiti.

Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Shinyanga Biasa Chitanda amewataka wakazi wa Mishepo kuacha kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina.

Amesema nyumba nyingi zinaanguka kutokana na kujengwa kwa tope na hazina misingi imara.

Related Posts