Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud amesema iwapo maisha ya watu yakiendelea kuwa ya dhiki na njaa, ni wazi hakutakuwa na amani ya kweli.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2024 katika viwanja vya Jazira Bububu Unguja alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Othman amesema ACT kinapigania uwepo wa amani ya kweli kwa kutaka Zanzibar iwe na uongozi unaosimamia nchi kuendeshwa kwa misingi ya kistaarabu, uwajibikaji na haki.
“Tunayasema haya kukumbushana, hatupiganii vyeo tunasema nchi yetu isimame iendeshwe kwa misingi ya kistaarabu, haki na amani. Kilichopo sasa ni watu kuwa kimya,” amesema kiongozi huyo.
Amesema wanaipambania nchi iwe na mamlaka ya kusimamia mambo yake, “huwezi kuwa na Serikali wakati mambo kadhaa huna mamlaka nayo kisha ukasema unatawala.”
Amesema kwa sababu wanapambania haki, hawatakubali mambo hayo yaendelee wanataka kuyashughulikia kabla ya uchaguzi.
Akizungumzia suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Othman amesema Zanzibar ilitoka kwenye maafa ya watu, kupata ulemavu majeraha, kuachwa vizuka na yatima.
Amesema Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alikubali kwenye mazingira magumu kuingia SUK ili kuifanya Zanzibar kwenda mbele na kuzingatia masilahi ya nchi.
Hata hivyo, Othman amesema kuna baadhi ya watu wanafanya hiyana hasa akitazama chaguzi ndogo zilizofanyika Pandani, Konde na Mtambwe.
Amelalamikia uwepo wa ghiliba na kwamba, hakukua na sababu ya kuendelea kufanyika ufisadi wa namna ile. Hata hivyo hakumtaja ni nani alifanya hayo.
Hata hivyo, Othman amesema wananchi hivi sasa wanapaswa kutafakari na wakiunge mkono chama hicho ili kiwe na uwezo wa kumaliza chaguzi zisizo na haki na ghiliba kwa nia ya kuleta haki na demokrasia ya kweli Zanzibar.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema hakuna nchi yoyote inayoweza kusonga mbele kimaendeleo, iwapo itakuwa na wizi na ufisadi na viongozi wasiowajibika kwa wananchi wao.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mansour Yussuf Himid amesema Wazanzibari wanataka kuishi kwenye nchi ya matumaini sawa na wengine, hivyo wananchi wanapaswa kuungana kuleta mabadiliko na kuwa na viongozi wanaowajibika kwa watu.
Amesema Zanzibar inahitaji mabadiliko kwa kuwepo na uongozi utakaojali utu na kuwajibika kwa watu katika jitihada za kuleta maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kidemokrasia.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Juma Said Sanani amewataka wazee Zanzibar wasisahau wajibu wao wa kuwaelimisha vijana kukiunga mkono chama hicho, ili kupigania haki na usawa sambamba na kustawisha upatikanaji wa ajira nchini.
Naye Katibu wa Ngome ya wanawake Mkoa wa Kusini Unguja, Ziada Mwadini Mussa amewataka wanawake na vijana kutokuwa na hofu na kwamba Wazanzibari hawatachoka kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Omar Ali Shehe amesifu juhudi za watu wa Pemba kwa kuwa na hamasa ya kukiendeleza chama.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Magharibi A kichama, Abdalla Haji Shaame amesema jambo pekee litakaloleta ahueni ya maisha kwa Wazanzibari ni kuunga mkono ACT kuleta mabadiliko ili kuitoa nchi kwenye umasikini.