HISIA ZANGU: Uwanja wa Mkapa kufurika saa sita mchana siyo sifa

TUNASHINDANA kila kitu katika miaka hii. Zama za ‘social media’. Wikiendi hii tulikuwa tunashindana tena katika matamasha mawili ya klabu pacha za Kariakoo Simba na Yanga. Simba Day na Wiki ya Mwananchi. Nani ataujaza uwanja?

Wote wawili wakafanikiwa kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa ambaye mwenyewe amelala Lupaso. Ukienda katika mitandao ya kijamii unakuta namna ambavyo kila mmoja alikuwa anajitapa kwamba kufika saa sita mchana uwanja ulikuwa umejaa au una zaidi ya nusu ya mashabiki. Haya ni mateso bila ya chuki.

Sidhani kama watu wanawahi kwa ajili ya kwenda kutazama wanamuziki. Nawajua mashabiki wetu. Wanawahi kwa ajili ya kwenda kutazama sehemu mbili kubwa. Utambulisho wa wachezaji na mechi yenyewe. Utambulisho wa wachezaji upo karibu na kuanza kwa mechi yenyewe. Hiki ndicho ambacho kinawapa mateso makubwa mashabiki.
Kwanini shabiki uingie saa sita mchana katika mechi ambayo inaanza saa kumi jioni au saa mbili usiku? Ni suala la hofu. Suala la kila shabiki kuwa na hofu ya utaratibu mbovu wa namna ya kuingia uwanjani. Kuwa na tiketi hakukuhakikishii kutazama mechi kwenye Uwanja wa Mkapa. Unaweza kuwa na tiketi na ukapigwa virungu usitazame mechi.

Una tiketi mkononi lakini virungu vinakufuata, mbwa wanakufuata, majasho ya watu yanakufuata. Unalazimika kusukumana kwa machozi, jasho na damu ili uweze kuingia uwanjani kuitazama timu yako pendwa. Hadi uweze kuingia jukwaani na kukaa unajikuta umechoka kimwili na kiakili huku ukiwa umechoka.

Haishangazi kuona hata mashabiki wasio na tiketi wanajitokeza Uwanja wa Mkapa kwa sababu wanaamini kwamba suala la kuingia uwanjani ni la mapambano zaidi kuliko kuwa na tiketi mkononi. Kwa wenzetu kama hauna tiketi hauwezi kwenda uwanjani kwa sababu hakuna namna unaweza kuingia uwanjani.

Miaka nenda rudi utaratibu ni mbovu vilevile. Karibu uwanja mzima unaingia uwanjani kwa kupitia mageti yaliyopo upande wa Magharibi. Umeona wapi? Kwa wenzetu maisha ni tofauti. Kila tiketi inampeleka shabiki katika jukwaa analokwenda kukaa. Anaingia katika geti la jukwaa analokwenda kukaa. Kwanini pale Kwa Mkapa yanafunguliwa mageti machache? Ni suala la kutafakari. 

Nimetazama mechi nyingi Ulaya. Nimetazama michuano mikubwa kama Kombe la Dunia na ligi mbalimbali. Kuingia uwanjani siyo vita. Unakaa nje ya uwanja unakunywa bia na kula nyama za kuchoma kisha unaweza kuingia taratibu uwanjani dakika 20 tu kabla ya mechi kuanza. Pambano linaweza kuwa kali vilivyo, lakini ndiyo utaratibu ambao wenzetu wamejiwekea.

El Clasico niliwahi kuingia Santiago Bernabeu dakika 15 tu kabla ya pambano kuanza na sikugusana na mtu. Ni pambano kali la Real Madrid dhidi ya Barcelona, lakini nilitembea kwa amani na tiketi yangu na kuingia uwanjani bila ya shida na tiketi ikanipeleka katika kiti changu bila ya bughudha. Kwanini niende uwanjani saa sita mchana katika mechi ambayo inachezwa saa mbili usiku?

Pambano linapoisha ghafla uwanja unakuwa mtupu kwa sababu kuna mageti mengi ya kutokea. Palepale nyuma ya jukwaa ambapo uliingilia ndio palepale unatokea. Hakuna rabsha katika kuingia wala hakuna rabsha katika kutoka uwanjani. Kwanini uwahi mapema zaidi kwenda uwanjani?

Kitu kibaya zaidi ni kwamba tunaliweka jambo lenyewe kama vile ni sifa wakati ni wazi kwamba jambo lenyewe linatushushia hadhi. Naamini baada ya mechi hizi mbili kuna mashabiki kibao ambao wamejiapiza kutorudi tena kwenye Uwanja wa Mkapa kutazama mechi za watani. Tunapoteza mashabiki.

Lakini pia kuna watoto kibao waliobebwa na wazazi wao wamepata adha ambayo wamejiapiza wakiwa wakubwa hawataenda uwanjani. Tunapoteza mashabiki. Wanaorudi tena na tena na ni wale manunda ambao wamezoea adha za Uwanja wa Mkapa. Wengine ni wazi kwamba wamekacha. Hawana muda tena.

Matokeo yake kila siku mashabiki wamekuwa wakikimbia Uwanja wa Mkapa. Tunajiuliza kwanini mashabiki hawaendi uwanjani? Kwa shida kama hizi za kuingia uwanjani mashabiki wanabaki nyumbani kutazama mechi katika televisheni. Kule wanaziona mechi vizuri na pia wanatazama marudio ya mgando kwa mambo yanayoendelea uwanjani. Kunguru muoga hukimbiza mbawa zake.

Wengine wanakwenda baa au vibanda umiza. Kule wanapata bahati ya kutazama mechi mbalimbali kwa wakati mmoja. Huku unaangalia Simba dhidi ya Kagera Sugar upande mwingine unatazama Manchester City dhidi ya Arsenal. Kwanini uende katika adha za Uwanja wa Mkapa? Hapa ndipo tumepoteza mashabiki. Hatutaki kutazama ushindani huu wa kibiashara na kila siku utaratibu wa kuingia Uwanja wa Mkapa umekuwa mbovu.

Matokeo yake wasemaji wamekuwa wakisifiwa kwa kuwaita watu uwanjani. Zamani enzi hizo za kina Zamoyoni Mogella hakukuwa na wasemaji na watu walijaa uwanjani kwa sababu hakukuwa na televisheni wala ushindani wa biashara wa soka la nje. Leo watu wanaoitwa wasemaji wamekuwa wakipambana kuita watu uwanjani bila mamlaka husika kujua tulikosea wapi.

Imefikia mahali hata mechi za Simba na Yanga zinalazimika kupigiwa debe mashabiki waje uwanjani. Mwenyeji akiwa Simba basi kuelekea katika pambano msemaji wa Simba analazimika kupambana kwelikweli ili mashabiki waje uwanjani. Vivyo hivyo mwenyeji akiwa Yanga.

Kama utaratibu wa kuufikia Uwanja wa Mkapa na kuingia uwanjani ungekuwa mzuri, leo hata mechi za kawaida za Yanga dhidi ya Namungo zingekuwa zinaleta mashabiki mara mbili ya wale ambao wamejitokeza. Hata hivyo, mashabiki wamekuwa wakikariri adha ambazo wanazipata katika mechi hizi na wanaamua kukaa nyumbani.

Kwenda uwanjani ni starehe, lakini kwa Tanzania sio starehe. Ni vita. Kwenda uwanjani unapaswa kuwa mtoko lakini kwetu sio mtoko. Kila siku tunapoteza watu ambao wanakwenda uwanjani halafu baada ya hapo tunaanza kuhangaika kuwarudisha tena kwa kupiga kelele nyingi katika redio kuwaomba mashabiki wajitokeze uwanjani.

Na tunalitazama suala la kufurika uwanjani saa sita mchana kama sifa kumbe ni ujinga unaotokana na hofu tuliyo nayo katika kuingia uwanjani. Wenye akili timamu wanapaswa kuchukua hatua. 

Bahati nzuri wenye mamlaka pia wamepata fursa ya kwenda nje ya nchi na kuona mambo yanavyokwenda. Sijui kwanini hawatengenezi utaratibu madhubuti kwa ajili ya kurekebisha hali ilivyo.

Related Posts