Kigoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amemuelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kujenga kituo cha polisi katika Kata ya Mwandiga iliyopo Kigoma vijijini, kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025.
Dk Nchimbi ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2024 wakati akisalimia wananchi wa Mwandiga, akielekea Kasulu kuendelea na ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Kigoma.
Akiwa Mwandiga, wananchi walikuwa wamebeba mabango mawili; moja linasema “tunaomba kujengewa kituo cha polisi Mwandiga” na lingine linasema “tunahitaji kituo cha afya”, jumbe ambazo zimemfikia Dk Nchimbi moja kwa moja.
Akizungumza na wananchi hao, Dk Nchimbi amesema amepokea kero na amemuelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani kufanya utaratibu wao kuhakikisha eneo hilo linapata kituo cha polisi.
“Wakati nakuja nimeona mabango yenu, nimevutiwa na mabango yenu, kuna moja linasema tunaomba kujengewa kituo cha polisi na lingine linasema tunahitaji kituo cha afya.
“Namuelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani (Masauni), kituo cha polisi kipatikane hapa kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Mkuu wa Mkoa (Thobias Antengenye), shirikiana na waziri kuhakikisha kituo hicho kinapatikana hapa,” amesema Dk Nchimbi.
Katibu mkuu huyo ameongeza ukiona wananchi wanaomba kituo cha polisi, ni ishara kuwa ni watu wema, hivyo amewapongeza kwa hilo.
Kuhusu ombi la ujenzi wa kituo cha afya, Dk Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kuhakikisha kata hiyo inapata kituo cha afya kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025.
“Namwelekeza Waziri wa Tamisemi, natambua ni mchapakazi mzuri, ahakikishe kituo cha afya kinajengwa Mwandiga kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” amesema mtendaji huyo mkuu wa CCM.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Assa Makanika amesema Kata ya Mwandiga ina zahanati, lakini kwa sababu ya ongezeko la watu, zahanati hiyo haitoshelezi mahitaji, hivyo wanaomba kujengewa kituo cha afya.
“Mkoa wetu sasa umefunguliwa kwa upande wa barabara, lakini tuna barabara moja ambayo nayo ikijengwa kwa lami tutakuwa tumefunguliwa. Tunaomba Serikali itukamilishie ujenzi wa barabara inayounganisha kata zetu kwa kiwango cha lami,” amesema mbunge huyo.
Kwa upande wake, mkazi wa Mwandiga, Stella Kiza amesema wanakabiliwa na changamoto ya maji na kutopatikana kwa huduma ya umeme katika eneo hilo, hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha wanapata huduma hizo za kijamii wakati wote.
“Mwandiga hatuna maji, tunapata shida sana, tunaomba Serikali ituletee maji safi, ili nasi kinamama tupumzike kutafuta maji umbali mrefu,” amesema mwananchi huyo.
Kuhusu kufungwa kwa Ziwa Tanganyika, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema wapo wanasiasa wa upinzani wanapotosha kuhusu suala la kufungwa kwa ziwa hilo, amesisitiza limefungiwa kwa muda, ili kuruhusu samaki kuzaliana na likifunguliwa litakuwa na manufaa makubwa kwao.
“Hili ni ziwa lenu likifunguliwa siku chache zijazo, mtapata samaki wa kutosha na tumeanza kusikia kwamba samaki wameonekana, jambo linaloongeza matumaini kwao na kwa Serikali,” amesema Makalla.