MAMBO ni moto. Miamba ya soka ya Afrika, Al Ahly na Esperance Tunis ndiyo itakayochuana kwenye mchezo wa fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuwasukuma nje wapinzani wao kwenye mechi za nusu fainali usiku wa Ijumaa.
Al Ahly ilikuwa nyumbani huko Cairo, Misri kukipiga na TP Mazembe katika moja ya mechi za kibabe kabisa na wenyeji kushinda 3-0, shukrani kwa mabao ya kipindi cha pili ya Mohamed Abdelmonem, Wessam Abou Ali na Akram Tawfik.
Mechi ya kwanza iliyofanyika DR Congo, timu hizo zilitoka sare ya bila ya kufungana.
Huko Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria, Mamelodi Sundowns ilishindwa kutumia vyema fursa ya kucheza nyumbani dhidi ya Esperance na kuchapwa 1-0 na kusukumwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-0, kufuatia kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Tunisia.
Rayed Bouchniba ndiye aliyewazima Mamelodi kwao kwa bao safi la kipindi cha pili na hivyo kuhitimisha safari ya Wasauzi hao kwenye michuano hiyo baada ya kuvuka kwa kutata kwenye robo fainali dhidi ya Yanga ya Tanzania.
Al Ahly ilipiga mashuti 16, huku 10 yakilenga goli, wakati Mazembe imepiga mashuti 11 na ni mawili tu ndiyo yaliyolenga goli la wapinzani wao. Miamba hiyo ya Misri ilipiga jumla ya pasi 445 huku pasi 350 zikiwa sahihi dhidi ya Mazembe iliyopiga pasi zote 342 na zilizokuwa sahihi ni pasi 222.
Huko Loftus Versfeld, Mamelodi ilimiliki mpira kwa asilimia 72 na kupiga mashuti 27, huku sita yakilenga goli, wakati Esperance ilimiliki mpira kwa 28 na kupiga mashuti sita, matatu tu ndiyo yaliyolenga goli na moja likitinga nyavuni. Mamelodi ilipiga pasi 491 na zilizokuwa sahihi ni 385, huku Esperance ilipiga pasi 208 na pasi 102 zikiwa sahihi.
Mechi ya kwanza ya fainali itapigwa Jumamosi, Mei 18 kwa Esperance kuwa mwenyeji huko Tunisia, wakati ya marudiano itapigwa, Jumamosi, Mei 25 huko Misri, ambapo Al Ahly itakuwa wenyeji. Patachimbika.