Mbeya. Changamoto ya upatikanaji wa nyama katika Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, huenda ikabaki historia baada ya kuanzisha mradi wa shamba la ufugaji wa ng’ombe wa nyama utakaohudumia soko la nyama kitaifa.
Halmashauri ya Mji Njombe imekuwa ikipitia changamoto ya upatikanaji wa nyama, ikitegemea mnada wa Mbarali mkoani Mbeya kukidhi mahitaji, huku kilo ya kitoweo hicho ikiuzwa kati ya Sh 10,000 hadi Sh 12,000 kulingana na aina ya nyama.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 5, 2024 kwenye maonyesho ya kilimo Nanenane yanayofanyika Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya, meneja wa shamba la Iselembu, John Wilson amesema matarajio yao ni kumaliza tatizo la upatikanaji nyama kuanzia halmashauri, mkoa hadi Taifa.
Amesema mradi huo unafuga ng’ombe wa kisasa aina ya boran na tangu kuanza mwaka 2019, wamefikisha 140, huku 40 wakiuzwa na kwamba mkakati wao ni kumaliza tatizo la uhaba wa nyama.
“Changamoto tunayopitia ni ukosefu wa malisho, eneo tulilonalo halitoshi japokuwa tunaendelea kuwasiliana na Serikali kuona namna ya kutuwezesha eneo la kutosha, ili kufikia malengo.
“Tumekuwa na uhaba wa nyama katika halmashauri yetu hata mkoa kwa ujumla, tunatarajia hadi miaka 10 ijayo tatizo hili liwe historia, kwani mbali na kuhudumia Njombe, tutafika hadi ngazi ya kitaifa,” amesema Wilson.
Meneja huyo ameongeza kuwa malengo yao ni kuzalisha ng’ombe 5,000 ambapo kwa sasa uzalishaji umefikia ndama 80 kwa mwaka na kwamba boran wana faida kutokana na kuwa na uzito mkubwa kuliko wale wa kienyeji.
Amesema wamekuwa wakipitia wakati mgumu kwenye upatikanaji wa chakula cha mifugo hiyo, hivyo kulazimika kufuata nyasi mkoani Mbeya ikiwagharimu Sh 5,500 kwa kila mzigo, huku mahitaji ni kilo 25 kwa siku.
“Utofauti wa ng’ombe huyu na wengine ni uzito, wanaweza kuwa na uzito kati ya kilo 200 hadi 300 ikiwa ni zaidi ya mara tano na wale wa kienyeji, tumeamua kulima mahindi ambayo tunayaandaa kwa ajili ya chakula kukwepa gharama kubwa ya kusafirisha kutoka Mbeya,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mifugo katika halmashauri hiyo, Daniel Mbata amesema kutokana na mradi huo wa kimkakati, wanatarajia kutoa mbegu bora za nyasi na kupanua eneo la malisho.
Amesema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa nyama, wameelekeza kila kata iwe na mtaalamu wa mifugo, ikiwa ni kushawishi watu wengi kujikita kwenye ufugaji.
“Tatizo la wafugaji wengi ni kutoanza na sehemu ya malisho, matokeo yake chakula cha mifugo kinapungua, hivyo sisi Serikali tutatafuta mbegu bora za nyasi na kuzungumza na Serikali ya kijiji cha Mtila ili kumuongezea eneo.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika halmashauri ya mji huo, Thadei Luoga amesema katika mapato ya ndani ya Sh9.4 bilioni watatenga asilimia nane kati ya 10 kuwekeza katika ufugaji kwa makundi ya vijana.
“Tunaiona fursa kubwa katika ufugaji, hili shamba la Iselembu ndilo litakuwa sehemu ya darasa na tutatenga asilimia nane kuwawezesha makundi ya vijana kujikita katika ufugaji wa ng’ombe wa nyama,” amesema Luoga.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo, Erasto Mpeta ameomba shamba la Iselembu kutumia maonyesho ya wakulima kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja na makundi tofauti kujifunza teknolojia mbalimbali za ufugaji.