Njombe, Makete. Takriban miongo miwili iliyopita ilikuwa ni jambo la kawaida kuzika watu watatu mpaka wanne kwa siku waliofariki kutokana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) wilayani Makete.
Wilaya hiyo ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na maambukizi VVU nchini na kupitia wakati usioelezeka, hasa ilipofikia hatua ya viongozi wa kaya (baba na mama) kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo na kuwaacha watoto wakiwa yatima.
Eneo hilo lililobarikiwa ustawi wa viazi, mahindi, ngano na mazao ya mbao yatokanayo na misitu, utajiri huo haukuonekana kutokana na janga la Ukimwi lililoikumba wilaya hiyo miaka ya 1990 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Haikuishia hapo. Mwaka 2003 kaya nyingi ziliathiriwa na baa la njaa kutokana na kupungua kwa uzalishaji mali, hali iliyowalazimu walio wengi, hasa vijana, kuhama eneo hilo na kwenda kufanya biashara katika maeneo mengine ya nchi.
Maambukizi ya VVU ni kati ya mambo yaliyochangia idadi kubwa ya familia na vijana kuondoka eneo hilo kwenda kutafuta afadhali ya maisha katika miji mikuu ya nchi kutokana na hofu ya kupata maambukizi.
Taratibu uchumi wa wilaya hiyo ukaanza kudidimia na kukosekana maendeleo kama ilivyo maeneo mengine, ikiwemo barabara ambayo ndiyo kichocheo cha uchumi wa eneo lolote.
Miaka 10 imepita tangu nilipozuru wilayani hapa (mwaka 2013) na kushuhudia nyumba kadhaa zikiwa hazina wazazi na watoto wakiwa peke yao.
Miongoni mwa vijiji nilivyovitembelea ni Ivalalila ambacho wakazi wake walikuwa wanawake zaidi ikilinganishwa na wanaume kutokana na wengi kufariki dunia kwa ugonjwa wa Ukimwi.
Waliokuwepo ni wazee wachache na vijana wa kiume chini ya miaka 30, ambao hata hivyo walikuwa na tabia hatarishi.
Uchunguzi nilioufanya Septemba 2013, ulibaini mwanamume mmoja alikuwa na wastani wa wanawake sita, wengi wao walikuwa wajane na kinamama waliowazidi umri.
Machi 31, 2023 miaka 10 baadaye nilitembelea kijiji hicho na kushuhudia mabadiliko makubwa. Licha ya maendeleo yaliyopo, nilishuhudia jamii iliyostaarabika, yenye mitazamo chanya na uelewa mpana kuhusu virusi vya Ukimwi na namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU.
“Kwa sasa suala la maambukizi ya virusi vya Ukimwi linafahamika, wananchi wanafahamu jinsi ya kujikinga na hata wanaotumia dawa wapo makini maana wameshaona madhara yaliyowapata wale ambao hawakufuata masharti ya dawa,” alisema Emanuela Konzo (37) mkazi wa kijiji hicho.
Pamoja na mafanikio ya kijiji cha Ivalalila, hali ya maambukizi ya VVU wilayani Makete kwa sasa ni tofauti na zamani kutokana na elimu kutolewa kwa jamii.
Hata hivyo, kuna mambo kadhaa yaliyosababisha virusi vya Ukimwi kusambaa kwa kasi katika wilaya hiyo.
Wakazi wilayani hapa wanataja mila na tamaduni za kabila la Wakinga ambazo zilikuwa kichocheo cha kuenea kwa kasi maambukizi kutokana na kurithishana wake, licha ya uwepo wa wapenzi zaidi ya mmoja na kuoa wake wengi.
Imani potofu kuamini kulogwa, wanaume kuondoka kwenda mbali na familia zao kama njia mojawapo ya uzazi wa mpango na ulevi wa kupindukia wa pombe za kienyeji.
“Kwa desturi yetu sisi Wakinga, kwa mfano mimi nina mke nikifariki ndugu yangu mwanaume awe mkubwa au mdogo kwangu, lazima amrithi mke wangu niliyemuacha bila kujua nimekufa kwa tatizo gani, anamrithi tu,” anasema Benito Chengula.
Anasema mila hiyo inatambulika tangu zamani na mwanamke hawezi kukataa kwa kuwa anajua jukumu la kurithiwa na shemeji yake au ndugu yeyote upande wa mumewe ambaye watakubaliana.
“Sasa kama mwanamke alishapata maambukizi yule anayemrithi atajikuta naye anayapata, hivyo kwenye ukoo kunaweza kujikuta wanaume wote mnapukutika kwa ajili ya mke mmoja tu,” anasema Benito.
Miongoni mwa mambo yaliyochochea maambukizi katika wilaya hiyo ni mwingiliano wa watu. Wakazi wanasema walifika watu kutoka maeneo mbalimbali kununua ngano, viazi na kupasua mbao.
Licha ya wageni kuingia katika wilaya hiyo, pia wakazi hao hasa wanaume walikuwa na desturi ya kukaa muda mrefu porini wakipasua mbao, hivyo walianzisha mahusiano na wanawake wengine.
Akisimulia, Benito anasema kwa kipindi cha miaka ya 2000 mpaka mwaka 2007 wilaya hiyo ilizika watu watatu mpaka wanne kwa siku.
“Kabla dawa hazijafika tuliwapoteza ndugu zetu wengi, hatukupata nafasi ya wapi tukapime, wapi tukapate dawa kama una maambukizi. Huduma hiyo haikuwepo kwa miaka ile ya 2003 mpaka 2004 hali ilikuwa mbaya zaidi na watu walikufa wengi.
“Kwa siku mnaweza kuzika watu watatu lakini bado mnakuwa mmeacha wengine kwamba mtazika kesho, tulipoteza ndugu zetu wengi kutokana na ugonjwa huu.
“Baada ya watu kuwa na utamaduni wa kupima na kuanza kutumia dawa, hali imekuwa shwari na maambukizi yamepungua, sehemu kubwa iliyobaki ni maambukizi ya zamani kwa kuwa mapya ni machache,” anasema Benito, ambaye ni mwenyekiti wa baraza la watu wanaoishi na VVU wilayani Makete (Konga).
Muuguzi aliyefanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 katika hospitali ya Wilaya Makete, Erica Kabelege anasema, “Kila siku walikufa watu zaidi ya watatu na ilifika muda jamii ilishindwa kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na badala yake kushinda wakizika. Makete kulikuwa na ile mila kwamba mtu akifa basi wataomboleza kwa wiki mbili, uchumi ukashuka.”
Martin Mponzi (22) ni miongoni mwa vijana waliozaliwa na maambukizi ya VVU. Anasema ilimchukua muda mrefu kuanza kupewa dawa baada ya kugundulika kuwa na maambukizi akiwa na miaka mitano.
“Waliozaliwa na maambukizi wapo 58 kwa eneo la wilaya nzima, hao ndio wamejisajili, wengine hatuna taarifa zao,” anasema Mponzi, ambaye ni katibu wa Konga wilayani Makete.
Mponzi ni miongoni mwa vijana waliolelewa katika familia, licha ya wazazi wote kupata maambukizi. Wapo watoto waliopoteza wazazi na hata ndugu wa pembeni hivyo kulelewa katika vituo vya malezi.
Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Fema Matamba, Ala Mbwilo anasema kituo hicho chenye watoto 12 sasa, kiliendelea kuwapokea mpaka mwaka 2010.
“Tulipokea watoto wa kike na wa kiume, kituo kiliangalia wenye mazingira magumu zaidi. Wapo waliomaliza vyuo na wengine wapo sekondari, kwa sasa hatuna tena watoto wadogo, maana wengi tuliwapata baada ya wazazi wao kufariki kwa ugonjwa wa Ukimwi,” anasema.
Kituo cha yatima Bulongwa kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kusini Kati Makete, kilianzishwa mwaka 1990 na kilihudumia watoto wengi zaidi, mkuu wa kituo hicho kwa sasa, Vaileth Haule anasimulia:
“Kuna nyakati tulipata watoto wengi mpaka 36, wakati huo changamoto ilikuwa ugonjwa wa Ukimwi uliosababisha vifo vya wazazi na wengine mama zao wakifariki wakati wa kujifungua, lakini kwa sasa tunavyoendelea wamezidi kupungua,” anasema.
Vaileth anasema wamekuwa wakiwarudisha kwenye jamii pindi wanapofikisha umri wa miaka 18 na kwa sasa hali imekuwa tofauti siyo kama zamani, kituo kina watoto 16 pekee, wengi wakiwa ambao mama zao walifariki wakijifungua.
Kwa nini Makete iliongoza kitakwimu
Wakati takwimu zikionyesha wilaya hiyo iliathiriwa zaidi kulinganisha na maeneo mengine nchini, Festo Sanga, Mbunge wa Makete (CCM) anasema maambukizi kwa sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa.
“Nimezaliwa Makete, nimekulia huko, nimesoma huko mpaka sasa hivi niko Makete, suala hilo lipo katika jamii yangu na limenikuta katika familia yangu. Makete ya mwaka 2000 mpaka 2010 ilikuwa na hospitali mbili, Ikonda na Bulongwa.
“Takwimu zilikuwa zinachukuliwa Ikonda, wagonjwa wengi walikuja pale wakitokea maeneo tofauti Mbeya, Njombe, Iringa na kwingineko, anapimwa pale anagundulika na takwimu zilibaki pale kuonyesha ni watu wa Makete,” anasema.
Sanga anasema idadi ya watu kwa sasa katika wilaya hiyo ni 109,600, hivyo kipindi cha nyuma walikuwa wachache na matumizi ya kondomu yalichelewa sana.
“Kwa sasa hospitali zimekuwa nyingi, kuna upatikanaji wa vipimo, tohara na elimu. Nimekulia katika jamii ambayo mtu akitumia kondomu ataifua na kuianika, kwa sasa zinapatikana kwa urahisi,” anasema.
Sanga anasema sehemu kubwa ya jamii iliyopata maambukizi imekubali kwamba ina ugonjwa na ipo tayari kuwalinda wengine wasipate. “Wanachukua dawa bila kujificha sababu wapo tayari kuwalinda wengine.”
Wilaya hiyo anasema imekuwa na mipango mikakati, ikifanya kazi kwa kushirikiana na watumishi wa afya, taasisi za kidini, shule na asasi za kiraia.
“Barabara imejengwa. Zamani tulitumia siku tatu mpaka nne kufika Makete, lakini sasa unatumia saa moja na nusu. Imefungua fursa za kiuchumi na biashara. Wananchi wengi wa Makete wanaishi maeneo mbalimbali. Imesaidia na wao sasa wanakuja kuwekeza nyumbani na kujenga nyumba za kisasa, kufungua biashara na watu wameongezeka.
“Sasa inajengwa barabara kutoka Makete kwenda Mbeya, mkandarasi ameshapatikana na itakuwa na urefu wa kilomita 97, ataanza na kilomita 39,” anasema Sanga.
Akitaja mikakati iliyotumika kupunguza maambukizi, Mganga Mkuu Wilaya ya Makete, Ligobert Kalisa anasema ni elimu kwa jamii kuhusu njia za kupata maambukizi, njia sahihi za kujikinga, kuwezesha upatikanaji wa kondomu, kuhamasisha tohara ya hiari kwa wanaume na watoto wachanga.
Anasema wamehamasisha upimaji wa hiari kwa wasiotambua hali zao, elimu kwa njia ya redio juu ya unyanyapaa, kufanya upimaji kwa makundi hatarishi na wanaotambulika kutokuwa na maambukizi kuanzishiwa dawa kinga za PrEP ili kupunguza maambukizi kwenye makundi hayo.
Akielezea mwenendo wa wagonjwa, Dk Kalisa anasema kwa sasa idadi ya wanaolazwa kwa magonjwa nyemelezi imepungua, kulinganisha na miaka ya nyuma ambayo asilimia kubwa ya waliolazwa kama siyo wote walikuwa wanaotokana na VVU.
“Tumefanikiwa kupambana na maambukizi. Katika kufikia malengo ya kidunia ya kudhibiti maambukizi mapya ifikapo mwaka 2030, Makete kupitia ofisi ya mganga mkuu wa wilaya imeendelea kufanya vizuri katika vipengele vikuu vitatu (95, 95, 95)” anasema.
Akifafanua vipengele hivyo, anasema katika asilimia 95 ya wanaoishi na maambukizi kupima na kujua hali yao, Makete imefanikiwa kwa asilimia 106.8.
“Asilimia 95 ya waliopima na kugundulika wanaanzishiwa dawa za kufubaza makali ya VVU, tumefanikiwa kwa asilimia 98. Asilimia 95 ya walioanza dawa wafanikiwe kufubaza VVU kikamilifu na kuwa na uwezo mdogo wa kuambukiza wengine, hili tumefanikiwa kwa asilimia 99,” anasema.
Kuhusu watoto waliozaliwa na maambukizi na vijana, Dk Kalisa anasema wanawafuatilia kwa kuwasiliana na wazazi wao, kupitia watoa huduma ngazi ya jamii, klabu mashuleni na kliniki zao vituoni.
Anataja takwimu za watoto waliozaliwa na maambukizi kuwa ni wawili mwaka 2021, watatu mwaka 2022 na wawili mwaka 2023.
Kuhusu maambukizi mapya ya VVU, Dk Kalisa anasema, “Maambukizi yameendelea kupungua kutoka asilimia 11 mwaka 2015 ambapo kati ya watu 8,452 waliopimwa, wenye maambukizi walikuwa 925 mpaka kufikia asilimia 3.8 mwaka 2022 ambapo waliopima walikuwa 20,658 na waliokutwa na maambukizi walikuwa 796.”
Hata hivyo, anasema takwimu za nyuma ambazo hazikurekodiwa, wengi walifariki kwa ugonjwa huo. Miaka iliyokuwa na vifo vingi anasema ni 2000 mpaka 2005 mwanzoni kabla ya dawa (ARV) hazijaanza kutolewa.
Anasema idadi ilianza kupungua mwaka 2006 hadi 2008 baada ya kuwapo mwitikio wa waathirika kujiunga na matibabu.
Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk Anath Rwebembera anasema ingawa kwa sasa maambukizi Makete yamepungua, utafiti wa viashiria vya Ukimwi ndicho kigezo cha kufahamu hali ya maambukizi. Alisema utafiti wa mwisho wenye matokeo ni uliofanyika mwaka 2016/2017.
“Utafiti mwingine umeshafanyika mwaka 2022/2023 na majibu yanatazamiwa kupatikana mwaka huu. Utafiti huu ndiyo utatuambia hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi nchini, pamoja na sababu za mabadiliko yoyote yatakayopatikana,” anasema.
Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation