Kasulu. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameingilia kati suala ya kata ya Kagerankanda kukosa diwani kwa miaka mitatu sasa, kwa kumwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Ezekiel Kabonge alivuliwa udiwani mwaka 2021 kwa madai hakuwa raia wa Tanzania, tangu wakati huo kata hiyo haijapata diwani mwingine.
Kero hiyo iliwasilishwa pia na wananchi Februari 2024 wakati wa ziara ya aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda. Hata hivyo, haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa na wananchi wa kata hiyo hawana mwakilishi.
Akiwa kwenye mkutano wake wa hadhara leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Dk Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kwenda Kasulu kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
“Kuna suala la diwani wa Kagerankanda aliyesimamishwa kwa muda mrefu. Namuelekeza Waziri wa Tamisemi, ndani ya siku 40, aje alimalize tatizo hili,” amesema Dk Nchimbi, huku akishangiliwa na wananchi kwenye mkutano huo.
Wananchi hao wamekosa uwakilishi katika ngazi ya kata kutokana na mzozo huo na sasa umebaki takribani mwaka mmoja kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwingine ambapo wananchi watamchagua Rais, mbunge na diwani wao.
Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi ameielekeza Wizara ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kushughulikia kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika wilaya hiyo, wakati ikiendelea na mipango ya kuunganisha mkoa huo kwenye gridi ya Taifa.
“Namwagiza Waziri wa Nishati kupunguza kukatikakatika kwa umeme hapa Kasulu, wakati taratibu nyingine zikiendelea,” amesema katibu mkuu huyo wa CCM.
Awali, mbunge wa Kasulu, Profesa Joyce Ndalichako amemweleza Dk Nchimbi kwamba jimbo lake limepokea fedha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, hata hivyo, ameomba kumaliziwa kwa ujenzi wa kituo cha afya Mwami Ntale ambacho Serikali ilitoa Sh300 milioni, sasa zimesalia Sh200 milioni ili kukamilisha ujenzi huo.
Akijibu changamoto hiyo, Dk Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Tamisemi kutafuta fedha hizo (Sh200 milioni) kabla mwaka huu haujaisha, ili zikamalizie ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa ameeleza aliamua kujiunga CCM baada ya kuona chama chake cha zamani hakina dhamira ya dhati na uwezo wa kutatua kero za wananchi.
“Pamoja na vyama tulivyonavyo, tuna nchi ya kujenga,” amesema Msigwa wakati akizungumza kwenye mkutano huo, huku akiwataka wananchi waachane na vyama vya upinzani.
Wakati huohuo, DK Nchimbi amewapokea wanachama wapya 24 waliotoka vyama vya ACT Wazalendo na Chadema. Pia alipokea kero 146 kutoka kwa wananchi 108 zimepokelewa kwenye mkutano wake na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.