Dar es Salaam. Pamoja na jitihada zinazofanywa na wataalamu wa afya katika utoaji wa elimu juu ya unyonyeshaji kwa kinamama wanaojifungua, jamii inayowazunguka, ikiwemo mama mzazi wa mwanamke aliyejifungua au mkwe wamekuwa kizingiti.
Hiyo ni baada ya wao kutumia uzoefu wa walichokifanya wakati wakinyonyesha miaka mingi nyuma, jambo ambalo linaweka ugumu, hususani kwa mama anayejifungua kwa mara ya kwanza kufuata yale aliyoambiwa hospitali.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 5, 2024 katika mjadala wa X space (zamani Twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), ikiwa na mada isemayo “Namna ya kutatua changamoto na kusaidia unyonyeshaji kwa watoto.”
Mjadala huo umeshirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini ambao wameeleza faida na hasara ya mtoto kutonyonyeshwa ipasavyo.
Mhariri wa Afya wa Mwananchi, Herrieti Makwetta akichokoza mada hiyo amesema wakati takwimu zikionyesha idadi kubwa ya watoto wanazidi kukataa kunyonya ziwa la mama kabla ya kutimiza miezi 24, chuchu bandia inayotoa maziwa mengi kwa urahisi na mama kukaa mbali na mtoto kwa muda mrefu zimetajwa kuwa sababu watoto wengi kususa ziwa.
“Mtoto kukataa kunyonya humnyong’onyesha sana mama na kumpa mawazo mengi, hata hivyo wataalamu wamebainisha mtoto hususa kunyonya kama njia ya kumwambia mama kwamba kuna kitu hakipo sawa,” amesema.
Imeeelezwa maziwa ya mama yanamkinga mtoto na magonjwa mengi, ikiwamo surua, kuhara na nimonia.
“Mtoto anaponyonya kwa kipindi chote bila kuwa na changamoto yoyote huepuka haya magonjwa na wataalamu wa afya wamekuwa wakishinikiza sana umuhimu wa siku 1,000 za kwanza hadi miaka miwili,” amesema Makwetta.
Hata hivyo, amesema ripoti inaonyesha matumaini kwani mtindo wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee miongoni mwa watoto walio chini ya miezi sita umeongezeka zaidi kadiri muda unavyopita, kutoka asilimia 26 mwaka 1991/92 hadi 64 mwaka 2022.
Naye Ofisa Lishe mtafiti mwandamizi kutoka TFNC, Dorice Katana amesema kina mama wengi wanapenda kunyonyesha watoto wao kwa miezi sita, ila changamoto anazokutana nazo ndiyo inafanya wasitekelezeke kile walichoelekwezwa na wataalamu.
Amesema kinamama waliozaa watoto wengi katika jamii ndiyo wanaonekana wataalamu zaidi na bahati mbaya kundi hilo ni ngumu kufikiwa katika utoaji wa elimu.
“Ndiyo maana tunahamasisha mama akiwa mjamzito aje na mwenzi wake pamoja na yule anayemhudumia nyumbani, ili akijifungua amsaidie katika kupata lishe bora,” amesema Dorice, huku akiongeza kwa bahati mbaya huwa hawafiki.
Amesema kitu kinachosikitisha zaidi mjamzito pekee ndiye anayekwenda na kunufaika na elimu inayotolewa, ila anapojifungua mama mkwe au mzazi ambao wamewahi kunyonyesha wanaonekana ndiyo wenye nguvu.
“Bahati mbaya pia mila na desturi zetu huwezi kumpinga mama mkwe au mama mzazi, hivyo unakuta mama aliyejifungua anashindwa kufuata yale aliyoelekezwa na mtaalamu. Ni vyema mkazo uwekwe kwa viongozi wa dini, misikiti na kimila ambao wanaaminiwa na watu wengi,” amesema Dorice.
Sizya Puya, mama wa watoto watatu amesema baada ya kujifungua alikwenda kukaa kwa mama yake mzazi ambaye amelea watoto watano na anaona ana uzoefu wa kutosha, hivyo taarifa ya mtoto mchanga kutopewa chochote kwa miezi sita ilikuwa ngumu kwake, kwani walisema maziwa ni mepesi mtoto atakuwa hashibi.
“Niwe mkweli hili nililizingatia kwa mtoto wangu wa pili, wa kwanza nilishindwa, msukumo kwenye jamii, mtoto wa kwanza uoga sijui chochote, kila anayekuja kumuona mtoto anakuja na taarifa zake nikaona nisije kupoteza mtoto,” amesema.
Amesema hali hiyo ilifanya mtoto wake wa kwanza kukataa kunyonya maziwa alipokuwa na miezi saba, jambo lililomfanya kwa watoto wengine wawili kuzingatia unyonyeshaji kwa miezi sita mfululizo.
“Kuna kazi kubwa ya kubadili mtazamo kwa jamii kuwa inawezekana huyu mtoto akapata maziwa ya mama kwa miezi sita bila kuwekewa maji wala maji ya glucose na uji wa muhogo,” amesema.
Pia amesema ni vyema kuonyesha faida ya kunyonyesha mtoto kwa miezi 24 hasa za kiafya, hasa kwa wanaopata watoto kwa mara ya kwanza.
FAO: Maziwa ya mama ni muhimu
Mtaalamu wa Lishe wa FAO, Stella Kimambo amesema maziwa ya mama ni muhimu kwa sababu yanaimarisha taya, misuli na masikio, huku akieleza kuwa kwa sasa kuna matatizo ya maradhi ya masikio na mengine yanayotokana na kukosa maziwa ya mama.
“Changamoto iliyopo tumerithi tangu zamani ya kwamba maziwa ya kwanza yamwagwe, kwa kuwa na wasiwasi kuwa ni machafu na hizi mila zinahitaji elimu na baba akielimika anaweza kusaidia kwa sehemu kubwa,” amesema.
Kutotambua kama mtoto ameshiba pia ni changamoto nyingine ambayo inasababisha mama mzazi na mkwe kukimbilia kumpa uji mtoto.
“Kumuanzishia mtoto chakula mapema ni kumuharibia mfumo wake wa chakula kama akipewa mapema figo zinakuwa hazijajitayarisha kuchakata chakula mapema,” amesema.
Stella amesema wakati mwingine hata kinamama hao wanapochagua chakula mbadala kwa ajili ya watoto wanakuwa hawajui namna ya kukiandaa.
Akitolea mfano wa uchanganyaji wa maziwa ya ng’ombe, baadhi hawajui ni maji kiasi gani yanayopaswa kuchanganywa ili kumlisha mtoto kwa sababu protini yake ni kubwa na haihitajiki kwa mtoto.
Njia sahihi ya unyonyeshaji
Mtaalamu wa unyonyeshaji, Anitha Mganga amesema wakati mwingine changamoto huwa kwa baadhi ya watoa huduma ambao hawaweki msisitizo na mkazo wa kuwasaidia kinamama, hasa wale waliojifungua kwa upasuaji.
Hiyo ni baada ya wao kusahau kuweka msisitizo wa wao kunyonyesha mapema.
“Pia katika kuwauguza wazazi, walezi na wasaidizi wamekuwa wakiishi na yale ambayo yalifanyika zamani na wakati mwingine kumuambia mama mzazi kuwa yeye alikua kwa maziwa ya ng’ombe,” amesema Anitha.
Walichokisema viongozi wa dini
Hata hivyo, suala la unyonyeshaji si la kisanyansi pekee, bali viongozi wa dini wanaeleza kuwa pia ni maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Mwakilishi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Mratibu wa Afya wa baraza hilo, Dk Salehe Abdallah amesema kwa upande wa Uislamu unyonyeshaji ni agizo lililotolewa na Mwenyezi Mungu.
Amesema kwenye Uislamu kupitia Quran, kuna inayozungumzia unyonyeshaji wa watoto. Sura hiyo inatoa maagizo kwa wazazi wote kushirikiana kumnyonyesha mtoto kwa miaka miwili.
Katika kushirikiana huko, mama anampa chuchu mtoto ili anyonye huku baba ambaye ni mlezi anatakiwa kusaidia uwezeshaji wa lishe wa mama anayenyonyesha.
“Hawajasema umpe mtoto chakula, bali umnyonyeshe kwa miaka miwili na baba ahakikishe mama anapata chakula,” amesema.
Amesema katika Uislamu pia kuna maelekezo kuhusu lishe ambayo inasema binadamu ukila chakula tumbo ligawiwe mara tatu ambayo ni sehemu ya chakula, maji na hewa, hivyo ukila hautakiwi kushiba sana, kwani kila kitu kinapaswa kuwa na nafasi yake.
“Hii inamaanisha mama anayenyonyesha apate maji, hewa na chakula, pia tunafundishwa tusile chakula cha aina moja, bali tule chakula chenye virutubisho na mchanganyiko,” amesema.
Maneno yake yaliungwa mkono na mwakilishi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Modest Pesha anayesema watu wanatakiwa kujali mtoto, kwani ni zawadi kutoka mbinguni.
Akinukuu maandiko amesema:”Hata mbweha wanatoa matiti yao kunyonyesha watoto wao, lakini watu wangu wamekuwa wasiokuwa na huruma kama mbuni jangwani.”
Amesema hata wanapowaanda watu kufunga ndoa wanatakiwa kutaja habari za kunyonyesha kwa sababu ni jukumu muhimu kwa ajili ya afya ya watoto na ustawi wa Taifa zima.
“Tunaamini elimu ya kutosha ikitolewa, itabadili mitazamo kwa siku hii ya maadhimisho ya kunyonyesha,” amesema.