Mafuriko yalivyowaacha ‘hoi’ wajasiriamali Moro | Mwananchi

Morogoro. “Nilikuwa nimelala nikasikia upepo mkali, kuweka mkono kwenye neti pembeni ya kitanda, kumbe maji yalikuwa yameshajaa ndani.”

Hivyo ndivyo anavyoanza kusimulia Oktavina Komba, mama wa watoto wawili kuhusu mafuriko yaliyotokea eneo analoishi Kitongoji cha Kilolelo, Kata ya Msegese wilayani Malinyi Mkoa wa Morogoro.

Machi 12, 2024 usiku kulinyesha mvua kubwa mkoani Morogoro na kusababisha maji kwenye Mto Furuwa kufurika.

Baadhi ya barabara zilifungwa kutokana na maji kujaa huku nyumba kadhaa zikibomoka na watu kukosa makazi.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa miundombinu na mali nyingine za wananchi zikiwamo nyumba ni Malinyi Mjini, Lugala na Misegese.

Hata hivyo, Oktavina alishuhudia mafuriko yakiingia ghafla nyumbani kwake wakati akiwa amelala, hivyo alishtuka na kulazimika kutoka nje haraka ili kuwaokoa watoto wake huku maji yakiwa yamejaa ndani.

Kabla ya mafuriko hayo, Oktavina alikuwa mjasiriamali akiuza kuku, lakini sasa hana uwezo wa kuendelea na biashara hiyo.

“Nilikuwa nikiuza kuku watatu hadi sita kwa siku, kuku mmoja nilipata hadi Sh7,000 kipato kilichotosha kukidhi mahitaji ya familia yangu kwa siku,” anasimulia Oktavina wakati akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi.

“Lakini kwa sasa, sina tena uwezo wa kuzalisha baada ya mafuriko kuondoka na kila kitu,” anasema Oktavina.

Mkazi mwingine wa Kitongoji cha Kilolelo, Mariam Khalfan ambaye ni mama wa watoto wanne, anasema alikumbwa na hali ngumu kwa kuhama makazi yake baada ya mafuriko.

Barabara inayounganisha Malinyi mjini na ilipo Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara ikiwa kwenye ukarabati baada mafuriko kusomba daraja.

Mariam aliyekuwa akiuza uji kabla ya mafuriko kutokea, anasema amelazimika kusitisha biashara yake kutokana na hali hiyo.

 Veronica Simbeye, mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi, alikumbwa na changamoto za kusafirisha bidhaa kutokana na barabara kukatika, hivyo kusababisha biashara yake kusimama.

“Nilipata shida sana baada ya mafuriko. Usafirishaji wa bidhaa ulikwama, barabara zikakatika na bidhaa dukani zikaisha,” anasema Veronica aliyeshindwa kuongeza bidhaa dukani kwake.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Kilolelo, Kata ya Msegese, Baptisti Mandimula anasema: “Mafuriko yalianza Machi mwaka huu, yakawa makubwa zaidi Aprili na kusababisha uharibifu zikiwamo nyumba 10 kubomoka.

“Wakazi wengi walipoteza mashamba, vyombo na vyakula. Tunaiomba Serikali kuwasaidia mbegu za muda mfupi ili waweze kulima na kupata chakula.”

Asha Khatibu, mkazi wa Ifakara anasema soko la jirani na Mto Lumemo walilokuwa wanalitegemea lilijaa maji hali iliyosababisha kinamama wafanyabiashara kusitisha biashara na wengine waliamua kutembeza bidhaa mitaani.

“Mitaji iliyumba na wengine wamefilisika kutokana na maji kujaa,” anasema Khatibu.

Mfanyabiashara ndogondogo na mwenyekiti wa Kitongoji cha Mguha, Alfred Alloyce anasema walishindwa kutimiza wajibu wao kutokana na maji kujaa maeneo mengi, mashamba yalisombwa na maji, huku wananchi wachache wakiokoa mali zao.

Katika Wilaya ya Kilombero, mkazi wa Igombati, Kata ya Lumemo, Selecia Madunda alipata majanga baada ya mvua kubwa kunyesha na ukuta kumwangukia.

 “Maji yalivyokuwa mengi, kufika hospitali ilikuwa changamoto maana ilibidi wanitafutie mtumbwi ndio wakanivusha kufika ilipo barabara kuu kisha nikakimbizwa Hospitali ya ST Francis” anasema Selecia.

Kwa upande wake, Oktaviana anasema wakati wa mafuriko wanawake kwenye kitongoji hicho walipata changamoto ya ukosefu wa huduma za afya na vifaa tiba.

“Ukisema uende hospitali yetu ya wilaya huwezi kufika njia yote ni maji tu, hadi ilipo hospitali badala yake tulikuwa tunanunua dawa tunapohisi maumivu, tunameza na maisha yanakwenda,” anasema Oktaviana.

Mkazi wa Ifakara, Asha Khatibu anasema, “hospitali tunayotegemea hapa ni hii ya St. Francis, sasa wanawake wengi hususan wajawazito walikuwa wanashindwa kufika, maana wengine walikuwa wanatoka maeneo ambayo hayapitiki kutokana na maji kuwa mengi, wanawake wengi walilazimika kupanda mitumbwi ili kuwahi matibabu.”

Mkazi mwingine wa Ifakara, Zainabu Hassan anasema kipindi cha mafuriko suala la usafi halikuwepo.

“Kipindi cha mafuriko maji yalizingira eneo kubwa, sasa uchafu ukawa mwingi vyoo vikajaa na vingine kuzibuka, lakini pamoja na yote hayo hakukutokea magonjwa ya mlipuko,” anasema Zainabu.

Familia ya Khatib Makoti kutoka Ifakara, imepata pigo baada ya wajukuu zake watatu kuzama walipokuwa wakivushwa kwa mtumbwi, huku mtoto wa miezi minne akiokolewa.

Nyumba iliyobomoka baada ya mvua kubwa iliyonyesha kuanzia Machi 12, 2024 usiku mkoani Morogoro na kusababisha mafuriko.

Makoti anasema siku nne baadaye walipata mwili wa mmoja na mwingine bado haujapatikana.

Alfred Aloyce, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mguha anasema mafuriko yalisababisha vifo vya watu wawili na kuangusha nyumba sita kwenye kitongoji chake.

“Wanafunzi walishindwa kwenda shule kwa siku saba hadi 14 kutokana na maji mengi.”

Hata hivyo, Kijiji cha Igombati kiliathirika zaidi na familia saba ziliyakimbia makazi yao, huku nyumba 22 zikibomoka.

Andrea Elias, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igombani anaiomba Serikali kuweka kingo kwenye Mto Lumemo.

Anasema mafuriko yalisababisha kaya 255 kupoteza mashamba kijijini hapo.

Mshamu Bimbumbi (80) ni mzee wa Makamo mwenyeji wa Malinyi anasema, “mafuriko kama haya yamewahi kutokea mwaka 1974, lakini ya mwaka huu  yamekuwa makubwa mno, kuna Mto Fulua ambao uko jirani na hapa, inabidi usafishwe ili tusipate mafuriko maana ule mto ndio unapokea maji mengi ya kuyaleta kwenye makazi ya watu.”

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba anasema barabara zilikatika, madaraja yalisombwa na makazi ya watu yaliharibika.

Anasema hadi sasa katika wilaya yake hakuna tathimini ya kina ambayo imeshafanyika kuonyesha ni hasara kiasi gani imesababishwa na mafuriko lakini uharibifu mkubwa umetokea.

“Zaidi ya watu 3,000 walilazimika kuondoka makwao, nyumba 1,000 zilibomoka. Uharibifu huo ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 30. Serikali imeanza kurejesha miundombinu ya mawasiliano kama madaraja ili kuimarisha upitaji wa maeneo mbalimbali na kuzuia uharibifu zaidi,”anasema Waryuba.

Kuhusu elimu anasema, “shule zilizoathirika kwa kiasi kikubwa ni shule za msingi Madibila, Kiwale  na Lugala. Shule hizi ziko maeneo ya Tambarare, madarasa yalijaa maji hadi futi nne, hatukuweza kuruhusu wanafunzi waingie na hilo limesaidia kutopata madhara kwa watoto wa shule.”

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya anasema mvua kubwa kuanzia Aprili mosi mwaka huu, zilisababisha mafuriko, ziliharibu maduka, zilisomba mashamba zaidi ya eka 2000 na watu 10 walifariki dunia.

Pia, anasema kulitokea maporomoko ya udongo yaliyochangia uharibifu wa reli uliosababisha treni ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) kukwama na abiria 544 kuokolewa kwa helkopita ya kijeshi.

Kyobya anasema Serikali ilitoa tani 189 za mbegu kwa wananchi ili kuzuia njaa baada ya mafuriko.

“Barabara nyingi ziliharibika, na bajeti ya ukarabati ipo tayari. Serikali ilitoa zaidi ya Sh400 milioni kwa ajili ya ukarabati wa Mto Lumemo ili kuzuia mafuriko,” anasema.

Kiongozi huyo anasema mashamba ya miwa yalisimamisha uzalishaji kwa zaidi ya mwezi mmoja, lakini uzalishaji umeanza tena baada ya maji kupungua. Hata hivyo, anasema shule na hospitali hazikuathiriwa sana kwa kuwa ziko kwenye miinuko.

Anasema Serikali inafanya mipango ya kuweka mazingira wezeshi ili mafuriko yakitokea tena yasilete madhara makubwa.

Kyobya anasema, “uchumi wa wananchi ulisimama kwa kuwa barabara kubwa ya Ifakara mpaka Mlimba ilikatika na mpaka sasa haijakamilika.

“Ifakara ni kama Kariakoo kwa halmashauri za Mlimba, Ulanga na Malinyi, hivyo kitendo cha barabara kukatika uchumi wa halmashauri hiyo ulisimama, lakini kwa ukarabati wa miundombinu tunaamini hali ya kiuchumi kwa wananchi wetu itaendelea kurekebishika kila hatua.”

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.

Related Posts