WAKAZI wa vijiji vya Msomera na Mkababu wilayani Handeni, Mkoani Tanga wameeleza kuridhishwa na ufanisi wa kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu kufuatia ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia miongoni mwao badala ya mkaa na kuni kama ilivyokuwa ahapo awali. Anaripoti Mwandishi Wetu,Tanga … (endelea).
Kwa mujibu wa wananchi hao, tangu kuanza kwa kampeni hiyo miezi mitatu iliyopita, wakazi hao hususani akina mama wamejikita zaidi katika matumizi ya gesi huku wakitaja changamoto kadhaa ikiwemo zile za kimazingira na kiafya zilizotokana na wao kutumia mkaa na kuni kama nishati za kupikia.
Wakizungumza walipotembelewa na viongozi kutoka wilaya ya Handeni, waliokuwa wakitathmini matumizi ya nishati safi katika wilaya hiyo, akina mama hao wamepongeza jitihada za Rais Samia za kuanzisha kampeni hiyo wakisema licha ya ugeni wake tayari imeonyesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mwitikio chanya kutoka kwa wananchi hao.
“Huu ni mwezi wa tatu tangu nianze kutumia gesi, nimejiuliza maswali mengi sana na kujilaumu kwa nini nilichelewa kuanza kutumia gesi. Kwa kweli nimepata manufaa mengi sana,” alisema Teresia Simon, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Msomera na ambaye anatoka jamii ya kimaasai.
Akina mama hao ni miongoni mwa wakazi 1500 walionufaika na mitungi ya gesi kutoka kwa kampuni ya Taifa Gas, katika mpango wa ushirikiano baina ya kampuni hiyo na serikali kupitia wizara ya nishati, ambapo Taifa Gas imekabidhi serikali mitungi 10,000 kwa ajili ya wananchi wake.
Naye Mariam Khatib ambaye ni mkazi wa kata ya Chang’ombe amesema kwamba kinyume na alivyotarajia, nishati ya gesi imempa mwamko mpya katika maisha yake kwa kuwa sasa anaweza kupika chakula chake kwa haraka hasa anapotayarisha chakula cha watoto ili waweze kuenda shuleni
“Sina tatizo la kuendelea kupambana na kuni tena ninapowashughulikia wanangu kula na kurudi shule. Gesi hii imenipa unafuu sana. Pia, nimejipanga kuhakikisha kwamba inapoisha, ninaijaza mara moja kwa sababu nimegundua ni nishati ambayo inaokoa muda na mambo mengi nyumbani na kuniruhusu kufanya kazi zingine,” alisema Mariam Khatib.
Ugawaji huu wa mitungi ya Taifa Gas uliofanyika mwezi wa Mei mwaka huu ulilenga kuwafikia wakazi wa kijijini ambao hawakuwa na imani ya matumizi ya gesi.
Taifa gas, katika kufanikisha hili, walifungua vituo vya kujazia gesi katika vijiji vya Msomera na Mkababu, pamoja na duka kuu mjini Handeni ili kurahisisha upatikanaji wa gesi kwa wanaohitaji.
Meneja wa programu hiyo ambaye pia ndio anasimamia Idara ya Mahusiano ya Umma katika kampuni ya Taifa Gas, Angellah Bhoke aliesema fursa za kufungua maduka na vituo vya kujazia gesi katika program hiyo ilitolewa kwa baadhi ya wakaazi wa vijiji hivyo ili nao waweze kunufaika na fursa ya biashara kupitia mpango huo.
“Kila tunapotoa mitungi kwa umma, lazima pia tufungue maduka au vituo vya kujazia ili tuwape wepesi wananchi watakapohitaji kujaza. Kwa hivyo, Taifa Gas pia inatoa fursa za kibiashara kwa wakaazi kuweza kumiliki maduka au vituo vya kujaza gesi kama biashara zao wenyewe. Hii pia inasaidia katika kuinua maisha ya Watanzania,” alisema Bhoke.
Tangu kuanzishwa kwa kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani inayoongozwa na Rais Samia, wadau wengi wa nishati safi wamejitokeza katika kupiga jeki kampeni hii. Taifa Gas kwa mfano imechangia zaidi ya mitungi 30,000, ambayo ni sawia na shillingi billioni 2 za kitanzania katika kuunga mkono kampeni hiyo.
“Tunaendelea kufanya kazi na viongozi mbali mbali nchini wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa , wakuu wa wilaya na taasisi mbali mbali katika kufanukisha kampeni hii. Tunafuraha kwamba katika kuunga mkono kampeni hii, tumeweza kufikia kila mkoa wan chi yetu,” alisema Bhoke.
Kwa upande wao, viongozi katika wilaya ya Handeni wametoa pongezi zao kwa kampeni hii ya Rais Samia na kusema kwamba wataendelea kuipigia chapuo hadi wananchi wote wa wilaya waweze kutumia nishati safi.
“Tuna imani kwamba ujio wa gesi hapa Handeni ni mwanzo mzuri kwetu na hatutarudi nyuma. Nimeagiza kupunguzwa kwa vibali vya ukataji wa miti inayotumika kuchoma mkaa kwa sababu sasa tuna lengo kuu la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika wilaya hii”. Napongeza Taifa Gas kwa ushirikiano huu ambao umetupendelea sisi wakaazi wa Handeni” alisema Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando.
Kulingana na takwimu za kitaifa, takriban watanzania 33,000 hupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya kuni na mkaa. Vile vile, nchi inapoteza takriban heka 400,000 za misitu kila mwaka kutokana na matumizi haya. Hii ndiyo chanzo cha kampeni ya matumizi ya nishati safi nchini kama ilivyozinduliwa na serikali.