Maafisa hao walisema hayo wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 79 leo tangu shambulizi la bomu la atomiki kwenye mji huo wa Hiroshima mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.
Wahanga wa shambulizi la bomu la atomiki Hiroshima wakumbukwa
Takriban watu 50,000 waliohudhuria sherehe hiyo walikaa kimya kwa dakika moja na kengele ya amani kupigwa mwendo wa 8:15 asubuhi wakati ambapo ndege ya Marekani aina ya B-29 ilipoangusha bomu mjini humo.
Mamia ya njiwa weupe, wanaochukuliwa kuwa ishara ya amani, waliachiwa huru kuruka angani.
Soma pia:Japan yalaani vitisho vya Urusi vya nyuklia katika kumbukumbu ya Hiroshima
Katika hotuba yake kwenye eneo la kumbukumbu, gavana wa Hiroshima Hidehiko Yuzaki alisema mataifa yenye silaha za nyuklia na wale wanaotumia silaha za nyuklia kama kitisho katika vita hupuuza kwa makusudi ukweli kwamba mara tu watu wanapovumbuasilaha, huzitumia bila ubaguzi.
Yuzaki ameongeza kuwa maadamu silaha za nyuklia zipo, ni wazi zitatumika tena siku moja.
Matumizi ya nguvu katika kutatua migogoro hayaepukiki
Wakati huo huo, meya wa Hiroshima Kazumi Matsui, amesema vita vya Urusi nchini Ukraine na mzozo unaoendelea kuwa mbaya kati ya Israel na Palestina unaongeza hali ya kutoaminiana na hofu miongoni mwa mataifa na akatilia mkazo mtazamo kwamba matumizi ya nguvu katika kutatua migogoro hayawezi kuepukika.
Mateso ya watu wa Hiroshima na Nagasaki hayapaswi kamwe kurudiwa
Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, aliyehudhuria hafla hiyo amesema hofu na mateso ya watu wa Hiroshima na Nagasaki miaka 79 iliyopita hayapaswi kamwe kurudiwa.
Kishida ameongeza kuwa dhamira ya Japan, nchi pekee iliyokumbwa na vita vya nyuklia, ni kuelezea ukweli wa mashambulizi ya atomiki kwa vizazi vijavyo, kuzingatia kanuni tatu zisizo za nyuklia, na kufanya juhudi thabiti kuelekea katika utambuzi wa ulimwengu bila silaha za nyuklia.
Manusura wa Hiroshima waendeleza kampeini dhidi ya matumizi ya nyuklia
Manusura wa shambulizi hilo ambao sasa wamezeeka wanaojulikana kama “hibakusha,” wanaendelea kushinikiza marufuku dhidi ya silaha za nyuklia huku wakifanya kampeni ya kutaka juhudi zao kuendelezwa na kizazi kipya.
Soma pia:Japan yaadhimisha miaka 78 tangu bomu la Atomiki Hiroshima
Kumbukumbu hiyo inakuja siku chache baada ya Japan na Marekani kuthibitisha tena kujitolea kwa Marekani kuepusha matumizi ya nyuklia ambayo yanajumuisha silaha za atomiki, ili kulilinda taifa hilo ambalo ni mshirika wake wa Asia.
Soma pia:Mkutano wa G7: Zelensky ashinikiza mpango wa amani Ukraine mjini Hiroshima
Bomu la atomiki lililorushwa na Marekani mjini Hiroshima mnamo Agosti 6, mwaka 1945, liliharibu mji huo na kuua watu 140,000.
Bomu la pili lilidondoshwa siku tatu baadaye hukoNagasaki lilisababisha vifo vya watu 70,000 zaidi.
Japan ilijisalimisha Agosti 15, na kumaliza Vita ya Pili ya Dunia na uchokozi wa Japan wa karibu nusu karne barani Asia.