MATAMASHA ya Simba na Yanga kuelekea msimu mpya yalifanyika katika Uwanja wa Mkapa wikendi iliyopita, lakini sijaona Kombe la Afrika. Labda bado ni mapema sana. Labda ni suala la kuwa na subira. Ndoto na kiu kubwa ya mashabiki wa soka nchini ni kuona siku moja Kombe la Afrika likitua nchini.
Safari ya robo fainali kwenye michuano ya Afrika imekuwa ndiyo kituo pendwa hapa nchini. Simba hata awe bora kiasi gani, mara nyingi mwisho wake umekuwa ni robo fainalli. Yanga baada ya uwekezaji wa kizazi kipya, naye amekwama kwenye robo fainali.
Bado kuna timu kubwa Afrika ambazo zimeendelea kuwekeza kıla kukicha. Al Ahly pale Misri sio mchezo. Mamelodi Sundowns pale Afrika Kusini ni moto juu ya moto. Pengine hatupo mbali sana, lakini hatupo karibu pia.
Kwenye mchezo wa mpira wa chochote kinaweza kutokea, lakini unahitaji mipango mikubwa. Nimewaona Simba wakicheza na APR kutoka Rwanda. Nimewaona Yanga wakicheza na Red Arrows kutoka Zambia.
Ni kweli timu zetu zimeboresha vikosi, lakini sijaliona Kombe la Afrika kwa Mkapa. Uzuri wa mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa maoni. Kwa namna ulivyowaona Simba na Yanga kwa Mkapa wikendi iliyopita unaona hata timu moja inashinda ubingwa wa Afrika msimu ujao?
Binafsi napata kigugumizi kujibu ndiyo. Bado tuna safari ndefu, lakini haiondoi ukweli kuwa timu zetu zinapiga hatua kwenda mbele.
Ukiwatazama Simba wanavyocheza unaona kabisa msimu huu hapa ndani wanaweza kusumbua sana. Mechi tano za kwanza zinaweza kutumika kutengeneza kikosi cha kwanza. Kikosi chao hakina mfalme kwa sasa. Vijana wao wengi wanataka kujitengenezea majina makubwa kwa mashabiki. Kuna namna hali hii itawachochea sana kupigana uwanjani.
Bado hawajapata timu lakini kwa mchezaji mmoja mmoja unawaona kabisa mafundi ndani. Debora Fernandez naona ni mtu na nusu. Labda ni mapema sana, lakini kwa dakika alizocheza kwa Mkapa unaona kabisa jamaa ni mali.
Kutoka Zambia kwa mara nyingine Simba wameshusha mtu. Joshua Mutale akizoea mapema ligi yetu, atasumbua sana. Simba imekuwa ikiteseka sana kwenye usajili na hasa kwenye misimu mitatu ya hivi karibuni, lakini msimu huu naona imekuja tofauti. Imeshusha watu wa maana wenye umri pia mdogo.
Ukimuangalia Steven Mukwala unamuona kabisa mwanaume wa shoka. Anajua sana kujiweka kwenye nafasi na uwezo mkubwa pia wa kuwaacha walinzi. Huyu sio mshambuliaji wa kusimama mbele ya lango la wapinzani. Ana nguvu na kasi ambayo Simba iliihitaji sana pale mbele.
Je, kwa namna ulivyowaona Simba kwa Mkapa unaliona Kombe la Afrika likitua nchini? Binafsi bado nina wasiwasi. Labda ni mapema sana. Labda tujipe muda kidogo timu icheze walau mechi tano za mwanzo za ligi.
Kuna mambo makubwa mawili ambayo Yanga wamefanya kuelekea msimu mpya. Kwanza, wamefanikiwa kuwabakisha wachezaji wao wote bora. Aziz Kİ na Djigui Diarra ni wawili kati ya wachezaji waliokuwa wanatajwa kuondoka klabuni, lakini wamebaki. Aziz KI ni mchezaji bora wa ligi yetu msimu uliopita, kiungo bora na mfungaji bora. Kumbakisha ni kubakisha ubora kikosini.
Jambo la pili kubwa kwa Yanga ni kuongeza wachezaji wengi ambao sio wageni wa ligi yetu na sio wageni wa michuano ya kimataifa. Clatous Chama, Jean Baleke na Prince Dube ni baadhi ya wachezaji wapya wa Yanga ambao wote wamecheza ligi yetu kwa muda mrefu.
Uzoefu wa ligi unawapa faida Yanga. Ugeni wao ni wa timu tu, lakini mazingira yote kwao ni rafiki. Yaani kuelekea msimu ujao wanakupa tafsiri halisi ya timu yenye kikosi kipana. Nimewataza wakicheza dhidi ya Red Arrows bado sijaliona Kombe la Afrika. Huenda ni mapema sana. Huenda tunahitaji kuwa na subira. Kama Dube na Baleke wataelewa mapema jinsi Yanga inavyocheza, shida ya mabao itapungua. Aziz Kİ atakuwa amepata wasaidizi haswa.
Yanga wamefanya pia usajili wa Mwamba wa Lusaka. Chama ni mchezaji wa daraja la juu sana kwenye ligi yetu. Chama ni hodari wa eneo la mwisho la ushambuliaji. Ukiangalia kwenye makaratasi Yanga inaogopesha. Yanga inatisha, lakini uwanjani unaona ni kama bado Gamondi hajapata anachotaka.
Ukiwatazama Yanga wikiendi iliyopita ni kama bado wanajitafuta. Labda ni mapema sana. Labda tunahitaji kuwa na subira. Baada ya mechi tano za kwanza tunaweza kuona tofauti kubwa. Kila nikiwaza Simba na Yanga kwenye ubingwa wa Afrika nawakumbuka Mamelodi Sundowns na Al Ahly. Bado tuna kazi ya kufanya lakini nadhani tunaelekea kuzuri.
Mahali pekee ambapo naona kabisa tunaweza kushindana na Al Ahly na Mamelodi Sundowns ni mtaji wa mashabiki. Kilichotokea Jumamosi na Jumapili kwa Mkapa kinapaswa kuwa ni utamaduni wa kudumu kwenye mechi zote za kimataifa. Kujaza uwanja unaobeba mashabiki 60,000 haipaswi kuwa stori kubwa kwa Simba na Yanga. Simba Day na Siku ya Mwananchi ni tafsiri halisi ya ukubwa wa klabu zetu. Ule mzuka wa mashabiki ni levo ya Kombe la Afrika kabisa. Ubingwa wa Afrika ni safari ndefu, lakini tayari tumeshaianza. Tunasonga mbele.
Karibu kila msimu unaona tunapiga hatua kwenda mbele. Tunahitaji sasa uwekezaji mkubwa wa wachezaji na eneo la utawala ili kuongeza pia weledi kwenye taasisi zetu. Tunahitaji pia kuwekeza sana kwenye eneo la masoko ili kulitumia soka letu vizuri.
Kwa namna watu walivyojaa Jumamosi na Jumapili ni wazi kuwa bado hatujawatumia vizuri mashabiki wa soka kibiashara. Natamani wakati wa maandalizi ya msimu mpya timu zetu zingebaki tu hapahapa nyumbani. Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma na Dar es salaam kote mechi zingepigwa. Simba Day na Siku ya Mwananchi zinapaswa kuongezewa uzito. Mashabiki wa hizi timu zetu kubwa mbili wengi wako hapa hapa. Ni kutengeneza mkakati wa kuwafuata hukohuko mikoani. Mpira ni mchezo wa maoni. Nimewaona Simba, nimewaona Yanga. Bado tuna safari ya kuufikia ubingwa wa Afrika, lakini kuna hatua tumepiga. Tunaimarika kila kukicha.
Natamani kuwaona Simba na Yanga walau kwenye mechi tano za kwanza. Natamani kuwaona tena na tena kuona namna wanavyoimarika. Mbio za ubingwa wa Afrika zinataka watu waliokamilika karibu kwenye kila kitu.