TUMEJIPANGA KUTEKELEZA MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA- MRAMBA

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Wizara ya Nishati imejipanga ipasavyo kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kufikisha lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi katika kipindi cha miaka 10.

Mha. Mramba amesema hayo leo Agosti 6, 2024 alipotembea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na faida zake mbalimbali ikiwemo kuepusha wananchi na magonjwa yanayotokana na moshi unaotokana matumizi ya kuni na mkaa wa asili.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania kupitia Sera mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa inatambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa jitihada hizo za kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia zinafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi.

Kuhusu Maonesho ya Wakulima ya Nanenane, amesema kuwa, yamekuwa ni sehemu ya wananchi kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Sekta ya Nishati ikiwemo miradi ya Gesi Asilia na Mafuta.

Katika hatua nyingine, amesema Sekta ya Nishati inafungamanisha Sekta nyinginezo ikiwemo Madini, Maji, Kilimo na Mifugo ambapo katika Mifugo vinyesi vya wanyama hutumika kuzalisha nishati kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kutoa elimu ya kwa wananchi kuhusu mafanikio ya Sekta ya Nishati pamoja na Nishati Safi ya Kupikia.

Related Posts