Aragija kuziamua Azam, Coastal, Sasii atajwa Simba, Yanga

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imemtangaza Ahmed Aragija kutoka Manyara kuwa mwamuzi wa kati wa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha Azam FC na Coastal Union utakaopigwa, keshokutwa, Alhamisi.

Wakati huohuo chanzo cha kuaminika kimeiambia Mwanaspoti kuwa licha ya waamuzi watakaochezesha mechi kati ya Simba na Yanga kutowekwa wazi, lakini Elly Sasii ndiye atakuwa pilato wa dabi hiyo.

Mchezo huo wa Ngao ya Jamii unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni huku Coastal Union ikiwa mwenyeji.

Katika mchezo huo, Janeth Balama kutoka Iringa na Ally Ramadhani wa Zanzibar watakuwa waamuzi wasaidizi wakati Nasri Siyah kutoka Zanzibar pamoja na Victor Mwandike kutoka Mtwara ndio watakuwa waamuzi wa akiba.

Agosti 8, 2024 ni ufunguzi wa msimu wa soka wa 2024-2025  nchini ambapo zinachezwa mechi za Ngao ya Jamii kuanzia hatua ya nusu fainali, kisha mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali. Ni ubabe tu unasubiriwa kuonekana katika mechi hizo za uamuzi.

Ngao ya Jamii ya sasa ni kama ilivyokuwa msimu uliopita inashirikisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu katika ligi. Mfumo wake ni kwamba nusu fainali ya kwanza ni kati ya timu iliyomaliza nafasi ya pili (Azam) dhidi ya nne (Coastal Union), kisha ile ya pili ni bingwa (Yanga) dhidi ya aliyeshika nafasi ya tatu (Simba).

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) wamepanga mechi hizo kuchezwa siku moja. Azam dhidi ya Coastal Union itaanza saa 10 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Zanzibar, kisha Yanga dhidi ya Simba itapigwa saa 1 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
 

Related Posts