Dar es Salaam. Raia wa Nigeria, Ezeaka Oluchukwu (50) amehukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini Tanzania bila kuwa na kibali.
Oluchukwu amehukumiwa kifungo hicho, leo Jumanne Agosti 6, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya kukiri mashtaka yake mawili na Mahakama kumtia hatiani.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo atatumikia kifungo hicho gerezani.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo, mshtakiwa huyo, alijitetea anaomba apunguziwe adhabu kwa sababu alikuja Tanzania kutafuta hifadhi baada ya kushuhudia ndugu zake akiwamo bibi yake akiuawa na kikundi cha Boko Haramu.
“Naomba nipunguziwe adhabu, nilikuja kutafuta hifadhi kwa sababu nilishuhudia ndugu zangu akiwamo bibi yangu akiuliwa na Boko Haramu, kwa hiyo hali hiyo ilikuwa ina niumiza,” amedai Oluchukwu.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
“Kutokana na mshtakiwa kukiri shtaka lake mwenyewe bila kulazimishwa, Mahakama inaona ni mkosaji kwa mara ya kwanza lakini pia imezingatia kuwa upande wa mashtaka hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma, Mahakama ina kuhukumu kulipa faini ya Sh250,000 kwa kila shtaka na ukishindwa utatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani,” amesema Hakimu.
Awali, wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Mohamed Mlumba akishirikiana na Ezekiel Kibona aliiomba Mahakama itoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo.
Akimsomea hati ya mashtaka, Wakili Mlumba amedia kuwa, mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 31, 2024 Mtaa wa Agrey uliopo Wilaya ya Ilala.
Amedai siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alikutwa akiishi nchini bila kuwa na nyaraka yoyote ya inayoonyesha ni raia wa Nigeria huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo akiwa raia wa Nigeria, alikutwa akifanya biashara ya kuuza simu na vifaa vyake, bila kuwa na kibali.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka na hoja za awali (PH) alikiri kutenda kosa hilo na ndipo Mahakama ilimtia hatiani.