Moshi. Wakati Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo akisema hafurahishwi na jina la Covid-19 walilopewa Halima Mdee na wenzake 18, vyama vya CCM na Chadema, wameonesha dhamira ya kumhitaji Halima kisiasa.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amekoleza mvutano huo wa kisiasa pale aliposema Halima Mdee na wabunge hao wenzake wa viti maalum, bado ni wanachama wa Chadema huku akikwepa kuwaita Covid-19.
Wakati hayo yakijiri katika maziko ya mama mzazi wa Halima, Theresia Mdee, CCM kimemkaribisha mwanasiasa huyo kijana kujiunga na chama hicho lakini Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu akaiambia CCM kuwa watasubiri sana kama wanamhitaji Halima Mdee.
Theresia Mdee alifariki dunia Julai 30, 2024, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, baada ya kuugua saratani ya shingo ya kizazi.
Viongozi mbalimbali wakiwamo wa serikali na wa vyma vya siasa leo Jumanne Agosti 6, 2024 wameungana na mamia ya waombolezaji katika maziko hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Pumuani Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akitoa salamu katika Ibada ya mazishi iliyofanyika, Askofu Shoo amesema hafurahishwi na jina wanaloitwa wabunge hao la Covid-19 na kutaka watu waheshimiane bila kujali wamesimama upande gani.
Amesema tangu mwanzo aliwakemea baadhi ya waliokuwa wakilitamka jina hilo mbele yake na aliwahoji kwa nini wanaitana jina hilo.
“Sasa nikawauliza wanangu mmefikia huko kwa sababu za ushabiki tu, kuchagua majina ambayo hayafai ndiyo mnawaita wenzenu au mnatafuta majina ambayo hayafai ndiyo mnajiita ninyi, nikasema hapana,” amesema Dk Shoo.
Hata hivyo, amesema alichokiona leo katika maziko hayo ni alama ya upendo, utu katika jambo ambalo linamgusa kila mmoja na wameamua kuweka tofauti zao kando huku akisisitiza kuwa huo ndio upendo wa kweli wa Kimungu.
Akizungumza katika maziko hayo, Spika Tulia amesema hajawashikilia wabunge 19 wa viti maalumu (Chadema) na kwamba bado ni wabunge wa Chadema.
“Yupo mbunge mmoja hapa wa Chadema ambaye hakupata nafasi ya kutambulishwa, Aida Khenani ni wa Chadema lakini yeye siyo sehemu ya wale 19,” amesema Dk Tulia.
Hata hivyo, amesema kila mmoja anapaswa kuelewa na kukitafakari kile alichokisema Askofu Shoo kwa kina na kukizingatia.
“Nadhani wote waliokuwa wanawaita (Mdee na wenzake 19) wamemsikia baba Askofu Shoo, maana ningesema mimi jambo lolote, wangesema mimi ni mwanasiasa na yeye ndiye amewashikilia bungeni hapana, mmemsikia hapa naibu katibu mkuu, amesema maneno mazuri kabisa kuhusu wabunge hawa kupitia msiba huu na kupitia kwa mheshimiwa Halima,” amesema Spika.
Wakati akimaliza kuzungumza, Dk Tulia ametoa pia salamu za Rais Samia Suluhu Hassan kwamba anatoa pole kwa familia yote na Mwenyezi Mungu azidi kuwatia nguvu.
Akitoa salamu za kushukuru kwa niaba ya familia, Mdee mbali na kuwashukuru wote waliowakimbilia wakati wa ugonjwa na hata alipofariki mama yao, pia ameeleze namna mama yake alivyompenda Rais Samia Suluhu Hassan licha ya kuwa alikuwa mwanachama wa Chadema.
“Naomba nitoe shukrani za dhati kwa Rais Samia, mtamfikishia salamu kwa kutufariji. Mimi ni opposition (Upinzani) na sijawahi kuwa CCM na wanajua japokuwa wazazi wangu hawa wote ni makada (CCM) nadhani mnanielewa,” amesema Mdee na kuongeza;
“Lakini mimi ndiye nilimfanya mama yangu akawa opposition mpaka anafariki ni mwanachama wa Chadema, lakini mama yangu pamoja na kuwa mwanachama wa Chadema alimpenda kwelikweli Rais Samia na ilifikia kipindi tukiwa tunateta pale mambo ya kisiasa anasema ahaaa, usinigusie. Na alipokuja kumtembelea mama hospitali kama mlifuatilia zile clip, alisema umekuja sasa nitapona, naomba mnifikishie shukrani.”
Halima pia amemshukuru Spika Tulia kwa namna alivyowakimbilia kwa kipindi chote na hata kumuandaa kisaikolojia.
“Nitakuwa mtomvu wa nidhamu nisipomshukuru kiongozi wetu, ulijitahidi na ilifika mahali uliniita ukaanza kuniandaa kisaikolojia kwamba ni ngumu kupokea lakini lazima nianze kujiandaa kisaikolojia kwamba mama yako unayempenda sana iko siku ataondoka na lazima uwe imara, nikushukuru sana kiongozi wangu,” amesema Mdee.
Pia, amewashukuru viongozi wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Freeman Mbowe, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salimu Mwalimu, viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kushiriki kwa hlai na mali tangu mama yake anugua hadi umauti ulipomfika.
Akizungumza Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, amemkaribisha Halima Mdee CCM kauli ambayo ilionekana kutopolewa vizuri na waombolezaji.
“Sasa dadangu Halima kwa sababu huko kwingine hakueleweki, njoo huku” amesema Mahanyu.
Baada ya Kauli hiyo, aliposimama Naibu Katibu Mkuu Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu akasema CCM watamuota sana Halima.
“Baba paroko, kuna jambo limechokozwa, lakini limeshajibiwa, eti anafanana na huko, aliuliza Mwalimu na kujibiwa na waombolezaji hapana, kisha kusema…hafanani ee,.. basi watamuota sana,” amesema Mwalimu.
Akimzungumzia marehemu, Mwalimu amesema alikuwa mama mwenye upendo, aliyewajali na kuwafariji na kuwaombea katika magumu yote waliyokuwa wakipitia kama Chadema.
“Pamoha na kwamba tunaunganishwa naye na binti yake Halima Mdee lakini bado mama alijipambanua kwa nafasi yake kama mzazi, hakika tulimpenda sana, na leo tunaposherekea maisha yake, namuomba sana dada yangu Halima Mdee na Profesa Mdee muendelee kuwa karibu na sisi na sisi tutaendelea kuwa karibu na ninyi,” amesema naibu katibu mkuu huyo.
Amesema tupunguze chuki, uhasama ubinafsi, choyo na tuongeze upendo na kutawaliwa na roho ya furaha ili kuleta amani na furaha kwa wenzetu na tuwe sehemu ya kuchangia maisha ya wenzetu.
Naibu Waziri Tamisemi, Festo Dugange akitoa salamu amesema walipokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na kwamba marehemu ameacha alama kupitia watoto wake.