Hai. Ester Kweka, mke wa mzee wa Usharika wa Kimashuku, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Laban Kweka (50) ameeleza jinsi mumewe alivyowaandalia familia nzima nguo za kwenda kanisani Jumapili, Agosti 4, 2024 huku akiwataka kuwahi.
Mzee huyo na mchungaji wake, Kantate Munis (42), walifariki dunia Agosti 4, 2024, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye uimbaji wa Usharika wa Gezaulole Wilaya ya Hai kugongwa na basi kubwa la abiria.
Ajali hiyo ilitokea wakati mchungaji Munis alipokuwa akikata kona kuingia Usharika wa Kimashuku, anakoishi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, ajali hiyo ilitokea Jumapili, Agosti 4, 2024, eneo la Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai.
Kamanda Maigwa amesema dereva wa basi hilo amekamatwa na anashikiliwa kwa taratibu za kisheria kutokana na uzembe wa kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Agosti 6, 2024, Ester amesema mume wake alikuwa msaada mkubwa kwa familia na aliipenda.
Amesema Jumapili walipoamka, aliwaandalia familia nzima nguo za kuvaa kanisani na kuwataka wawahi bila kuchelewa.
“Siku hiyo tuliamka vizuri na siku ya Jumapili alituandalia sisi sote nguo kwa ajili ya ibada. Baadaye alitoka kwenda dukani, aliporudi alikuta bado hatujajiandaa, akatuuliza mbona mnachelewa kanisani au mnasubiri hadi kengele igongwe? Wahini kanisani,” amesimulia Ester.
Amesema waliondoka kwenda kanisani na walimuacha nyumbani akijiandaa kwenda kwenye uimbaji Usharika wa Gezaulole.
Amesema huo ndio ulikuwa mwisho wa kuonana naye, mpaka walipopata taarifa za kifo chake.
“Alikuwa ni msaada mkubwa kwangu na kwa watoto. Sasa watoto wananiuliza maswali mengi kuhusu kilichotokea kwa baba yao na siwezi kuwajibu. Tumepata pigo kubwa kwa kumpoteza baba wa familia,” amesema Ester.
Amesema mumewe kamuachia watoto watatu wote wa kike.
Ombeni Swai, mdogo wa marehemu amesema familia imepata pigo kubwa kwa kumpoteza kiungo muhimu.
“Ametuachia pengo kubwa sana. Tulipopata taarifa za ajali hii iliyoondoa uhai wa wapendwa wetu hawa, mzee Kweka na mchungaji wetu wa usharika, mioyo ilikufa ganzi hatukujua ni kipi tutafanya,” amesema Swai.
Hata hivyo, amesema mwili wa ndugu yao utapumzishwa kwenye makazi yake ya milele Alhamisi Agosti 8, 2024 nyumbani kwao Kimashuku, Kata ya Mnadani wilayani hai.
Akitoa ratiba ya maziko, Msaidizi wa Mkuu wa Jimbo la Hai, Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo, Mchungaji Dominick Mushi amesema mwili wa mchungaji Munis utaagwa katika Usharika wa Kimashuku Alhamisi saa 10:00 alasiri, kisha kupelekwa nyumbani kwao Kisamo kwa ajili ya maandalizi ya maziko yatakayofanyika Ijumaa.
“Mwili wa mzee wetu wa kanisa pia utazikwa Alhamisi katika makaburi ya familia, natoa tena pole kwa familia zote mbili na waumini wote kwa jumla,” amesema mchungaji Mushi.