Dk Nchimbi akomalia fidia ya Sh1.4 bilioni waliopisha mradi

Kibondo. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amemtaka Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha wanalipa fidia ya Sh1.4 bilioni kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kibondo – Mabamba.

Dk Nchimbi amebainisha hayo leo Agosti 6, 2024 katika Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, akihitimisha ziara yake mkoani humo.

Agosti 4, 2024, kiongozi huyo wa chama alianza ziara yake ya siku tatu mkoani humo ambapo amepokea kero za wananchi na kuzitafutia utatuzi kwa kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.

Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Kibondo, Dk Nchimbi alipokea kero za wananchi kutoka kwa Mbunge wa Muhambwe (CCM), Dk Florence Samizi ambaye amezungumzia changamoto ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara, Sh1.4 bilioni.

Dk Samizi amezungumzia pia kusimama kwa ujenzi wa barabara ya Kibondo Townlink kwa sababu mkandarasi aliyepewa kazi hizo hajalipwa fedha zake, jambo lililomfanya asitishe shughuli zake akisubiri kulipwa.

“Ndugu Katibu Mkuu, miradi hii ni muhimu sana kwetu, tunaomba mkandarasi alipwe fedha zake ili akamilishe ujenzi huo kwa wakati ili wananchi waendelee kufurqhia miundombinu hiyo,” amesema mbunge huyo wa Muhambwe.

Akizungumza kwenye mkutano wake wilayani Kibondo, Dk Nchimbi ameielekeza Serikali kulipa fidia hiyo ya Sh1.4 bilioni kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya Kibondo – Mabamba yenye thamani ya Sh60 bilioni.

“Serikali ihakikishe inalipa fedha hizi ili wananchi wapate stahiki zao. Naamini hizi siyo fedha nyingi za kumshinda Waziri Bashungwa kuzilipa kwa haraka haraka,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza.

Vilevile, Katibu Mkuu wa CCM ameitaka barabara ya Kasulu – Kibondo pia ipewe kipaumbele ili ujenzi wake ukamilike na wananchi waendelee kufanya shughuli zao za usafiri na usafirishaji kwa urahisi zaidi.

Wakati huohuo, Dk Nchimbi amemwelekeza waziri huyo kumlipa mkandarasi anayejenga barabara ya Kibondo Townlink ili aendelee na kazi kwani kwa sasa amesimamisha shughuli zake kwa sababu hajalipwa fedha zake.

Wakizungumza na Mwananchi kwenye mikutano ya kiongozi huyo wa chama, wananchi wameeleza kuridhishwa na miradi ya maendeleo inayopelekwa mkoani kwao Kigoma, hata hivyo wameitaka serikali ikamilishe kwa haraka ujenzi wa barabara ili mkoa huo ufanane na mingine nchini.

Mkazi wa Kakonko, Samuel Chaza amesema barabara ndiyo kero kubwa kwa wananchi wa Kigoma hasa Kibondo na Kakonko, hivyo ametaka serikali kukamilisha ujenzi ulioanza ili kuufungua mkoa huo.

“Tunaomba serikali ikamilishe hizi barabara katika vipande vilivyobaki. Tunataka mkoa wetu uwe kama mingine huko, tunamshukuru Mama Samia kwa kutukumbuka watu wa Kigoma,” amesema mkazi huyo wa Kakonko.

Kwa upande wake, Jesca Bukani amesema wanaokabiliwa na changamoto ya maji kwani wanahangaika kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kila siku, hivyo wameiomba serikali iwasogezee huduma hiyo kwa haraka.

“Kibondo tunataka maji, hapa kuna shida kubwa ya maji, tunaomba serikali ituletee maji,” amesema mwanamke huyo huku akielezea kwamba wamekuwa wakitumia maji ya visima ambayo si salama kwa afya zao.

Related Posts