Suala la Wenje, Lissu ‘kutikisa’ Kamati Kuu Chadema

Dar/mikoani. Ni kikao cha moto. Hivi ndivyo unaweza kuelezea kile kinachotarajiwa kutokea katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitakachoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

Kamati kuu hiyo chini ya Mwenyekiti Freeman Mbowe inakutana kuanzia Alhamisi, Agosti 8 hadi 9, 2024 ikitarajiwa mambo kadhaa yataibuka.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Agosti 6, 2024, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kamati kuu itapokea na kujadili taarifa ya hali ya siasa, usalama na mwenendo wa hali ya uchumi nchini.

Pia amesema itapokea taarifa ya awali kuhusu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, taarifa kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa na taarifa kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea katika hatua mbalimbali nchini.

Ingawa Mrema hakutaka kueleza kwa kina juu ya ajenda hizo, Mwananchi lina taarifa kwamba kikao hicho kitatoa ratiba za uchaguzi wa ngazi ya mikoa na kanda, zikiwemo za Pemba, Kusini na Pwani pamoja na uteuzi wa wagombea.

Mbali na ajenda hizo, mambo ambayo yametajwa siyo rahisi kuepukika, ni pamoja na uamuzi wa mjumbe wa kamati kuu, Ezekia Wenje kutangaza nia ya kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho-Bara.

Wenje ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Kanda ya Victoria ya chama hicho, amesema atajitosa kuomba ridhaa ya nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Tundu Lissu, suala ambalo limezua mjadala mkali mitandaoni.

Katika mjadala huo, wapo wanaosema Wenje ametumia haki yake kidemokrasia na wanaona kama amechochea mvutano kwenye uongozi kutokana na matamshi yake.

Wakati anatangaza nia hiyo jana Agosti 5, Wenje alisema ameona anastahili “kuwa msaidizi wa Mbowe”.

Kutokana na hilo, wapo wanaohoji Wenje amejuaje Mbowe atawania tena uongozi na atashinda? Je, atashikaje nafasi ya mwenyekiti wa kanda na makamu mwenyekiti taifa? Mbona ametangaza nia kabla ya kipenga cha uchaguzi ngazi ya taifa? Je, ametumwa na Mbowe kutangaza nia? Kutokana na maswali hayo, vyanzo vyetu ndani ya chama hicho, vimesema suala hilo si rahisi kupita bila kujadiliwa.

Jambo jingine ambalo kamati kuu hiyo inatarajia kukutana nalo ni suala la Lissu kueleza azma yake kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu ujao 2025.

Lissu alieleza hilo alipoulizwa na wanahabari kama bado ana nguvu zilezile za mwaka 2020 na akasema chama kikimpitisha na wananchi wakamuunga mkono atakuwa tayari.

Jana Jumatatu, Agosti 5, 2024, Wenje alizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, mbunge wa zamani wa Nyamagana amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kuongeza ufanisi wa kazi na uwajibikaji.

“Kutokana na uzoefu nilionao kwenye chama, nimejitathmini kuwa nina uwezo wa kuwa msaidizi wa Mbowe, naomba ifahamike chama chetu cha Chadema kimekuwa kikijipambanua siku hadi siku katika kupigania haki za watu, ikiwemo uhuru, haki na maendeleo,” amesema.

Uamuzi huo ndio unaoibua fukuto ndani ya chama hicho na mmoja wa wajumbe wa kamati kuu amesema, “Kaka, hiyo kauli ya Wenje imekuja kuharibu, ameitoa kipindi kibaya, yaani sijui kamati kuu itakuwaje ila siyo poa.”

Alipoulizwa kwa nini siyo kauli nzuri, mjumbe huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema:”Unajua anaposema anafaa kumsaidia Mbowe, imeibua maswali, hivi ametumwa na Mbowe, je, Mbowe kwani atagombea tena, atashinda, je Lissu hataki kugombea tena ama.”

“Yaani hii kamati kuu itakuwa moto, kwa sababu kuna hilo suala la Wenje, kuna ile ya Lissu kusema atawania urais, zote ni kauli nzito ambazo tusipokuwa makini zitatuvuruga.”

Mjumbe huyo aliongeza kwa kusema hata kama suala la Lissu na Wenje halitakuwa sehemu ya ajenda lakini linaweza kuibuliwa na mtu yeyote na likajadiliwa kama ambavyo kamati kuu iliyopita liliibuliwa sakata la rushwa na kujadiliwa.

Mtazamo kama huo pia umeibuliwa na wachangia mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kauli hizo.

Hata hivyo, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Samwel John amesema uwezo wa mtu unapimwa kutokana na uzoefu alionao na hivyo Wenje ametimiza takwa la kikatiba kutia nia kwenye nafasi hiyo.

“Uzoefu wa Wenje katika Chadema unaonyesha amekomaa katika siasa na kimsingi ametimiza takwa la kikatiba na endapo  Lissu atagombea tena nafasi hiyo, wanakwenda kuleta hamasa kubwa kwa wapigakura na mwisho wa siku wataamua ni nani anayewafaa, pamoja na kwamba Lissu anakubalika zaidi yake,” amesema Samwel.

Hoja ya Lissu kuwania urais aliitoa Julai 26, 2024, akizungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini kutoka ughaibuni.

Katika maelezo yake, Lissu aliulizwa na waandishi kama anajiona anaweza kuwania urais uchaguzi ujao naye akawajibu akisema:

“Nia yangu ya kugombea mwaka 2025 ipo palepale, nitaitikia wito wa Watanzania na nitaitikia wito wa chama changu kama kitanitaka kufanya hivyo.”

Lissu ambaye mwaka 2020 aliwania urais na kushindwa na Dk John Magufuli wa CCM aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, alisema kwa sasa chama hicho kinaandaa wagombea wa nafasi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kinaibuka mshindi.

Mtazamo huo wa Lissu umeibua mijadala, wapo wanaoona kwamba Lissu anapaswa kumwachia mgombea mwingine kuwania nafasi hiyo kwa maelezo chama hicho huwa hakina uataribu wa kurudia wagombea urais.

Kundi jingine linadai Lissu alikosea kueleza hayo kwani utaratibu anaujua wa kutangaza nia ya nafasi ya urais. Pia wapo wanaosema licha ya Mbowe kuwahi kuwania nafasi hiyo mwaka 2005, wanamwona kama mtu sahihi kugombea tena hapo mwakani.

“Mambo ni mengi ndugu yangu, Lissu anajua utaratibu ila Lissu alikosea kwani kuna mwongozo kwa wanaoutaka urais kuwasilisha kusudio kwa maandishi kwa katibu mkuu naye atapeleka kamati kuu kwa hatua za kufanya utafiti na kuandaa taarifa ya kupeleka baraza kuu.”

Hayo ni maelezo ya mjumbe wa Baraza Kuu akielezea azima hiyo ya Lissu huku akisisitiza: “Unajua unaweza kuona kwa mbali Lissu anataka kuwekwa kando. Kwa sababu Wenje anataka nafasi yake, tetesi huku ni kwamba Mbowe atawania urais, je Lissu atakuwa nani sasa.”

Mwananchi limefanya jitihada za kumtafuta Lissu kuelezea kinachoendelea ndani ya chama hicho bila mafanikio.

Mwananchi limezungumza na wanachama kanda tatu za Chadema kupata mtazamo wao juu ya suala la Wenje kutaka nafasi ya Lissu.

Kanda hizo na mikoa yake kwenye mabano ni za Victoria, Serengeti na Magharibi.

Mwanachama kutoka Mwanza, Victor Kikachichi amempongeza kujitokeza kwake akidai kufanya hivyo ni kudhihirisha wazi chama hicho kinafuata misingi ya kidemokrasia.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Paulo Paulin amesema nafasi hiyo inastahili mtu shupavu na mkongwe, hivyo kutangaza kwake imeoneesha wazi ndani ya chama hicho kuna mkanganyiko kati yao.

“Wenje namfahamu tangu akiwa Mwalimu Butimba baadaye akawa mbunge wa wa Nyamagana, ndani ya Chama bado ni mchanga na hii imeonekana kwenye chama kuna mgawanyiko ila kwa makamu mwenyekiti nafasi hiyo haimfai na hastahili,” amesema.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Peter Francis ameshauri nafasi ya makamu mwenyekiti ishikwe na mtu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi na anayeweza kuhimili changamoto za chama.

“Katika mazingira ya kawaida inawezekana lakini kiuhalisia Wenje hana uwezo huo,” amesema.

Mwenyekiti Chadema Tabora, James Kabepele amesema alichokifanya Wenje kimetafsiri na kuwapa majibu waliodhani hakuna demokrasia ndani ya chama hicho.

“Kinachofanywa na Wenje kinatupa heshima kwa kiasi kikubwa na sio Wenje pekee ambaye anaweza kugombea, tunakaribisha wengine kugombea nafasi za uongozi kwenye chama chetu,” amesema.

Mkazi wa Tabora, Hamida Ally amesema ameonesha ukomavu wa kisiasa pamoja na ujasiri akidai nafasi anayoitaka kwa sasa inashikiliwa na mtu kikubwa mwenye umaarufu ndani na nje ya chama hicho.

Naye Silvester Lugembe, mkazi wa Simiyu amesema Wenje katumia vizuri nafasi ya katiba ya Chadema inayotoa nafasi kwa mwanachama yeyote kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi yeyote.

Hata hivyo, George Nkuba amedai alichokifanya siyo sahihi licha ya katiba kumruhusu alipaswa kusubiri kwanza kipindi cha kujenga chama kipite ndio ajitokeze kwa kuwa kwa sasa wanatakiwa viongozi wenye ushawishi kama ilivyo kwa Tundu Lussu.

Uamuzi wa Wenje pia umeungwa mkono na wanachama mkoani Mara wakidai anafaa kwa nafasi hiyo kwa kuwa anakijua chama vizuri na ana misimamo isiyoyumba.

“Ni mfia chama ana weza kufanya vizuri, misimamo yake ni kama mtangulizi wake kwa hiyo apewe nafasi naamini kwa kushirikiana na mweneyekiti watakifikisha chama sehemu sahihi,” amesema Fazel Janja, mkazi wa Geita

Naye, Eliya Magafu amesema umefika wakati wanachama wengine kupewa nafasi kungoza akidai changamoto ya kidemokrasia imetolewa na Wenje na anachotakiwa kufanyiwa ni kupewa nafasi na sio kubanwa.

Imeandikwa na Beldina Nyakeke (Mara), Timothy Lugoye (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Johnson James (Tabora) na Samwel Mwanga (Simiyu).

Related Posts