Morogoro. Umati mkubwa wa wananchi umejitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuhudhuria mkutano wa hadhara wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo umefanyika leo Jumanne, Agosti 6, 2024 ukihitimisha ziara ya Rais Samia mkoani humo aliyoianza Agosti 2, 2024.
Katika siku hizo amezindua, kuweka mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika mkutano wa leo, milango ya uwanja huo ilianza kufunguliwa saa moja asubuhi na ilipofika saa nane mchana uwanja huo ulijaa hadi wananchi wengine kujikuta wakibaki nje wakifuatilia kupitia runinga baada ya askari kufunga milango kwa ajili ya usalama.
Milango hiyo imefungwa baada ya Rais Samia kuingia uwanjani hapo akiongozana na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wengine akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima.
Miongoni mwa wananchi waliofika katika uwanja huo ni vijana ambao pamoja na kumsikiliza Rais Samia pia wamevutika na burudani zilizokuwa zikitokewa na wasanii mbalimbali akiwamo Diamond Platinum, Marioo, Shoro Mwamba, Mr Blue, Dulla Makabila na Khadija Kopa.
Burudani nyingine zilizovutia wananchi ni zile zilizotolewa na wasanii wa mkoani Morogoro akiwamo MC Hamza na kikundi cha vijana wa hamasa wa CCM.
Katika hotuba yake, pamoja na kuzungumzia masuala mbalimbali, Rais Samia amewashukuru wananchi wa Morogoro kwa kujitokeza kwa wingine kwenye mikutano aliyokuwa akiifanya tangu alipoanza ziara.
Moja ya tukio lililovuta hisia za wengi ni pale, msafara wa Rais Samia ulipokuwa ukitaka kuondoka, mkuu huyo wa nchi alipanda juu ya gari lake na kuanza kupiga picha ‘selfie’ na kwa kutumia simu yake ya mkononi na wananchi hao hali iliyoibua shangwe uwanjani hapo.