‘Watanzania kateni bima msisubiri hadi muugue’

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuwa na tabia ya kukata bima ya afya itakayowasaidia pale watakapougua.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, wakati akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo baada ya kupokea ugeni wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar leo Jumanne, Agosti 6, 2024.

“Ni muhimu tuanze kukata bima wakati afya zetu zikiwa sawa sawa ili ukiugua usianze kukimbizana. Ukiwa na bima yako inakusaidia kwa zaidi ya asilimia 90 ya magonjwa.

“Ukienda kukata bima wakati unaugua ile ada yake inakua juu. Mfano ukienda na saratani au ugonjwa wa moyo huwezi kulipia sawasawa na yule ambaye haugui kabisa,” amesema Profesa Janabi.

“Matibabu ni gharama na kusema Serikali iweze kuhudumia kila kitu ni gharama kubwa sana. Mfano huwezi kutoa 600,000 au milioni kwa mwezi kusafishwa figo. Lazima uwe na bima ya afya.”

Kilichomsukuma Profesa Janabi kuyasema hayo yote ni baada ya kuupokea ugeni huo ukiongozwa na Mwenyekiti Baraza la Wawakilishi la Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Sabiha Thani.

Thani na ujumbe wake wamefika kujionea huduma zinazotolewa hospitalini hapo sambamba na kujifunza kuhusu huduma za bima na afya kwa jumla ambayo kwa bara inazaidi ya miaka 12.

“Mwaka jana Wizara ya Afya Zanzibar ilipitisha sheria ya kuanzisha mfuko wa huduma za afya na huduma zimeanza kutolewa. Hivyo tukaona tuje kujifunza kwa kuwa wenzetu wameanza siku nyingi,” amesema Thani ambaye pia ni mwakilishi wa viti maalumu vya wanawake kundi la wazazi.

Amesema watakaporudi watakwenda kuishauri Serikali waboreshe yale maeneo muhimu ukizingatia marais wote wawili wameipa Wizara ya Afya kipaumbele.

“Hii ni ziara ya mafunzo ili Serikali yetu ikaboreshe pale kwenye mapengo iweze kuweka sawa na watu wapate huduma bora zaidi. Tukishaboresha kutakuwa hakuna sababu ya kwenda maeneo mengine,” amesema.

Akizungumza kuhusu ushauri huo mmoja ya Watanzania, Magreth Yusto mkazi wa Dar es Salaam amemuunga mkono Profesa Janabi huku akisema maradhi hayatabiriki ni muhimu kuwa tayari wakati wote.

“Ni kweli hata mimi naona ni sawa kwa sababu ugonjwa hautabiriki, sasa ukiwa na bima inasaidia. Namimi niombe elimu itolewe juu ya umuhimu wa bima,” amesema.

Hata hivyo, wakati Profesa Janabi anatoa rai hiyo, mwishoni mwa mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alitia saini muswada wa bima ya afya kwa wote kuwa sheria.

Muswada huo ulipitishwa na Bunge la Tanzania Novemba mwaka jana na baada ya kuwa sheria, kila mwananchi atakuwa na uhuru wa kuchagua skimu ya bima ya afya na kujiunga nayo ili kumwezesha kupata huduma za matibabu wakati wowote anapohitaji.

Sheria hiyo inaweka mfumo wa bima ya afya kwa wote na makundi mbalimbali kujumuishwa ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma na wa sekta binafsi, waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi na wananchi wasio na uwezo ambao sheria imeweka utaratibu wa kuwawezesha kuwa na bima ya afya.

Ingawa, matarajio ya Watanzania kuanza kwa huduma hiyo bado kwa kuwa hadi Julai mosi mwaka huu kwenye makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya katika mwaka 2024/25 yaliyowasilishwa bungeni, Sh6 bilioni zilitengwa kushughulikia baadhi ya mambo ikiwamo maandalizi ya bima ya afya kwa wote.

Related Posts