Mbeya. Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila unatarajiwa kuzikwa kesho katika Kijiji cha Godima wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.
Mwili wa Mwalabila aliyefariki dunia Agosti 4, 2024 kwa ajali ya gari mkoani Pwani, umesafirishwa leo kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ukitokea Kibaha mkoani Pwani ulikokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi.
Akizungumza na Mwananchi baada ya ndege kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, dada wa marehemu, Ericka Mwalabila amesema Sauli anazikwa kesho kijijini kwao Godima Wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya.
“Tutamzika kaka nyumbani kijijini Chunya kesho, kwa sasa tunaanza safari ya kuelekea huko,” amesema Ericka.
Miongoni mwa watu waliojitokeza kuupokea mwili wa Mwalabila ni pamoja na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga na Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka.
Akizungumzia msiba huo, Kasaka amesema wakazi wa Chunya hawatasahau mchango mkubwa wa miradi ya maendeleo aliyokuwa akiichangia Mwalabila enzi za uhai wake.
Amesema miongoni mwa miradi aliyoichangia ni wa maji katika Jimbo la Chunya na kuwezesha kupatikana saa 24.
“Binafsi nikiri kwamba Mwalabila ameisaidia sana Serikali na wananchi kwa ujumla, tumepoteza mtu wa thamani na pengo lake katu haliwezi kuzibwa,” amesema Kasaka.
Amesema mbali ya kuchangia miradi ya maendeleo, lakini pia alikuwa mlipa kodi mzuri na aliajiri vijana wengi. “Na alikuwa katika mchakato wa kuendeleza utoaji wa huduma ya maji, na mimi kama mbunge nitamuenzi kwa kusimamia huduma hiyo ipatikane saa 24 kwenye jimbo letu la Chunya,” amesema Kasaka.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni aliyefika uwanjani hapo kuungana na waombolezaji wengine waliofika kuupokea mwili huo, Adam Mwantende amesema taratibu za maziko zitaanza kesho saa 6:30 mchana.
Hata hivyo, amesema kabla ya kifo chake, Mwalabila alipanga mipango mingi ya maendeleo na Serikali ya Kijiji na aliahidi kuchangia kwenye miradi tofauti inayotekelezwa ukiwamo wa maji.
“Ndio maana unaona umati mkubwa hapa uwanjani kuja kumpokea ni kutokana na mchango aliokuwa nao kwao, hakuwa mtu wa kujikweza, sasa mipango tuliyokuwa tumepanga naye ndiyo imeishia hapa, ni pigo kubwa si kwa familia tu, bali kwa kijiji chote,” amesema Mwantende.
Diwani wa Sangambi, Junjulu Mhewa amesema wataendelea kuyaenzi mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.
“Kwetu ni pigo kubwa, marehemu alichangia miradi mingi ya maendeleo ikiwamo ya shule za msingi na sekondari, kwa sasa niseme tu naiombea familia moyo wa subira na wawe wavumilivu ni kipindi kigumu kwao na wamtangulize sana Mungu katika kila hatua,” amesema diwani huyo.
Sauli wakati wa uhai wake, alikuwa mwekezaji kwenye sekta ya usafirishaji akimiliki mabasi yaendayo mikoani pamoja na migodi ya dhahabu wilayani Chunya.
Keneth Jackson, mmoja wa wafanyakazi wake, akizungumza na Mwananchi Agosti 4, 2024 alisema Mwalabila alikuwa msimamizi mkuu wa migodi hiyo, hivyo kama wafanyakazi wanasubiri uamuzi wa familia.