Dar es Salaam. Wakati uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kitaifa ukiimarika ikilinganishwa na mwaka 2024, walimu kutoka shule za msingi 801 nchini Tanzania bado wanalazimika kufundisha wanafunzi zaidi ya 100 darasani jambo ambalo ni kinyume na viwango vilivyoweka serikalini.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Best Education ya mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), uwiano wa kitaifa mwaka 2024 ni mwalimu mmoja wanafunzi 51 ndani ya darasa ikilinganishwa na wanafunzi 57 waliokuwapo mwaka 2023.
Kufuatia hali hiyo, mdau wa elimu anashauri matumizi ya teknolojia au kutumia walimu waliopo mitaani kwa kulipwa fedha kidogo ili waweze kujitolea kufundisha katika shule zilizo na uhaba huku fedha za kijikimu zitoke katika bajeti za ndani za halmashauri au michango ya wazazi.
Wengine wanashauri kufanya uwekezaji zaidi katika kuajiri walimu ili kuendana na kasi ya ongezeko la wanafunzi.
Uchambuzi wa kina unaonyesha Mkoa wa Tabora huenda ukawa unahitaji kutupiwa jicho zaidi katika ajira za walimu zinazotangazwa ili kuweza kuunusuru kwani shule zake zinaongoza kwa kuchomoza katika kumi la kwanza zenye hali mbaya.
Ripoti hiyo ya elimu inatoka ikiwa ni siku chache tangu Serikali itangaze nafasi za kazi 11,015 katika sekta ya elimu, kufuatia ahadi kadhaa za kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha wa 2024/25 zilitolewa katika nyakati tofauti, baadhi zikiwa zimetolewa bungeni jijini Dodoma.
Akizungumza njia zinazoweza kutumika katika kukabiliana na hali hiyo, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDSM), Faraja Kristomus ameshauri walimu waliopo mitaani na hawana ajira watumiwe.
Walimu hao wanaweza kutumiwa kwa Serikali kupitia halmashauri kutenga baadhi ya fedha kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kutafuta walimu wa kujitolea katika shule zilizo na uhaba.
“Fedha hizo kidogo zitakuwa kwa ajili ya kujikimu ili kuwapunguzia ugumu wa maisha, badala ya kuendelea kubaki mtaani wakasaidia kuziba pengo linalosababishwa na uhaba wa walimu,” amesema Kristomus.
Amesema kwa halmashauri ambazo mapato yake ya ndani ni madogo na zimekuwa zikitegemea baadhi ya fedha za ruzuku ya Serikali kuu basi wazazi wanaweza kukubaliana kusaidia suala hilo kupitia vikao vya kamati za shule na bodi.
Amesema katika hilo mzazi anaweza kutoa alichonacho na si fedha pekee bali inaweza kuwa chakula, sehemu za kukaa.
Njia nyingine iliyopendekezwa ni matumizi ya teknolojia katika kufundisha kwa njia ya mtandao, mwalimu mmoja anaweza kuunganishwa na vifaa vya kisasa ili kufundisha watu wengi.
“Kwa Tanzania bado haijafika huko japokuwa ni kitu ambacho kimekuwa kikizungumzwa ila tunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kufanya uwekezaji,” amesema Kristomus.
Wakati shule zikiendelea kukabiliwa na uhaba wa walimu kwa vipindi tofauti, Ripoti ya Tume ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) 2023 iliyotolewa Mei 2024 inaonyesha kozi hiyo ndiyo inayoongoza kwa kutoa wahitimu wengi kuliko kozi yoyote.
Ripoti za miaka tofauti za TCU zinaonyesha kuwa mwaka 2023, walimu waliohitimu walikuwa 15,103, mwaka 2022 walikuwa 15,335 huku mwaka 2021 wakiwa 14,050.
Idadi ya wahitimu inaakisiwa na wingi wa wanafunzi wanaodahiliwa kwa vipindi tofauti huku mwaka 2023/24 kati ya wanafunzi 106,570 waliodahiliwa kuanza mwaka wa kwanza kwenye kozi 17 zilizoainishwa, waliochagua ualimu walikuwa 27,731.
Wakati udahili na watu wanaohitimu fani elimu ikionekana kuwa kubwa, hadi Desemba mwaka jana madarasa ya awali na msingi pekee yalikuwa yanahitaji walimu zaidi ya 116,885 ili kuweka uwiano wa walimu kwa wanafunzi sawa.
Kwa mujibu wa Kitabu cha hali ya Uchumi wa Taifa 2023 kilichotolewa na Wizara ya Fedha Juni mwaka huu, madarasa ya awali yalihitaji walimu 52,884 na shule za msingi zilihitaji walimu 64,001 ili kuwa na uwiano uliopangwa na Serikali pindi walimu hao watakapojumuishwa na waliokuwapo mashuleni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mkoa wa Tabora ndiyo unaoongoza kwa kuwa na uhitaji mkubwa wa walimu kwa kuwa uchambuzi unaonyesha shule sita kati ya kumi zenye hali mbaya nchini zinatoka mkoani humo.
Shule ya msingi Kalemela ambayo ndiyo kinara wa uwiano mkubwa wa wanafunzi kwa mwalimu iliyopo Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora inatajwa na ripoti hii kuwa na wanafunzi 1,164 shuleni hapo huku ikiwa na mwalimu mmoja pekee.
Shule hiyo inafuatiwa na ile ya kange ambayo pia inapatikana wilayani humo iliyo na wanafunzi 1,320 huku ikihudumiwa na walimu wanne wanaogawana wanafunzi hao jambo linalofanya kila mmoja kufundisha walimu 330.
Shule ya Malinyi iliyopo Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 311 huku Shule ya Barari iliyopo Manya mwalimu mmoja akibeba wanafunzi 306.
Shule ya Msingi Kadoke iliyopo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 297, Shule ya Msingi Mhande Geita, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 287, Shule ya Msingi Urasa iliyopo mkoani Tabora mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 277.
Shule nyingine katika orodha ya kumi zenye hali mbaya ni Cheyo A na Ngamila zilizopo Tabora ambako mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 255 na 247 mtawaliwa.
Shule iliyofunga orodha hiyo ni ule ya Mpasi iliyopo Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga mji ambayo mwalimu mmoja anabeba mzigo wa wanafunzi 234.8.
Tamisemi inataja Mkoa wa Katavi kuwa na uwiano mkubwa huku ikieleza mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 74 ndani ya darasa moja. Simiyu inafuata ambako mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70.
Tabora iko namba tatu na mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 69, Geita (mwalimu mmoja wanafunzi 67.8), Kigoma (mwalimu mmoja wanafunzi 64.5), Rukwa (mwalimu mmoja wanafunzi 64.4).
Mikoa mingine ni Shinyanga ambayo mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 63.8, Singida (mwalimu mmoja wanafunzi 60.6), Mara (mwalimu mmoja wanafunzi 60.4) na Dodoma mwalimu mmoja wanafunzi 56.7.
Ili kushughulikia masuala haya, Serikali inahitaji siyo tu kuongeza idadi ya walimu wapya, bali pia kuboresha programu za mafunzo kwa walimu. Kuongeza uwekezaji katika vyuo vya ualimu na kutoa mafunzo ya kitaalamu endelevu kwa walimu waliopo kazini kunaweza kusaidia kuziba pengo.
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, John Mwombeki amesema jitihada za Serikali za kuajiri walimu zaidi ni za kupongezwa lakini kiwango cha ajira kinapaswa kuongezeka ili kuendana na ongezeko la idadi ya wanafunzi.
“Bila kuboresha uwiano wa walimu kwa wanafunzi kwa kiwango kikubwa, ubora wa elimu uko hatarini,” amesema Mwombeki.
Mshauri wa Elimu, Sarah Kiwanga amesisitiza kuwa ipo haja ya kuwapo kwa mafunzo maalumu zaidi kwa walimu.
“Kwa mabadiliko mapya ya elimu yanayoendelea, siyo tu kuhusu idadi bali pia ubora wa walimu. Tunahitaji walimu wanaojua mbinu za kisasa za ufundishaji na wanaoweza kushughulikia madarasa makubwa kwa ufanisi,” amesema.