Vita ya ubingwa Ligi Kuu Bara karata ngumu

YANGA, Azam na Simba ndizo timu zinazopigania nafasi mbili za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Pia ndizo zinazowania ubingwa unaoshikiliwa na Yanga.

Katika kipindi hiki cha lala salama ya msimu wa 2023/24, ngoma imekuwa ngumu kutokana na wapinzani wanaokutana nao katika kusaka matokeo mazuri.

Tumeshuhudia Jumatano iliyopita Yanga ikitoka suluhu ugenini dhidi ya JKT Tanzania, katika mchezo ambao umeacha maswali mengi kutokana na ubora wa uwanja walioutumia wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Ukiangalia mechi tano za mwisho kwa timu hizo kucheza, hakuna iliyoshinda zote, Yanga na Simba zimekuwa na matokeo sawa kila mmoja akishinda tatu, sare moja na kupoteza moja, wakati Azam ikizipiga bao kidogo kwa kushinda tatu na sare mbili, haijapoteza.

Suluhu ya Yanga dhidi ya JKT Tanzania, imewashtua vigogo wote hao ambao kila mmoja ameanza kuweka tahadhari katika karata zake ngumu na muhimu kuelekea michezo ya mwisho wa msimu, huku  wenyewe kwa wenyewe wakiombeana njaa.

Yanga wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 59, wamebakiwa na mechi saba zenye pointi 21 kumaliza msimu, wanahitaji alama 15 pekee kuanzia sasa ili kuteteta ubingwa wao kwani watafikisha 74 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine. Watahitaji kushinda mechi 5 tu.

Azam ina mechi sita zilizobaki ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 54, ikishinda mechi zote, itamaliza ligi na pointi 72. Hapo dua zao ni kuomba Yanga iteleze.  Ukija kwa Simba, wanashika nafasi ya tatu wakiwa na mechi tisa mkononi kumaliza msimu, pointi zao kwa sasa ni 46, wakishinda mechi zote zilizobaki watafikisha 73.

Katika mechi zao saba zilizobaki, Yanga itacheza nne nyumbani dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar, Tabora United na Tanzania Prisons, huku tatu za ugenini ni dhidi ya Mashujaa, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji.

Tukianza na mchezo wa Jumamosi hii dhidi ya Coastal Union, rekodi zinaonyesha timu hizi zilipokutana katika mzunguko wa kwanza, Yanga ikiwa ugenini Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ilishinda bao 1-0.

Yanga imekuwa na rekodi nzuri mbele ya Coastal ikiwa uwanja wa nyumbani kwani katika mechi tatu za mwisho, imeshinda zote kwa matokeo ya mabao 3-0 kila mechi, hivyo kuna asilimia kubwa kuendeleza ubabe wao.

Coastal ina mtihani mzito mbele ya Yanga kwani rekodi yake ya mechi tatu za ugenini za hivi karibuni sio nzuri kwani imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja.

Kwa sasa timu hiyo inapambana kumaliza nafasi ya nne, hivyo licha ya kuwa na rekodi mbovu, bila shaka mchezo utakuwa mgumu kwa kila mmoja kuhitaji kufikia malengo yake.

Baada ya Coastal, Yanga itasafiri hadi Lake Tanganyika mkoani Kigoma kupambana na Mashujaa, hii itakuwa Mei 5, 2024. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda mabao 2-1.

Mashujaa huu ni msimu wao wa kwanza Ligi Kuu, hivyo inakwenda kukutana na Yanga kwa mara ya pili baada ya mzunguko wa kwanza kupoteza ugenini.

Ukiangalia rekodi ya Mashujaa ikiwa nyumbani, katika mechi tatu za mwisho imeshinda mbili na kupoteza moja, hivyo inaweza kutoa upinzani kwa Yanga ukizingatia kwamba, katika uwanja wao wanakuwa wagumu sana.

Mbali na hilo, pia Mashujaa ipo kwenye hatari ya kushuka daraja, ni wazi itapambana kuhakikisha haipoteza mchezo huu. Kazi ipo hapo.

Karata ya tatu ya Yanga ni Mei 8, 2024 katika uwanja wa nyumbani ikicheza dhidi ya Kagera Sugar ambapo mzunguko wa kwanza, walitoka suluhu.

Yanga inapocheza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, imekuwa na matokeo mazuri, mechi tatu za mwisho imeshinda mbili kwa matokeo ya 5-0 na 3-0, huku ikitoka sare moja ya 3-3.

Kagera wenyewe wakiwa ugenini katika mechi zao tatu za hivi karibuni, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. Ukiangalia msimamo, Kagera ipo katikati, mechi hii inaweza isiwe ngumu sana kwa Yanga.

Mei 13, 2024, Yanga itatakiwa kuwa Uwanja wa Manungu pale Morogoro. Mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda nyumbani mabao 4-1, lakini pia ina rekodi nzuri ya kushinda mechi tatu mfululizo ilipocheza ugenini dhidi ya Mtibwa.

Mtibwa msimu huu hali ni tete, kwa sasa inaburuza mkia, katika mechi zake nane zilizosalia, inapaswa kupambana kweli kwani pointi 17 ilizonazo ikizembea itakwenda na maji. Mechi zao tatu za hivi karibuni nyumbani, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja, siyo matokeo mazuri kwao.

Ikitoka Morogoro, Mei 22, 2024 Yanga itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kucheza dhidi ya wenyeji wao Dodoma Jiji. Tulishuhudia mchezo wa kwanza, Yanga ilipata ushindi kiduchu wa bao 1-0

Licha ya hivyo, lakini Yanga inapocheza ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, matokeo si mabaya kwake kwani mechi tatu za mwisho imeshinda mbili na suluhu moja, zote hizo imeondoka na clean sheet. Dodoma Jiji mechi zao tatu za mwisho ilizocheza nyumbani hivi karibuni imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja.

Yanga itamalizia mechi zake mbili za mwisho nyumbani, itaanza dhidi ya Tabora United, Mei 25, 2024, baada ya ile ya kwanza ugenini kushinda 1-0.

Tabora United imepanda daraja msimu huu, ukiangalia rekodi ya mechi tatu za mwisho ilizocheza ugenini, imepoteza zote, hivyo itakuwa na kazi kubwa mbele ya Yanga, kwa sasa timu hiyo nayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja. Mei 28, 2024 ambapo ligi itafikia tamati, Yanga itacheza dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo wa kwanza matokeo yalikuwa 2-1. Timu hizi zinapokutana mechi huwa ngumu.

Yanga katika mechi tatu za mwisho nyumbani ilipocheza dhidi ya Tanzania Prisons, imeshinda moja, sare mbili. Tanzania Prisons rekodi yao ya mechi tatu za mwisho hivi karibuni ilipocheza ugenini, imepoteza moja, sare mbili, haijashinda.

Safari yao ya mechi tisa itaanzia ugenini Aprili 30, 2024 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo ambayo mzunguko wa kwanza matokeo yalikuwa 1-1.

Namungo katika mechi tatu za mwisho nyumbani ilipocheza dhidi ya Simba, haijashinda zaidi ya kuambulia sare mbili na kupoteza moja. Rekodi yao katika mechi tatu za hivi karibuni ikiwa nyumbani dhidi ya wapinzani wengine imeshinda moja na kupoteza mbili.

Mei 3, 2024, Simba itaikaribisha Mtibwa Sugar, mzunguko wa kwanza ugenini Simba ilishinda 4-2, huku rekodi yao ya nyumbani dhidi ya Mtibwa, ikiwa ni nzuri kutokana na kushinda zote, matokeo yakiwa hivi; 5-0, 2-0 na 5-0.

Mtibwa Sugar hivi karibuni katika mechi zake za ugenini imeshinda moja, sare mbili, haijapoteza. Wenyeji hao wa Turiani mkoani Morogoro, kumbuka pia wana kibarua dhidi ya Yanga na Azam, hivyo katika kujinasua na janga la kushuka daraja, wanakutana na vigogo wote. Mei 6, 2024, Simba itakuwa nyumbani mbele ya kibonde wake wa mzunguko wa kwanza, Tabora United ambayo iliichapa mabao 4-0.

Tabora United rekodi ya mechi tatu za ugenini ilizocheza  karibuni haijashinda hata moja, imepoteza zote. Kumbuka Tabora iliyopo katika hatari ya kushuka daraja inacheza dhidi ya Yanga na Simba katika mechi sita zilizobaki.

Mei 9, 2024 inaweza kuwa mechi ya kuamua kati ya Azam na Simba, hiyo ni kutokana na namna timu hizo zilivyo kwenye msimamo. Mechi ya kwanza Simba ikiwa mwenyeji, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1. Mechi sita za mwisho walizokutana, sare ni nne, huku kila mmoja akishinda mechi moja.

Mei 12, 2024, Simba itaenda Kaitaba kucheza dhidi ya Kagera Sugar baada ya mzunguko wa kwanza nyumbani Simba kushinda 3-0. Simba katika mechi tatu za mwisho ugenini kucheza na Kagera Sugar, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. Wakati rekodi ya Kagera Sugar nyumbani hivi karibuni katika mechi tatu haijashinda wala kupoteza, imetoka sare zote.

Dodoma Jiji wana kazi mbele ya Simba katika mchezo utakaopigwa Mei 16, 2024 pale Jamhuri, Dodoma ambapo Simba mechi tatu za mwisho ikicheza ugenini dhidi ya mwenyeji wake huyo imeshinda zote.

Ukiangalia rekodi ya Dodoma Jiji ilipocheza nyumbani katika mechi tatu karibuni, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. Mei 21, 2024, itakuwa ni zamu ya Simba kuikaribisha Geita Gold baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza ugenini Simba kushinda 1-0, huku rekodi ya Simba nyumbani mbele ya Geita Gold ikiwa nzuri kutokana na kushinda mara mbili walizokutana. Geita Gold mechi za ugenini hivi karibuni imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja, bado inajitafuta ikiwa katika timu nafasi tano za chini. Mei 25, 2024 Simba itaikaribisha KMC, mzunguko wa kwanza matokeo yalikuwa sare ya 2-2, huku mechi zao tatu za mwisho kukutana, Simba ikishinda mbili na sare moja.

Rekodi ya KMC katika mechi tatu za mwisho ugenini, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. KMC kwa sasa nayo inapambana kumaliza nne bora.

Mwisho kabisa Mei 28, 2024, Simba itacheza nyumbani dhidi ya JKT Tanzania, mechi ya kwanza Simba ilishinda 1-0. Rekodi walipokutana mechi tatu za mwisho Simba imeshinda mbili na kupoteza moja. JKT Tanzania rekodi yao ya kucheza ugenini mechi tatu za mwisho imepoteza moja na kuambulia sare mbili, haijashinda. Kwa sasa timu hiyo inapambana isishuke daraja baada ya kupanda msimu huu. Katika mechi tisa zilizobaki Simba itacheza sita jijini Dar es Salaam, tatu nje ya mkoa huo. Zote hizo zitakuwa ndani ya siku 29 kukiwa na wastani wa mechi moja kila baada ya siku tatu.

Mei 6, 2024, Azam itakuwa Manungu – Morogoro kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar. Azam mzunguko wa kwanza walishinda 5-0, huku rekodi zikionyesha Azam imeshinda mechi mbili ugenini dhidi ya Mtibwa na kupoteza moja.

Mtibwa mechi tatu za mwisho nyumbani imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. Mei 9, 2024, ni mchezo unaosubiriwa na wengi kwani unaweza kutoa hatma ya timu mbili zinazokwenda kukutana, Azam dhidi ya Simba, pia Yanga itauangalia kwa karibu kutokana na hesabu zilivyo. Mara ya mwisho wawili hao walitoka 1-1. Rekodi za mechi sita zilizopita ambazo Azam alikuwa mwenyeji zipo hivi; Azam 1-1 Simba, Azam 1-0 Simba, Azam 1-1 Simba, Azam 1-2 Simba, Azam 1-1 Simba, Azam 2-2 Simba.

Mei 12, 2024, Azam itakuwa mgeni wa KMC, mzunguko wa kwanza, Azam ilikuwa mwenyeji ikashinda 5-0, safari hii itakuwa mgeni, lakini mchezo utapigwa palepale Azam Complex.

Matokeo ya Azam mbele ya KMC inapokuwa ugenini katika mechi tano za mwisho, siyo mazuri kwani imepoteza tatu, imeshinda moja na sare moja.

Ukija kuangalia KMC matokeo yake ya mwisho mechi tatu za nyumbani, imeshinda moja na sare mbili, hivyo haina muendelezo mzuri. Wenyeji JKT Tanzania, wataikaribisha Azam katika mchezo utakaopigwa Mei 20, 2024, ukipangwa kuchezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Mzunguko wa kwanza, Azam nyumbani ilishinda 2-1.

Azam katika mechi tatu za mwisho ilizocheza ugenini dhidi ya JKT Tanzania, imeshinda zote kwa bao 1-0, hivyo rekodi inawabeba, lakini JKT Tanzania katika mechi zao tatu za mwisho hivi karibuni ikiwa nyumbani, haijapoteza wala kushinda, zote imetoka sare.

Baada ya kutoka ugenini, Mei 25, 2024 Azam itakuwa nyumbani kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Kagera Sugar, matokeo ya mzunguko wa kwanza Azam ugenini ilishinda 4-0. Timu hizo katika mechi tatu za mwisho zilipokutana nyumbani kwa Azam, wenyeji walishinda mbili na sare moja. Rekodi ya Kagera Sugar mechi zao tatu za hivi karibuni wakiwa ugenini, wameshinda moja, sare moja na kupoteza moja.

Funga dimba kwa Azam msimu huu itakuwa Mei 28, 2024 ugenini dhidi ya Geita Gold, ngoma itapigwa Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita. Mzunguko wa kwanza Azam nyumbani ilishinda 2-1.

Mechi tatu za mwisho walizokutana wawili hawa Azam akiwa mgeni, zinaonyesha kuibeba Geita kwani imeshinda mbili na sare moja, Azam itakwenda Nyankumbu ikifahamu kwamba sio sehemu salama kwao. Geita Gold rekodi ya mechi tatu za karibuni ikiwa nyumbani zinaonyesha kwamba haijashinda hata moja, hivyo haina matokeo mazuri.

Katika mechi zilizosalia, zipo 17 zinazoweza kuamua hatma ya vigogo hao kutokana na timu zaidi ya moja kucheza dhidi yao wote. Mtibwa Sugar ni timu ambayo imebakisha mechi tatu dhidi ya vigogo hao watatu kama ilivyo kwa Kagera Sugar, huku zingine zikiwa ni mechi mbilimbili. Mechi hizo ni Yanga vs Kagera Sugar, Kagera Sugar vs Simba, Azam vs Kagera Sugar, Mtibwa Sugar vs Yanga, Simba vs Mtibwa Sugar, Mtibwa Sugar vs Azam, Simba vs JKT Tanzania, JKT Tanzania vs Azam, Dodoma Jiji vs Yanga, Dodoma Jiji vs Simba, Yanga vs Tabora United, Simba vs Tabora United, Azam vs Simba, Simba vs Geita Gold, Geita Gold vs Azam, Simba vs KMC na KMC vs Azam.

Ukiachana na takwimu zilizoanishwa hapo zikionyesha ugumu wanaokwenda kukutana nao timu ndani ya ligi kuelekea mwisho wa msimu, kuna mambo mengine manne yametajwa kuchangia jambo hilo.

Katika kipindi hiki tulichopo sasa, mvua zimekuwa zikinyesha kwa kiwango kikubwa, huku viwanja vingi vikiwa si rafiki inapotokea hali hiyo. Imeshuhudiwa mchezo wa JKT Tanzania dhidi ya Yanga ulioahirishwa kutokana na mvua iliyonyesha na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kujaa maji, ulichezwa siku inayofuatia mechi ikaisha kwa suluhu.

Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alionyesha kutofurahishwa na uamuzi wa kuutumia uwanja huo wakati awali ulionekana haupo katika hali nzuri.

“Kupata alama moja kwenye uwanja kama ule ni kitu kizuri tu kwangu, unawezaje kushinda kwenye uwanja kama ule? Sijui ni maamuzi gani haya yamefanyika,” alilalamika Gamondi.

“Huwezi kucheza mpira wa kuvutia kwenye uwanja kama ule, tunaona soka la Tanzania linapiga hatua ni jambo zuri, lakini uwanja kama huu unakwenda kuiweka wapi heshima hiyo, kwanini ilazimishwe mechi kuchezwa pale ingekuwa sawa hata kusogeza mechi mbele au kuhamishwa kupelekwa uwanja mwingine.”

Viwanja ambavyo mara nyingi vimekuwa changamoto kipindi cha mvua ni Meja Jenerali Isamuhyo (Dar), CCM Kirumba (Mwanza), Manungu (Morogoro), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Sokoine (Mbeya) na Nyankumbu (Geita). Miongoni mwa viwanja hivyo, Yanga na Azam watalazimika kwenda kucheza huko katika mechi zao zilizosalia.

Yanga na Azam watalazimika kwenda Manungu kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini pia Azam ana mechi dhidi ya JKT Tanzania inayotumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, kisha watamaliza ligi kwa kukabiliana na Geita Gold pale Nyankumbu.

Simba yenyewe haina mechi katika viwanja hivyo, lakini itacheza Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma watakapoenda kupambana na Dodoma Jiji, uwanja ambao unawapa shida vigogo kuondoka na ushindi, pia Yanga itakwenda kucheza.

Si Yanga, Azam wala Simba, bali ni wachezaji wa timu zote kwa sasa ni kama wapo sokoni katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu.

Hilo linawafanya kupambana sana ndani ya uwanja ili tu kuzivutia timu kuwapa mikataba kwa ajili ya msimu ujao.

Kocha wa Tanzania Prisons, Ahmed Ally, amefichua jambo hilo hivi karibuni baada ya kusema: “Ligi inaelekea ukingoni wachezaji wanajituma na kufanya mechi zote kuwa ngumu, kila mmoja anatafuta soko kwa ajili ya msimu ujao.”

Hakuna timu inayotaka kumaliza sehemu mbaya, hapa inaifanya ligi kuwa ngumu zaidi kwani wapo wanaowania ubingwa na nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Zingine zinapambana kuepuka kushuka daraja, pia zipo zinazohitaji kuweka heshima.

Katika mechi saba Yanga ilizobaki nazo, itacheza dhidi ya Coastal Union inayowania kumaliza nafasi ya nne, pia itapambana na Mtibwa Sugar iliyopo mkiani kwa sasa ikipambana isishuke daraja.

Pia Yanga itapambana na Mashujaa ambayo nayo haipo salama, inapambana isishuke daraja.

Azam inayopambana katika mechi sita zilizosalia kuwa sehemu nzuri zaidi ikiwemo kubeba ubingwa, itatakiwa kutofanya makosa mbele ya Mtibwa Sugar, Geita Gold na JKT Tanzania ambapo mechi hizo zote itacheza viwanja korofi.

Simba wamebakiwa na mechi tisa, watacheza mechi tatu nje ya Dar dhidi ya Namungo, Dodoma Jiji na Kagera Sugar, pia wana kibarua mbele ya Azam.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, alisema katika mechi zilizosalia, watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri, huku wakiacha hesabu za mwisho ndiyo ziamue.

“Nafikiri ubingwa umekuwa mgumu, lakini cha muhimu ni kuendelea kupambana katika mechi zilizobaki kuweza kushinda halafu mwisho wa ligi tujue hesabu zipo vipi,” alisema Matola.

Gamondi naye amezungumzia ugumu uliopo katika mechi zilizobaki akisema hivi sasa timu zinapambana kila moja kuhakikisha zinamaliza katika nafasi nzuri.

Kocha huyo raia wa Argentina amekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba, kwake hilo analifanyia kazi kuhakikisha halitibui mipango yake, lakini huwa hafurahii kukutana na timu zinazojilinda zaidi.

“Kipindi hiki ligi inakuwa ngumu kwa sababu kila mmoja anataka kupata matokeo ya kuwa sehemu nzuri na kufikia malengo,” alisema Gamondi na kuongeza.

“Falsafa yangu ni kucheza soka la burudani na kupata matokeo mazuri, siyo kujilinda zaidi.

“Hivyo basi, siku zote unapocheza na timu inayojilinda haikupi nafasi nyingi za kufunga, lakini huwa tunapambana kwa uwezo wetu kuhakikisha tunauweka mpira kwenye nyavu.”

Katika kutoa motisha ili wachezaji wapambane kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu, viongozi wa timu wamekuwa wakitoa ahadi mbalimbali za fedha.

Hiyo inawafanya wachezaji kujituma zaidi pindi wanapoingia uwanjani kupambania pointi tatu kitu kinachozidisha ugumu wa ligi.

Katika mchezo wa juzi kati ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga uliomalizika kwa suluhu, wenyeji waliahidiwa kiasi cha Sh60 milioni kama wangeshinda, lakini suluhu imewafanya waambulie Sh30 milioni.

Motisha kama hizo mara nyingi huwepo katika mechi ngumu au kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa ligi timu zinapopambana kufikia malengo yao.

Ukiangalia JKT Tanzania wakati inakwenda kucheza dhidi ya Yanga, ilikuwa nafasi ya pili kutoka chini, ahadi waliyopewa imewafanya wachezaji kujituma kadiri wawezavyo, wakaambulia pointi moja iliyowapandisha hadi nafasi ya nne kutoka chini. Safari bado inaendelea.

Related Posts