MAAFISA UGANI WANAHITAJI MAFUNZO YA MARA KWA MARA KUHUSU TEKNOLOJIA NA MBINU ZA KISASA ZA KILIMO ZINAZOZALISHWA.

 

Na: Amina Hezron – Dodoma.

Imeshauriwa kuwa uwekezaji katika sekta ya kilimo ujikite zaidi katika kuangalia namna ya kuboresha mbinu mbalimbali za ugani na teknolojia za kisasa ili kuwasaidia maafisa ugani kufikisha taarifa bora na za kisasa kwa wakulima vizuri na kuinua tija.

Ushauri huoumetolewa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Catherine Msuya wakati wa kongamano la kimataifa lililolenga kuangalia mchango wa uwekezaji katika sekta ya kilimo ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo china na Marekani lililofanyika Jijini Dodoma kwenye maonesho ya Kitaifa ya wakulima nanenane.

“Maafisa ugani bado wamekuwa wakiendelea kutumika njia za zamani japokuwa zipo jitihada zinazoendelea za kufanya wanafunzi ambao wapo vyuoni kujifunza mbinu za kisasa, lakini vipi wale wagani ambao tayari kundi kubwa lipo kule likifanya kazi wanajifunza wapi,hivyo ipo haja ya kuwekeza katika kuwapa elimu na maarifa ya hayo mapya na ya kisasa yanayokuja” alibainisha Prof. Catherine.

Aliongeza “Unakuta Mgani amemshauri mkulima kutumia mbegu flani ambayo ilikuwa ikitumika siku zote na ikifanya vizuri lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ile mbegu haifanyi vizuri mkulima mfugaji au mvuvi anakuwa anasahau kwamba kuna mabadiliko ya tabia nchi hivyo lawama zinakuwa kwa afisa ugani”.

Awali akifungua kongamano hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kilimo ili kuhakikisha tija inaongezeka hivyo amewataka wakulima kutumia maarifa mbalimbali wanayopewa ili waweze kufikia lengo lao na la Taifa.

“Natoa wito kwa sisi viongozi na watumishi wenye dhamana kusaidia wakulima tuendelee kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili wakulima wetu wanapolima wahakikishe wanapata nafasi ya kuuza mazao yao kwa njia ambayo haina vikwazo ili wabadili mazao yao kuwa fedha hiyo ndiyo njia nzuri ya kuongeza kipato na kuondoa umaskini”, alisema Prof Kitila.

Aidha ametoa wito kwa wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza katika kilimo hususani kwenye viwanda kwasababu lengo ni kuongeza thamani mazao ya kilimo Mifugo, Uvuvi, Misitu na Madini ili kuweza kusafilisha bidhaa zilizoongezeka thamani na kupata fedha nyingi zaidi.

Aidha kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amesema kuwa Kongamano ni nyezo muhimu kwasababu linawafungua watu macho kujua yale ambayo hawakuwa wakiyajua na linasaidia kutoa nafasi ya kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa changamoto kwa pamoja kupitia majadiliano.

“Kuna mengi ambayo tukienda kukaa tukayatafakari na mengine kutengenezewa mpango kabisa mimi naamini yatawaongezea sana maarifa mapya kwa Wananchi wetu kutoka hapo walipo na kupiga hatua moja mbele”, alisema mhe Pinda.

Maafisa Ugani hao kupitia chama chao cha maafisa ugani Tanzania (TSAEE) wanakutaka kwenye maonesho hayo ya Kitaifa ya nanenanen Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali mpya na za kisasa zilizopo ili kuwajengea maarifa mapya ambayo yatawasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali za wakulima kwenye maeneo wanayotoka nchi nzima.

Related Posts