TIMU ya Taifa ya Kriketi U19, juzi imetinga nusu fainali ya mashindano ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia baada ya ushindi mzito wa mikimbio 353 dhidi ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Dar Gymkhana.
Tanzania ilimaliza hatua za makundi kwa kushinda mechi zote tatu ukiwemo wa mikimbio 162 dhidi ya Ghana Jumapili iliyopita.
Ni kipigo cha ‘mwana ukome’ walichokitoa Tanzania kwa Msumbiji ambayo ilifungwa na Ghana kabla na kuonekana ni wachanga kwenye michuano hiyo.
Wakiongozwa na Kassim Kiseto aliyetengeneza mikimbio 133 peke yake, Tanzania ilipata kura ya kuanza na kutengeneza mikimbio 379 huku ikipoteza wiketi nne na kutumia mizunguko yote 50.
Kukuru kakara za vijana wa Msumbiji U19 ziliwafikisha kwenye mikimbio 26 tu baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 12 kati ya 50 na hivyo Tanzania kuondoka wababe kwa jumla ya mikimbio 353.
Pamoja na Kiseto aliyetengeneza zaidi ya mikimbio 133, Mohamed Simba Mbaki pia aling’ara kwa kuipaa Tanzania mikimbio 77, wakati Sayan Jobanputra pia alifanya vizuri kwa kutengeneza mikimbio 62.
Nigeria iliwaadhibu majirani zao Ghana kwa jumla ya mikimbio 119 katika mchezo wa pili, juzi Jumanne kwenye Uwanja wa UDSM jijini.
Nigeria U19 waliopata kura ya kuanza, walitengeneza mikimbio 183 baada ya wote kutolewa huku wakiwa wametumia mizunguko 40 kati ya 50 iliyowekwa.
Jitihada za Ghana U19 ziligota kwenye mikimbio 64 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 27 kati ya 50.
Femi Oresenwo aliyetengeneza mikimbio 49 na Ali Rahmon aliyeweka mkimbio 44 ndiyo walioibeba Nigeria U19 dhidi ya Ghana.
Tanzania ilianza vyema mbio za kufuzu fainali hizo kwa Divisheni ya pili baada kuishinda Nigera kwa wiketi sita katika Uwanja wa Dar Gymkhana wikiendi iliyopita
Kwa kutinga nusu fainali, Tanzania ina zaidi ya asilimia 70 ya kucheza fainali za kombe la dunia kwani ni timu tatu kati ya nane zilizo katika nusu fainali ndizo zitakata tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia na kupanda daraja kuwa divisheni ya kwanza.
Uhakika wa Msumbiji kuyaaga mashindano ulipatikana baada ya kufungwa na Tanzania, kwani walipoteza kwa Ghana kwa wiketi tano katika mchezo wa ufunguzi.