Njombe. Wakazi zaidi ya 5,000 wa vijiji vinne vya kata za Makonde na Mawengi wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe, wameondokana na changamoto ya kutegemea usafiri wa majini baada ya kujengewa barabara tangu uhuru upatikane nchini.
Barabara hiyo itawasaidia wakazi hao kupata huduma muhimu kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya na mikoa jirani.
Awali, wakazi hao walitegemea usafiri wa majini kwa huduma za kitabibu na nyinginezo, hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata matibabu kwa haraka.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara baada ya kuzindua barabara hiyo leo Jumatano Agosti 7, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva amesema Kata ya Makonde ina vijiji vitatu ambavyo ni Ndowa, Kimata na Makonde.
Amesema vyote hivyo vilikuwa vikitegemea usafiri wa meli ya MV Njombe na mitumbwi. Hata hivyo, sasa wana barabara itakayorahisisha mawasiliano.
Mwanziva amesema tangu alipofika wilayani humo mwaka mmoja uliopita, kilio cha kwanza kukipokea kutoka kwa wakazi wa eneo hilo ni barabara.
“Sasa barabara ndiyo hii, tutapita kwa gari, hii ni hatua kubwa tumepiga ya maendeleo, kwa sababu barabara ni kiini cha uchumi. Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Serikali itoe Sh1.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii, pia nawapongeza viongozi wa eneo hili akiwamo mbunge Joseph Kamonga, kwa juhudi za kuhakikisha barabara hii inapatikana,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Mbunge wa Ludewa, Kamonga amesema ahadi yake wakati wa kampeni ilikuwa kuleta maendeleo na alipoelezwa kuhusu uhitaji wa barabara hiyo, aliona ni muhimu kuandika barua maalumu bungeni ili kupata fedha za ujenzi wake.
Amewashukuru wote walioshiriki katika kufanikisha ujenzi huo licha ya kuwapo changamoto.
Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Ludewa, Butene Jilala amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 28 bado inaendelea kujengwa na itagharimu Sh1.4 bilioni mpaka kukamilika kwake.
“Shughuli zinazofanyika sasa ni pamoja na kukata na kulipua milima ili kufungua njia na ujenzi wa zege, makaravati na uchongaji wa barabara,” amesema Jilala.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Njombe, Daniel Okoka amesema alipotembelea kijiji hicho Desemba, 2023, changamoto kubwa zilizotajwa na wananchi ilikuwa ni barabara, umeme na mawasiliano ya simu.
“Sasa barabara ndiyo hii na tayari magari yameshaanza kupita, namshukuru mbunge na Serikali kwa jumla kwa kusikia kilio cha wananchi hawa,” amesema Okoka.
Diwani wa Makonde, Chrispin Mwakasungura amesema tangu alipoingia kwenye udiwani mwaka 2005, ajenda yake ya kwanza ilikuwa ni ujenzi wa barabara na ya pili ni ujenzi wa shule ya sekondari kijijini hapo.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge Kamonga kwa ushirikiano na upendo wao katika kufanikisha malengo haya,” amesema diwani huyo.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Makonde, Bernard Haule amewaonya makandarasi kuwa waaminifu kwa kuwalipa vijana wanaofanya kazi kwa wakati ili nao waweze kunufaika na miradi hiyo.