Pazia la Ligi ya Championship msimu huu linafungwa kesho Jumapili huku utamu utakuwa jijini Arusha wakati Pamba itakaposaka nafasi ya kuzika mzimu ulioitesa kwa zaidi ya miaka 20 kutopanda Ligi Kuu.
Ligi hiyo iliyoanza Septemba 9 ikishirikisha timu 16 inafika tamati huku Ken Gold ikiwa imepanda Ligi Kuu na pointi 67 ikiwa na mechi moja, ilhali Ruvu Shooting ikishuka First League na itakamilisha kwa kuvaana na Green Warriors.
Macho na masikio ya mashabiki wa soka yatakuwa Arusha wakisikilizia Pamba Jiji iliyoshuka daraja 2000 ikipambana kurudi Ligi Kuu kwani ina pointi 64 ikiwa nafasi ya pili itakapovaana na Mbuni ambao haina cha kupoteza, lakini ikiiombea njaa Mbeya Kwanza inayovaana na Transit Camp.
Msimu huu Championship ilikuwa na utamu kutokana na ushindani ukilinganisha na msimu uliopita kwa JKT Tanzania waliopanda kabla ya mechi mbili. Ken Gold waliopanda walisubiri hadi mchezo wa 29 kwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya FGA Talents.
Kesho itakuwa uwanjani kutafuta hata pointi moja ili kufikisha 68 ambazo zitawaweka kileleni na kuwa bingwa wa Championship msimu huu.
Kama haitoshi mbali na Ruvu Shooting haijaeleweka timu nyingine itakayoshuka kati ya Copco wenye pointi 22 na Pan Africans wenye alama 19.
Mechi za leo ndizo zitaamua nani aungane na Ruvu Shooting kucheza First League msimu ujao, ambapo Copco itakuwa ugenini dhidi ya TMA, huku Pan ikiikaribisha Stand United.
Ken Gold iliyojulikana kama Gipco FC iliyokuwa mkoani Geita, imeshiriki Championship misimu mitatu mfululizo kabla ya kupanda mwaka huu. Timu hiyo haikuwa na matokeo mabaya misimu hiyo ikimaliza nafasi tano za juu. Licha ya kusota hadi mechi 29 msimu huu imeufanya Mkoa wa Mbeya kuwa na timu mbili za Ligi Kuu msimu ujao ikiungana na Tanzania Prisons.
Kazi ipo pia katika nafasi nne za juu ambapo hadi sasa Biashara United iliyo katika vita ya kupanda ilijichanganya na kuachwa na Ken Gold, Mbeya Kwanza na Pamba Jiji.
Kupoteza mechi dhidi ya Pan Africans 2-1 kulifanya mbio kuishia hapo na kusubiri muujiza kupitia play off (mchujo).
Iwapo Pamba Jiji itapoteza dhidi ya Mbuni itaungana na Biashara United kucheza play off na mshindi atakutana na timu ya Ligi Kuu kuwania kupanda.
Pia iwapo Mbeya Kwanza itapoteza au kupata sare dhidi ya Transit Camp, itakutana na Biashara katika play off kuwania kuwania kurejea Ligi Kuu.
Mtihani mwingine utakuwa timu zinazowania kubaki Championship ukihusisha timu tano FGA Talents waliopo nafasi ya 10 kwa alama 31 sawa na Stand United, Green Warriors (28), Transit Camp (27) na Copco wa 14 alama 22.
Straika wa Ken Gold, Wiliam Edgar anakuwa mchezaji wa kwanza kuwa na mabao mengi ndani misimu mitano.
Katika msimu uliopita straika wa JKT Tanzania, Edward Songo aliibuka mfungaji bora kwa mabao 18 ikiwa ni rekodi yake mfululizo misimu mitatu nyuma licha ya timu yake kutopanda hadi 2023/24.
Katika msimu wa 2017/18 aliyekuwa nyota wa JKT Tanzania, Hassan Mwaterema alitwaa tuzo ya mfungaji bora na mabao 16.
Msimu wa 2018/19, nyota wa Namungo (sasa Mashujaa), Reliant Lusajo alitwaa tuzo hiyo kwa mabao 16 na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu.
Kwa sasa Edgar anaingia kwenye rekodi mpya ya kutupia idadi kubwa ya mabao (20) wakiwa na mchezo mmoja.
Nyota huyo anaandika historia ya kupandisha timu ya pili kwake akianza na Mbeya Kwanza 2021/22 na sasa anarejesha heshima kwa Ken Gold.
Hata hivyo, Edgar alikutana na upinzani mkali kumkimbiza kwenye ufungaji mabao Boban Zirintusa wa Biashara United (19) na Maulid Shaban wa Mbeya City mwenye 15.
Kushuka daraja Ruvu Shooting kunafanya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuendelea kuitegemea Mbeya kuwasogezea uhondo wa Ligi Kuu. Ruvu Shooting ambayo iliuzwa Manispaa ya Iringa ili kukata kiu ya mashabiki na wadau wa soka kuwasogezea burudani, lakini kushuka kunarejesha huzuni.
Hadi sasa mikoa ya Iringa, Njombe, Katavi, Rukwa na Songwe haina timu za Championship wala Ligi Kuu, huku Ruvuma ikiiangalia FGA Talents inayodaiwa kununuliwa na mmoja ya vigogo.
Tayari timu hiyo iliyokuwa na makao yake jijini Dodoma, imeshahamia Songea na baadhi ya mechi zake za nyumbani imekipiga katika Uwanja wa Majimaji mjini humo.
Mbeya licha ya kuondokewa na Ihefu iliyouzwa na kubadilishwa kuwa Singida Black Stars na kuhamishiwa mjini Singida, inabaki na Tanzania Prisons na Ken Gold katika Ligi Kuu, huku Mbeya City ikiwa Champioship sawa na Mbeya Kwanza.