Chunya. Mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa, wamejitokeza kuuga mwili wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila maarufu kwa jina la Sauli (46), aliyefariki dunia kwa ajili ya gari Agosti 4, 2024.
Sauli ambaye ameacha wake watatu na watoto 16, alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya gari lake alilokuwa akiliendesha akitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya kugongwa na lori lililokuwa limebeba mchanga.
Sauli anazikwa leo saa 11 jioni katika makaburi ya kijijini kwao, Godima wilayani Chunya.
Miongoni mwa waliotoa salamu za pole wakati wa kuuaga mwili huo nyumbani kwake eneo la Kibaoni wilayani Chunya ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chunya, Noel Chiwanga, Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Barabara (Latra), Johansen Kahatano na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Latra, Kahatano amesema kifo cha Sauli ni pigo kwa sekta ya usafirishaji na amesisitiza kuwa wataendelea kuenzi mema yote aliyoyafanya katika sekta hiyo enzi ya uhai wake.
Amesema katika miaka mitano ya uwekezaji wake katika sekta hiyo, Sauli amekuwa mdau muhimu na ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya usafirishaji kuendelea kuifariji familia yake kwa kuendeleza mema aliyoyafanya ikiwamo ya kutoa ajira kwa vijana.
“Kwa niaba ya Bodi na Wakurugenzi wa Latra, tunatoa pole nyingi kwa familia. Sauli alikuwa mdau mkubwa wa uwekezaji na niombe tuendelee kuenzi yote mema aliyofanya enzi za uhai wake,” amesema Kahatano.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya, Bosco Mwanginde amesema wamepoteza mtu muhimu katika maendeleo ya wilaya kwa kuwa alikuwa akitoa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali.
“Hiki si kilio cha mtu mmoja, bali ni cha wana Chunya wote, kwa sababu alitoa nguvu zake za hali na mali kusaidia makundi na mtu mmoja mmoja kusukuma maendeleo,” amesema Mwanginde.
Mbunge Kasaka amesema Sauli alikuwa na ndoto nyingi za kuleta maendeleo Chunya, ikiwamo ya upatikanaji wa tenki la maji katika eneo la Kibaoni.
“Niwaombe watumiaji wa barabara kuongeza umakini kwa sababu tunaona athari nyingi zinazotokea, ikiwamo kumpoteza mpendwa wetu Sauli. Katika kuenzi ndoto zake, nitahakikisha tenki la maji na huduma hii inapatikana kwa wingi,” amesema Kasaka.
Isaya Edwine, mmoja wa wafanyabiashara waliofanya kazi na marehemu, alisifu ushirikiano wake katika kusukuma maendeleo ya Chunya na kueleza kuwa wachimbaji wamepoteza mtu muhimu.
“Alikuwa mpambanaji katika kupigania maisha na kusukuma maendeleo. Ameajiri vijana wengi katika maeneo mbalimbali, binafsi namkumbuka sana kwa jinsi tulivyoshirikiana,” amesema Edwine.
Kamanda Kuzaga, akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi, amesema wamesikitishwa na kifo cha Sauli kutokana na mchango wake.
Ameahidi Jeshi la Polisi litakuwa bega kwa bega na familia yake katika kipindi hiki kigumu.
“Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, naomba kuwasilisha salamu za pole. Tumeguswa sana na kifo hiki, tunakubali yaliyotokea huku tukibaki karibu na familia kwa kipindi hiki,” amesema Kamanda Kuzaga.
Joshua Mlambalala, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni amesema marehemu alioa wake watatu na kuacha watoto 16, wa kiume tisa na wa kike saba.
“Marehemu hakuondoka patupu. Katika uhai wake, ameoa wanawake watatu na kupata watoto 16, wavulana tisa na wasichana saba. Sauli alikuwa mtu wa watu, tunasikitika kumpoteza,” amesema Mlambalala.