Kesi ya unyang’anyi inayowakabili waliokuwa askari polisi yakwama Kisutu

Dar es Salaam. Serikali imeshindwa kuendelea na usikilizwaji katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh90 milioni inayowakabili watu watano wakiwamo waliokuwa askari polisi, kutokana na mshtakiwa mmoja kutokuwepo mahakamani.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa wa tatu, Stella Mashaka kutoletwa mahakamani akitokea mahabusu Segerea, jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 197/2023 ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba  F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo(42) maarufu kama Rasta na mkazi wa Kipawa; G 7513 D/Coplo Majid Abdallah(35) na mkazi wa Kunduchi na WP  6582 D/ Coplo Stella Mashaka( 41) mkazi wa Railway.

Wengine ni waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya RHG General Traders Ltd ambao ni Ashiraf Sango (31) na  Emmanuel Jimmy( 31), wote wakazi wa jiji hilo.

Leo Jumatano, Agosti 7, 2024 wakili wa Serikali Neema Moshi, ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswagwa kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini mshtakiwa mmoja hajaletwa mahakamani.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na leo tuna shahidi mmoja ambaye yupo mbele ya Mahakama yako, lakini kwa bahati mbaya mshtakiwa wa tatu katika kesi hii( Stella) hajaletwa mahakamani kutokana na changamoto za usafiri kutoka mahabusu ya Segerea,” amedai wakili Moshi.

Amedai kutokana na hali hiyo aliomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23, 2024 itakapoendelea na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana.

Awali, kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa Msajili wa mahakama hiyo.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023   Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji, zilizopo Wilaya ya Ilala.

Kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa kuiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.

Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.

Related Posts