Viwanja vya Kombe la Dunia Saudi Arabia ni kufuru

HIVI karibuni mamlaka za soka za Saudi Arabia ziliachia picha za viwanja 15 ambavyo vimepangwa kujengwa kwa ajili ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2034 na kwa sasa ndio nchi pekee iliyoomba kuandaa.

Picha mbalimbali zilionyesha viwanja bora vya kisasa vinavyoonekana vya kuvutia na kimoja kati ya hivyo kitakuwa kama kijiji.

Inaelezwa viwanja vipya vitakavyojengwa ni 11 kisha viwanja vinne vitafanyiwa marekebisho kufikia ubora wa hivyo 11.

Taarifa pia inaeleza viwanja hivyo vitajengwa katika miji minne ambayo ni Riyadh, Jeddah, Al Khobar na Abha.

Kwa mujibu wa The Times, licha ya ukweli hawajachaguliwa kuandaa michuano hiyo, kuna uwezekano mkubwa wakapewa kibali kwani mpango wa FIFA ni kupeleka mashindano hayo katika nchi za Kiarabu.

Wakati mamlaka zinaachia picha hizo na miundo kamili ya uwanja, mashirika ya kutetea haki za binadamu yameelezea wasiwasi wao juu ya ujenzi wa viwanja hivyo, huku kukiwa na hofu kutakuwa na unyanyasaji wa wahamiaji wengi watakaokwenda kufanya kazi ya kutengeneza viwanja hivyo kama ilivyokuwa kwa Qatar wakati wanaandaa michuano ya  Kombe la Dunia mwaka 2022.

Moja kati ya viwanja vikubwa zaidi na bora utajengwa huko jijini la Neom ambako bado hakujajengwa ingawa serikali ya nchi ipo katika mchakato wa kukuunda na kutakuwa na gari zitembeazo juu na mji utakuwa katika bahari.

Uwanja huo utakaopewa jina la  “uwanja wa kipekee zaidi duniani”, utajengwa mita 350 kutoka chini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa inaeleza: “Uwanja wa Neom utakuwa uwanja wa kipekee zaidi duniani. kwanza utajengwa mita 350 juu ya ardhi, mandhari ya kuvutia na utafunikwa na paa la jiji lenyewe.”

Kiwanja kingine kikali ni New Murabba, ambacho kitakuwa na muundo wa kutatanisha kwani ukiangalia kwa nje kitakuwa kinaonekana kama korongo bandia na miamba.

Uwanja huo wenye viti 45,000 utakuwa ni sehemu ya mpango wa maendeleo ya eneo la Murabba huko Riyadh.

Uwanja wa Michezo wa Jiji la Prince Faisal bin Fahd ni moja wapo ya viwanja vya kuvutia kwa mujibu wa picha zilizoachiwa.

Kwa mwonekano uwanja huo utapambwa na vitu mbalimbali vya asili, kale na urithi wa nchi hiyo.

Inaelezwa uwanja huo utajengwa kwa kutumia vifaa vya asili kabisa na hata umeme wake utatokana na nishati ya jua na itafungwa paneli kubwa zaidi za nishati ya jua.

Hata hivyo, uwanja unaoripotiwa kuvutia zaidi kuliko vyote utakuwa ni Uwanja wa King Salman wenye uwezo wa kuchukua watu 92,000 ambao utakuwa ndio uwanja mkubwa kuliko yote.

Uwanja huo umechukua eneo la mita za mraba 660,000, utatumika kama uwanja wa nyumbani wa timu ya taifa ya Saudia na utaandaa mechi ya ufunguzi na ya mwisho ya michuano hiyo.

Ndani ya uwanja huu kuna eneo VIP na VVIP, ambayo huenda yakatumika kukaliwa na wakuu wa nchi mbalimbali.

Uwanja wa kisasa utakuwa na maeneo maalumu ikiwa pamoja litakalokuwa kwa ajili ya mfalme na watu wake litakalokuwa na viti 150, kutakuwa na vyumba vya wageni 120, viti 300 vya VIP, na viti 2,200 kwa wageni mbalimbali wa hadhi ya juu.

Pia kutakuwa na maduka mbalimbali kwa ajili ya kununua vitu ili kuvutia watalii ama mashabiki wataotembelea eneo hilo.

Skrini nyingi kubwa pia zitawekwa ndani ya uwanja ili kusaidia watazamaji kuona vizuri zaidi kila tukio linaloendelea ndani humo.

Related Posts